Matobo manne yanayomtesa Barthez

Muktasari:

Katika msimu huo uliomalizika hivi karibuni ilikuwa kivumbi kuanzia kwa mastraika hadi kwa makipa.

MSIMU wa kimashindano katika soka la nchini umemalizika. Katika Ligi Kuu Bara Simba imefunga hesabu kwa ubingwa na kujitwalia tiketi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kwenye vumbi la FA, Mtibwa Sugar, ndio iliyofanya kweli na sasa itacheza Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika msimu huo uliomalizika hivi karibuni ilikuwa kivumbi kuanzia kwa mastraika hadi kwa makipa. Kati ya walinda milango walifanya vizuri ukiachana na Aishi Manula wa Simba, Razack Abalora (Azam), Benedict Tinocco (Mtibwa Sugar), mwingine utakayetakiwa kumtaja hapo lazima awe Ally Mustapha ‘Barthez’ wa Singida United.

Barthez, ambaye ni kipa mkongwe kati ya hao wote akizichezea pia Simba na Yanga hapo awali, anayo historia yake ndefu tu kwenye ligi hiyo, akipangua yaliyoonekana kuwa mabao kadhaa ya wazi na yapo pia yaliyomshinda akaishia kuufuata mpira wavuni.

Kwa muda wote ambao kipa huyo amecheza Ligi Kuu Bara, kafungwa mabao kadhaa, lakini kuna manne ambayo hakika hataweza kuyasahau. Unataka kuyajua ni mabao hayo? Tulia, ndio maana Mwanaspoti lipo kwa ajili yako.

KIKI YA OKWI (Machi 8,2015)

Wakati huo Barthez alikuwa Yanga. Baada ya kucheza na Simba mechi ya mzunguko wa kwanza Oktoba 18, 2014 na mechi kumalizika kwa sare ya bao 1-1, timu hizo zikarudiana Machi 8, 2015 na Yanga ya kipa huyo ikalala bao 1-0.

Huku mchezo ukiendelea na Simba ikionekana kujenga shambulizi kutokea mbali, Barthez akaingia mtegoni na kufanya kosa analolijutia hadi sasa. Alitoka golini na kusogea ndani ya uwanja na Emmanuel Okwi kama alivyotosha safari hii, alimcheki Barthez alivyotoka golini na fasta akajua la kufanya.

Akiwa karibu na katikati ya uwanja, akaupiga mpira kwa juu na jitihada za Barthez kukoa jahazi hazikuzaa matunda. Kipa huyu hatalisahau bao hilo kwani lilikuwa la maudhi makubwa kwake, lilimdhalilisha.

Ushindi huo uliipandisha Simba hadi nafasi ya tatu na msimu huo Okwi alimaliza msimu akifunga mara nne tu.

KONA YA KICHUYA

Barthez aliendelea kuteseka na mabao ya maudhi kutoka kwa mastraika wa Simba baada ya kufungwa bao la kona ya moja kwa moja, japo safari hii Msimbazi walikuwa wakisawazisha.

Ilikua Oktoba Mosi, 2016 katika mechi ya mzunguko wa kwanza. Bao hilo lilifungwa dakika ya 86 kwa kona iliyopigwa na Shiza Kichuya na hakika iliwashangaza wengi.

Kama kawaida yake, akitumia mguu wa kushoto, Kichuya, ambaye alikuwa ndio anaanza kujenga jina Simba baada ya kusajiliwa kutoka Mtibwa Sugar, hakuwa na papara. Kwanza aliushika mpira na kisha kuuweka vizuri. Akarudi nyuma hatua kama nne hivi na kuachia kiki ambayo Barthez aliishuhudia tu ikiwa nyavuni.

Bao hilo lilifungwa dakika nne kabla ya mchezo kumalizika huku Simba ikiwa pungufu baada ya Jonas Mkude kutolewa kwa kuonyeshwa kadi nyekundu baada ya kumzonga mwamuzi akilalamikia bao lililofungwa na Amissi Tambwe.

LA FAINALI YA FA

Ndio, safari hii akiwa na kikosi cha Singida United alitinga fainali ya Kombe la FA na walivaana na Mtibwa Sugar na walikubali kichapo cha mabao 3-2 katika fainali iliyochezwa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.

Katika fainali hiyo, kuna mabao mawili ambayo Barthez hataweza kuyasahau. Ni kwa kuwa yalijaa wavuni kwa kutumia makosa yake ya kujirudia. Dakika ya 21, kiungo Salumu Kihimbwa wa Mtibwa aliachia shuti kali baada ya kumchungulia Barthez aliyekuwa amesogea kidogo mbele ya lango, mpira huo uliopigwa kimahesabu ulienda moja kwa moja nyavuni. Ulikuwa udhalilishaji mwingine dhidi yake. Bao jingine katika mechi hii lilikuwa la kona ya moja kwa moja ambayo ilipigwa dakika ya 37 na beki wa kushoto wa Mtibwa, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’. Yalikuwa yale yale ya Kichuya.

Kwa wanaomchunguza vizuri Barthez, huwa anafungwa kirahisi mabao ya kona zinachongwa na wanaotumia mguu wa kushoto.Kichuya na Baba Ubaya wamethibitisha hili.