MATAWINI: Pablo arejesha mzuka Simba

Thursday November 25 2021
Simba PIC
By Daudi Elibahati

TUMEANZA ligi upya, hiyo ndiyo kauli ya wanachama wa Simba baada ya ushindi wa mabao 3-1, walioupata dhidi ya Ruvu Shooting katika uwanja wa CCM Kirumba.

Hayo yamesemwa na wanachama wa Simba tawi la New Mapambano kata ya Azimio lililopo Temeke Mwisho kwa kile walichodai kuanzia sasa wapinzani wao wataisoma namba.

Mwenyekiti wa tawi hilo, Albino Lwila alisema kuwa ushindi walioupata utaamsha ari ya wachezaji kupambana zaidi baada ya kuanza kwa kusuasua.

“Wengi wamekuwa wakitubeza lakini niwaambie tu kuwa ndio tumeanza kuonyesha Simba ni timu kubwa hivyo wakae kwa kutulia maana tunarejea kwenye nafasi yetu,” alisema.

Katibu Mkuu wa tawi hilo Nurdin Chodo alisema kuwa uzoefu wa Pablo unampa matumaini makubwa ya kufanya vizuri licha ya kutozoea mazingira ya Soka la Bongo.

Tawi Simba PIC
Advertisement

“Kadri tunavyozidi kupata matokeo ndio tunajiweka kwenye nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wetu kwa kuwa timu yetu imekuwa na desturi ya kila kocha anayekuja katikati anachukua ubingwa, hivyo nikifikiria hilo huwa naona pia Pablo atafuata nyayo za watangulizi wake,” alisema.

Mjumbe wa tawi hilo Said Kisoma alisema kitu ambacho Pablo anapaswa kukifanya ni kuwapa nafasi kila mchezaji kwa kuwa kila aliyepo kweye kikosi hicho ana kiwango kikubwa.

“Timu ina zaidi ya wachezaji 30 ni wakati wa kuwapa kila mmoja nafasi kwa sababu wengine wanapokosa mechi za kucheza kwa muda mrefu wanashindwa kujiamini na kutoka kwenye mstari,” alisema.

Naye Kassim Mtanga ambaye ni mjumbe kwenye tawi hilo alisema kilichowaangusha kwenye mechi za mwanzoni ni kutolewa katika michuano ya kimataifa ila wanaamini umoja waliokuwa nao utawarejesha katika hali ya kawaida.

“Viongozi wetu wanapaswa kupewa pongezi kwa utulivu na mshikamamo walioonyesha maana laiti wangekuwa hawa wenzetu muda huu tungekuwa tunaongea mengine,” alisema.

Tawi hili linaitwa Simba New Mapambano, lilianzishwa Mwaka 1978 lina wanachama 152, viongozi ni Mwenyekiti Albino Lwila, msaidizi wake ni Mohamed Soloka, Katibu Mkuu ni Nurdin Chodo, msaidizi ni Ally Mkumba, mtunza fedha ni Sosthenes Amasi.

Advertisement