MATAWINI: Mabadiliko Yanga yatolewa jicho makini

YANGA haitaki kukosea kabisa kufanya mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu hiyo kutoka kwenye mfumo wa uwanachama kwenda kwenye uwekezaji wa kugawana hisa kama ilivyo kwa klabu ya Simba.

Utofauti wa Yanga ni asilimia 49 zitagawanywa kwa wawekezaji watatu na asilimia 51 zitabakia kwa wanachama na tayari uongozi wa klabu hiyo umetoa elimu kwa viongozi wa matawi ili wakawaelimisha mashabiki kabla ya kufikia jambo lenyewe.

Mwanaspoti leo limetembelea tawi la Yanga la Kigogo Luhanga na limekutana na wanachama pamoja na viongozi wake ambao wamefunguka walivyopata elimu kuelekea mchakato huo na hawataki kufanya makosa kabisa na wanataka kila hatua izingatiwe.

Katibu wa tawi hilo, Zuber Ndali alisema baada ya viongozi wa matawi kukutana na viongozi wa klabu hiyo makao makuu Jangwani, walipewa elimu na baada ya hapo wakaa kikao wenyewe na kuchambua mchakato unavyokwenda wakagundua una manufaa kwao.

“Hatutaki mambo kama yaliowakutana Simba huko FCC, tunazingatia taratibu zote za kiserikali ili kila kitu kiende sawa kwa wakati sahihi, ili Yanga irejee kwenye makali yake na ndio maana unaambiwa kutangulia sio kufika, tunaweza tukaacha wanahangaika huko FCC,” alisema.

Kwa upande wa makamu mwenyekiti wa tawi hilo, Khamis Kindamba hakutaka kuzungumzia mambo ya mchakato, isipokuwa dukuduku lake ni kuwaambia Simba wasijitape wamewabeba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati bado hawajamaliza ligi ya ndani na ASFC .

“Bado hazijamalizika mechi za ligi kuu na Kombe la Shirikisho la Azam huenda tukawa mabingwa na tukajipeleka wenyewe huko Caf kwa hiyo Simba hawana haja ya kutembea kifua mbele eti wametubeba,” alisema.


SAFU YA UONGOZI YANGA

Mwenyekiti wa tawi hilo ni Nikodemas Ngonyoka, makamu wake ni Khamis Kindamba, katibu ni Zuber Ndali, msaidizi wake ni Jacqline Patrick na mtunza hazina Zainabu.

Tawi hilo lilianzishwa 2002 na lina wanachama 147.


Tutumie picha nzuri ya pamoja ya tawi lenu popote mlipo tutaichapisha kwenye ukurasa huu kila Jumatano. Tuma kwa namba 0658 376417