MATAWINI: Huku Mo Dewji, kule Manji

Thursday June 10 2021
tawi simba pic
By Clezencia Tryphone
By Olipa Assa

SIMBA wana jambo lao msimu huu, unataka kujua ni jambo gani!!, Mwanaspoti linakuletea uhondo wote kutoka kwenye tawi la Nyayo za Simba lililopo Kigogo Luhanga, jijini Dar es Salaam, lililofurahia ujio wa mwenyekiti wa zamani wa Yanga, Yusuf Manji.

Kama ilivyo ada ya Mwanaspoti kuwapa nafasi wanachama wa klabu za Simba na Yanga kuyatoa ya moyoni, awamu hii lilipiga kambi Kigogo ambako lilikutana na kioja hicho kwamba kwa ubora wa timu ya Msimbazi wanataka Manji arejee Jangwani akamwage mpunga wasajili kikosi cha ushindani.

Mjumbe wa kamati ya utendaji wa tawi hilo, Paul Rwambo alisema kutokana na aina ya ubora wa kikosi chao wanahitaji kukutana na Yanga bora, hivyo wanawashauri Yanga wampokee Manji ili awasaidie kwa jambo hilo.

“Kwanza tunataka kuchukua taji la ligi kuu na ASFC na fainali tukutane na Yanga na sasa tumenunua makufuli wakijifanya kukimbia kama siku ile tunafunga mageti hadi wacheze na ndio maana tunataka Manji arejee ili wawe na kikosi bora wasiwe wanakimbiakimbia;

Aliongeza “Tumewabeba msimu ujao watacheza Caf hivyo hatutaki wakatutie aibu kwa kuanza kulalamikia marefa maana kule kuna waamuzi wenye taaluma yao, hivyo Manji akirejea atafanya mambo hawatakuwa na ulalamishi tena, kwani Simba na Yanga ndizo zilizobeba taswira ya nchi,” alisema.

Ukiachana na hilo, alisema anashangazwa kuona mashabiki wa Yanga kila anapocheza winga Benard Morrison na akafanya vizuri wanaanza kuleta chuki, hivyo alisema Manji akirejea atawaondolewa kulialia na wataanza kucheza soka la ushindani ambao utaleta taswira nzuri.

Advertisement

“Soka linahitaji pesa, wakidhani sisi tunamwogopa Manji wanakuwa wanajidanganya kabisa, ndio maana unakuta mambo ya kulialia Simba kwa sasa hayapo kwa sababu Mo Dewji kafanya mambo, tunawatakia mabadiliko mema ili tucheza soka la ushindani, leo hii Simba haiwezi kuchukua mchezaji yoyote Yanga ambaye hataendana na ubora wa kikosi chetu, zaidi wao wachukue wanaokaa benchi kwetu na watawabadilishia timu yao,” alisema.


SAFU YA UONGOZI

Mwenyekiti ni Kisagase Athuman, Katibu ni Athuman Mdaka, mtunza hazina Anna Kileo na mmoja wa wajumbe ni Paul Rwambo, Meshack Kamota.

Tawi hilo lilianzishwa mwaka 2020 na lina wanachama zaidi ya 50.


Tutumie picha nzuri ya pamoja ya tawi lenu popote mlipo tutaichapisha kwenye ukurasa huu kila Jumatano. Tuma kwa namba 0658 376417

Advertisement