Matampi: Bingwa CAF anayekiwasha Coastal Union

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Uwepo wa Matampi langoni kwa Coastal umeifanya timu hiyo kuwa imara kwenye ulinzi ikiwa nafasi ya pili kwa timu zilizoruhusu mabao machache ikifungwa 15 tu nyuma ya vinara Yanga iliyofungwa 11 hadi sasa.

PALE kikosini Coastal Union kuna mchezaji anaitwa Ley Matampi, mkali aliyesafiri kutoka Mji Mkuu wa DR Congo, Kinshasa wa matajiri hadi mwambao wa bahari, Tanga. jiji la mahaba, kusaka ugali kupitia soka.

Matampi ni kipa mwenye wasifu na uzoefu mkubwa katika soka la Afrika akiwa na medali ya ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika alioupata akiwa na TP Mazembe mwaka 2017 baada ya kuwaondosha Supersports United ya Afrika Kusini kwenye fainali kwa jumla ya mabao 2-1.

Fainali ya kwanza ilipigwa Afrika Kusini na kumalizika kwa suluhu, hapo Matampi alikuwa benchi hakucheza lakini fainali ya pili iliyopigwa DR Congo mwamba alianza na kuipa ushindi timu yake wa mabao 2-1.

Kipindi hicho langoni kwa Supersport alikuwepo Ronwen Williams ambaye Jumamosi hii atakuwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kikosi cha Mamelodi Sundowns kuikabili Yanga.

Siku zimepita. Sasa Matampi yupo kwa Wagosi wa Kaya, Coastal Union na makala haya yanakupa fursa ya kumfahamu vyema mkali huyo kutoka DR Congo.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

WASIFU UMESHIBA

Matampi kwa soka la Afrika ni mwamba kwani amecheza kwa mafanikio TP Mazembe, pia ameichezea mechi kibao timu ya taifa ya DR Congo kwa misimu tofauti.

Ukiachana na Mazembe, Matampi pia amewahi kuzichezea DC Motema Pembe, FC Renaissance JS Group Bazano za nchini kwao sambamba na Kabuscorp SC do Palanca ya Angola na ya Saudi Arabia na sasa Coastal.

Wasifu mkubwa ameupatia Mazembe alipocheza kwa mara ya kwanza kuanzia mwaka 2011 hadi 2014 kabla ya kuondoka na baadaye kurudi 2017 na kucheza kwa mwaka mmoja na kutimkia uarabuni.

SAMATTA HADI NGUSHI

Matampi alisajiliwa Mazembe wakati mmoja na nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya PAOK Salonika ya Uturuki.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Wamecheza pamoja kwa miaka minne kabla ya Matampi kumwacha Samatta na kutimkia Kabuscorp ya Angola lakini miaka miwili mbele Samatta naye aliuzwa kwenda KRC Genk ya Ubelgiji.

Wakati Samatta yuko Mazembe wawili hao walikuwa wachezaji tegemeo kikosini hapo kwa maeneo tofauti na Matampi alikuwa langoni na Samatta akiwasha katika ushambuliaji.

Mambo yamebadilika tena, Samatta ni tegemeo Ulaya lakini Matampi ni tegemeo Coastal Union na mastraika wake tegemeo ni Crispin Ngushi na Salim Aiyee.

DIARRA, AYOUB WANASUBIRI

Ukiangalia msimamo wa makipa wanaoongoza kwa hati safi (clean sheets) kwenye Ligi Kuu Bara, jina la mwamba huyu ndilo lipo juu.

Matampi hadi sasa ana jumla ya clean sheets 10 katika mechi 21 za ligi ilizocheza Coastal hadi sasa chini yake akiwepo Djigui Diarra wa Yanga mwenye nane kisha Costantine Deusdedith wa Geita Gold na John Nobel wa Tabora United kila mmoja akiwa nazo saba.

Ayoub Lakred wa Simba anazo tano sawa na Ramadhan Chalamanda wa Kagera Sugar wakiwa chini ya Jonathan Nahimana wa Namungo na Yona Amosi wa Tanzania Prisons kila mmoja akiwa nazo sita.

Matampi ndiye kipa mwenye umri mkubwa zaidi (34) anayedaka kikosi cha kwanza kwenye Ligi Kuu Bara hadi sasa, umri sawa na Deugratius Munishi anayesugua benchi Namungo.

KUIPELEKA COASTAL CAF

Pamoja na kuwa timu maarufu na ya muda mrefu nchini, Coastal Union haijawahi kufanya vizuri kwenye michuano ya CAF.

Mara ya mwisho Coastal kushiriki michuano ya CAF ilikuwa mwaka 1989 katika Kombe la Washindi na kuishia hatua ya kwanza baada ya hapo wamekuwa watazamaji tu.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Msimu huu ujao Tanzania itaingiza timu nne kwenye michuano ya CAF kwa maana ya timu mbili kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na mbili katika Kombe la Shirikisho na Coastal inaonekana kuziwania nafasi hizo.

Kwa sasa timu hiyo ipo nafasi ya nne katika ligi ikiwa na alama 30 nyuma ya vinara Yanga inayoongoza na pointi 52, Azam yenye 47 na Simba yenye 45 huku nyuma yake zikiwepo Tanzania Prisons na KMC zenye alama 28 kila moja.

Uwepo wa Matampi langoni kwa Coastal umeifanya timu hiyo kuwa imara kwenye ulinzi ikiwa nafasi ya pili kwa timu zilizoruhusu mabao machache ikifungwa 15 tu nyuma ya vinara Yanga iliyofungwa 11 hadi sasa.

Kama ataendelea kuilinda vyema ngome ya Wagosi wa Kaya hao na timu ikapata matokeo yatakayoifanya kumaliza ndani ya nafasi nne za juu basi anaweza kuandika historia ya kuwa miongoni mwa mastaa walioirudisha timu hiyo kwenye michuano ya CAF baada ya muda mrefu kupita.