Mastaa Yanga: Tuachieni Mwambusi

MASTAA wa zamani wa Yanga na klabu kongwe za Tanzania, wameusisitiza uongozi wa klabu hiyo kukomaa na Juma Mwambusi mpaka mwisho wa msimu na kuacha kubabaika na wageni.

Wanaamini kama Kocha huyo wa zamani wa Mbeya City, Prisons na Azam atapewa utulivu wa kutosha akaingiza mambo yake kikosi basi Yanga itakuwa na pumzi na fiziki ya hatari ambayo itawasaidia kumalizia ligi kicheko.

Beki wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Bakari Malima alisema Mwambusi akipewa sapoti ya kutosha kuna mambo atayabadilisha kwa wachezaji ikiwemo kucheza kwa pumzi na ufiti ndani ya dakika 90, vitu alivyoviona vilikosekana kwa Cedrick Kaze aliyetimuliwa.

“Wamwache Mwambusi amalize msimu kwani wakimleta kocha mpya, atakula pesa zao tu, akikosa ubingwa atakuwa na kisingizio hajasajili timu, mashabiki na viongozi tuungane tuwe kitu kimoja kumpa moyo kocha, pia apewe mahitaji yake yote,” alisema Malima ambaye ni miongoni mwa wachezaji waliojenga jina Yanga.

“Hadi sasa hakuna mwenyewe kwenye ubingwa lolote linawezekana, tofauti na baadhi wanaoipa nafasi zaidi Simba, Mwambusi atarejesha fiziki na pumzi kwa wachezaji, angalau kwenye mechi zao tutaona kupambana ingawa inaweza isifike asilimia kubwa, hivyo amalize msimu ndipo waanze kumsaka kocha atakayeanza na timu,” alisema staa huyo huku Yanga ikitarajiwa kurejea kambini na Mwambusi ijumaa hii kujiandaa na mechi ya Prisons.

Yanga wamemtangaza Mwambusi atakaa na kikosi hicho mpaka mwisho wa msimu ingawa Mwanaspoti linajua wameshamalizana na Mfaransa, Sebastian Migne ambaye atatua nchini muda wowote kuanzia sasa kusoma kikosi na atashauri pia ishu za kiufundi kwenye mechi za kuelekea mwisho wa msimu.

Staa wa zamani wa Mecco ya Mbeya, Abeid Kasabalala alisema Yanga chini ya Mwambusi anaitarajia ibadilike katika mambo mawili aliyoyataja kuwa kuitengeneza timu na fiziki, lakini kwa sharti la viongozi kumtimizia anachostahili na muda wa kufanya hayo.

Kasabalala alisema pamoja na Mwambusi kuwa kocha mzuri, mashabiki wasitarajie kuona makubwa katika mechi za hivi karibuni zaidi watashuhudia uwezo wa mchezaji mmoja mmoja kama vile ilivyokuwa kwa kocha aliyeondoka Kaze ambaye alijaribu kutengeneza timu.

“Yanga inahitaji muda kutengenezwa, lazima mashabiki waambiwe ukweli ili Mwambusi asije akafanya kazi kwenye mazingira magumu na wakaanza kumchukia kama ilivyokuwa kwa Kaze ambaye naye asingeondoshwa mapema kwani alijaribu kukitengeneza kikosi, taaluma isiendeshwe na mihemko hatuwezi kufika,” alisema.

Naye kocha wa Pan African, Godian Mapango aliunga mkono hoja ya Malima, anamwamini Mwambusi kubeba jukumu la kumaliza msimu salama na ana uzoefu na Yanga na Ligi Kuu Bara kwa jumla.

“Shida ya mashabiki wengi wanatembea na matokeo mfukoni, lakini hadi sasa hakuna anayeweza kujihakikishia ubingwa, Mwambusi aungwe mkono ili afanye kazi yake vizuri, naamini wachezaji watakuwa na fiziki na pumzi ya kutosha kutokana na aina yake ya mazoezi,” alisema.

Kiungo mahiri wa Yanga, Mukoko Tonombe aliliambia Mwanaspoti ana imani na Mwambusi na wachezaji wakizidisha morali pamoja na uongozi kuwa karibu nao zaidi ana uhakika timu hiyo itamaliza pazuri kwenye michuano ya FA na Ligi Kuu Bara.

Yanga wanaongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara wakiwa na pointi 50 na ndiyo klabu ambayo haijapoteza mechi yoyote tangu msimu huu uanze.