Mastaa Yanga kama Ulaya

Muktasari:

  • Cristiano Ronaldo ‘CR7’, Lionel Messi, Neymar  na hata Kylian Mbappe wamekuwa wakivaa viatu maalumu na hata soksi zikiwatofautisha na wengine kupitia wadhamini binafsi na hata wale wa klabu wanazozitumikia, lakini sasa unaambiwa kwa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga mastaa wake nao wamejitofautisha.

KWA wachezaji nyota wa soka katika baadhi ya klabu barani Ulaya sio ajabu kukuta wakivaa soksi na hata viatu vikiwa na majina au sura zao mbali na bendera za mataifa watokapo kama kuwatofautisha na wengine.

Cristiano Ronaldo ‘CR7’, Lionel Messi, Neymar  na hata Kylian Mbappe wamekuwa wakivaa viatu maalumu na hata soksi zikiwatofautisha na wengine kupitia wadhamini binafsi na hata wale wa klabu wanazozitumikia, lakini sasa unaambiwa kwa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga mastaa wake nao wamejitofautisha.

Baadhi ya nyota wa timu hiyo inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa sasa ikiwa na pointi 62 kupitia mechi 24 wameibuka kwa kiuvaa soksi zinazowatofautisha zikiwa na bendera za nchi wanazotoka bila kujali kama ni Watanzania au ni wale wa kigeni.

Mwanaspoti limefanya utafiti kwa mastaa wa Yanga, limegundua namna wanavyoishi kistaa, ipo hivi kila mchezaji ameweka nembo kwenye soksi zake, hivyo hakuna anayeweza kuingiliana na mwingine.

Asilimia kubwa za soksi za mastaa hao, zimechorwa nembo za bendera za nchi zao, kama kuwaonyesha utambulisho wa walipotokea.

Picha ambazo gazeti la Mwanaspoti ziliwanasa mastaa hao ni  za mastaa kutoka Uganda, Afrika Kusini, Zambia, Burkina Faso, Ivory Coast na Tanzania na  baadhi yao, walilizungumzia hilo, kubwa zaidi ni kujivunia utaifa wao.

Mechi ya Ligi Kuu Bara ya Aprili 24, JKT Tanzania ikiwa mwenyeji wa Yanga, ikimalizika kwa suluhu, mas-taa wa wanajangwani wengi walionekana wakiwa na soksi za nembo za nchi zao.

Baadhi ya mastaa hao ni  kama Khalid Aucho, Mahlatse Makudubela, Bakari Mwamnyeto, Gift Fredy, Kibwana Shomari na Stephane Aziz Ki na wenyewe wamefichua mchongo mzima ulivyo.


AUCHO-UGANDA

Kiungo wa timu hiyo, Khalid Aucho alisema kuchora bendera ya nchi yake kwenye soksi ni kama fash-eni, pia kujivunia utaifa wake.

“Ninajivunia taifa langu la Uganda ndio maana nimeweka bendera inayonionyesha natokea wapi, licha ya kuwa fasheni ningeweza kuchora kitu kingine, ila bendera ndio kitu kilichonifurahisha zaidi,” alisema na kuongeza;

“Unaweza ukaprinti mwenyewe ama ukaongea na mtu wa klabu, tupo wachezaji wengi ambao tu-mechora bendera ya nchi zetu na siyo lazima hilo, unaweza ukachora kitu kinachokufurahisha.”

Alisema wachezaji wenzake aliowaona wamechora bendera ya nchi zao ni Mwamnyeto, Mahlatse Ma-kudubela ‘Skudu’, Gift Fredy, Kennedy Musonda, Kibwana Shomari, Joseph Guede, Aziz Ki ambao Ka-mera ya Mwanaspoti pia iliwanasa wakiwa na soksi hizo maalumu.


KIBWANA-TANZANIA

Alisema kitendo cha kuchora bendera kwenye soksi zake, anajisikia fahari kuwa Mtanzania, “Ningeweza kuchora kitu chochote, ila nimejisikia kuchora bendera ya nchi yangu.

Aliongeza “Kuna rafiki yangu ambaye aliniambia ananichorea bure, lakini tupo wachezaji wengi ambao tumefanya hivyo, pia inasaidia mtu asijichanganye kuchukua soksi zangu.”

Alisema kila soksi ya mchezaji ina nembo, wapo waliochora vitu vingine vinavyowafurahisha zaidi.