Mastaa wote Polisi kupigwa nyungu

Muktasari:
Watanzania wengi wameamua kurejea katika tamaduni zao za zamani za tiba asilia kama kujifukiza ili kuepukana na ugonjwa wa Covid 19.
NYUNGU imekuwa habari ya mjini kwa sasa na sasa wakati wachezaji wa klabu ya Polisi Tanzania inayoshiriki Ligi Kuu Bara, wakitarajiwa kuanza kurejea kambini watakutana na kitu ambacho hawajahi kukutana nacho hapo awali.
Ndio, mpango mzima ni kuwa wachezaji hao kabla ya kuanza mikiki mikiki ya kurejea kwa Ligi Kuu Bara hapo Juni Mosi, 2020, watajifukiza ikiwa ni mkakati wa kukabiliana na virusi vya corona.
Hivi karibuni Rais John Pombe Magufuli akiwataka Watanzania kurejea tiba za asili kwa kujifukiza ili kukabiliana na janga hilo, ambapo Waziri mwenye dhamana na michezo, Dk Harrison Mwakyembe alionyesha mfano wa kujifukiza kupitia video katika mtandao wake wa kijamii ' Instagram'
Akizungumza na Mwanaspoti leo Jumapili Mwenyekiti wa Polisi Tanzania, Robert Munis amesema baada ya wachezaji wao kurejea kambini watajifukiza wote ikiwa ni njia ya kujikinga na ugonjwa wa Covid 19.
Amesema mbali na kupiga nyungu, pia watawapima virusi hivyo ili kujiridhisha kabla kuanza kampeni za kumaliza mechi za ligi zilizobaki.
"Tutawapima joto kwanza na vipimo vingine na baada ya hapo tunawapiga nyungu kisha kila kitu kitaanza kwenda sawa, tunafuata maelekezo ya serikali na wataalamu wa afya kabla na baada ya kukusanyika," amesema.
Amesisitiza kwamba wachezaji wote ni lazima wazingatie muda wa kuingia kambini ili kuanza ratiba ya mazoezi wakati wakisubiri miongozo mingine.
Kuhusu wachezaji kulala kambini, Munis amesema hakuna shaka kwa kuwa wana vyumba vya kutosha kwenye Chuo cha Polisi Moshi na kwamba, kila mchezaji atalazimika kukaa chumba cha peke yake.
“Tuna eneo kubwa, uwezo wa kila mchezaji kukaa chumba chake tunao, sisi tunafuata taratibu za wataalamu wa afya na viongozi wetu wa serikali,” amesema.
Polisi Tanzania inashika nafasi ya sita ikijivunia pointi 45 baada ya kushuka dimbani mara 29 huku wakishinda michezo 13, sare sita na kupoteza michezo 10.