Mastaa waingilia usajili Yanga, wamtaja Kelvin Yondani!

Muktasari:

WAKONGWE wa klabu ya Yanga wameona kasi ya usajili iliyoanza klabuni hapo wakaibuka na kutoa angalizo kwa viongozi. Tayari Yanga imeshasainisha wachezaji wawili wa kigeni kutoka DR Congo mmoja wao akiwa veki wa AS Vita, Shaban Djuma na Mercey Vumbi.

WAKONGWE wa klabu ya Yanga wameona kasi ya usajili iliyoanza klabuni hapo wakaibuka na kutoa angalizo kwa viongozi. Tayari Yanga imeshasainisha wachezaji wawili wa kigeni kutoka DR Congo mmoja wao akiwa veki wa AS Vita, Shaban Djuma na Mercey Vumbi.

Straika wa zamani wa Yanga, Makumbi Juma ‘Homa ya Jiji’ alisema wakati wanaangalia wachezaji wa kuachwa hasa upande wa wageni, kamati hiyo inatakiwa kumtazama Haruna Niyonzima kwa jicho la ufundi na sio kumchoka kwa kukaa naye muda mrefu bila kujali kipaji chake.

Alitoa sababu ya kwanini Niyonzima bado ni muhimu ndani ya kikosi hicho,kuwa hana papara kuisambaza mipira ya upendo eneo la kati, mzoefu, anaijua mifumo ya Yanga na bado ana kiwango cha juu endapo kama atachezeshwa mara kwa mara.

“Kuna wachezaji waliachwa kwa mkupuo ndani ya Yanga, lakini imeonekana bado walikuwa wanahitajika, ninachokiona kwa Niyonzima hawaangalii nini anakifanya akiwa uwanjani, bali wanachukulia mazoea kwa kumuona muda mrefu, sasa huo sio mpira, mchezaji hawezi kuwa vizuri kama hachezeshwi mara kwa mara, kwani kadri anavyocheza ndivyo anavyozidi kujiamini na kuwa bora;

“Zamani mchezaji alikuwa anakaa na timu moja kwa miaka 10 na ndio maana tulikuwa na kombinesheni imara kwasababu tulipata muda wa kuzoeana na ushindani ulikuwa mkali, hii ya kuacha wachezaji kila msimu haijengi kabisa, lazima uwepo muda wa wachezaji kuzoeana, ukiachana na hilo timu iingie kwenye mfumo wa kisasa,”alisema staa.

Mbali Niyonzima, eneo lingine aliloona linatakiwa kulindwa ni la wachezaji vijana watakaobeba taswira ya uzalendo ndani ya timu hiyo akiwataja baadhi kama Dickson Job, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Kibwana Shomari na Feisal Salum ‘Fei Toto’ kwamba wakiendeleza watafanya makubwa.

Beki wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Bakari Malima alisema kama kuna umakini unatakiwa kufanywa na kamati ya usajili ni kuleta wachezaji wenye viwango sahihi na sio vya maigizo.

“Mfano kama wanamuacha Niyonzima wanatakiwa walete mwenye uwezo zaidi yake nje na hapo watakuwa wanawakosea mamilioni ya mashabiki wa Yanga ambao wanahitaji furaha ya kudumu msimu

“Sio mchezaji ameonekana mechi moja akicheza na Stars na Malawi wanataka kumchukua na kwa upande wa wazawa wameisumbua Simba, Yanga wanataka kumsajili, lazima skauti zao zifanye kazi kumsajili mchezaji mwenye uwezo wa uhakika sio kubahatisha, mfano walimtoa Kelvin Yondani je pengo lake limezibika, angalau usajili wa Shaban Juma unaona atakuja kufanya kitu,”alisema Malima huku akisapotiwa na wadau wengine waliohojiwa na Mwanaspoti.

Yanga imepanga kufanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi chao kwa kusajili mastaa wapya nane ambao kwa mujibu wa viongozi ndio mapendekezo ya Kocha Nabi. Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema kuwa miongoni mwa hao wanaotakiwa kuna nafasi ya kipa namba moja wa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.