Mastaa Simba washangilia kambini kuisoma Yanga ikipigwa

BENCHI la Ufundi la timu ya Simba limekitazama kikosi kinachoendelea kujifua jijini Arusha na kuona jambo moja huu ni wakati wa kutamba kwa Chris Mugalu.

Tangu kuanza kwa mazoezi ya Arusha, Mugalu amekuwa akifanyishwa mazoezi mazito na walimu wake; Didier Gomez na mwalimu wa mazoezi ya viungo, Adel Zarane, kwenye kuhakikisha kwamba anakuwa katika utimamu wa kutosha kimwili kuanzia mwanzoni mwa msimu.

“Mugalu alikuja Simba akiwa majeruhi na hakuweza kuanza mechi nyingi. Lakini mara alipoanza kuwa fiti, alikuwa tishio na alifunga magoli 14 kwenye Ligi Kuu ya Tanzania. Kwa mchezaji mgeni kwenye ligi yetu, hiyo ni idadi kubwa ya mabao,” chanzo cha MwanaSpoti kimeeleza.

Chanzo hicho makini cha gazeti hili kimeeleza kwamba benchi la ufundi la Simba lina matarajio makubwa kwamba Mugalu anaweza kufunga walau magoli 20 kwenye msimu au hata kufikia rekodi ya Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ ya kufunga mabao 27 kwenye msimu mmoja wa ligi.

“Fikiria tu kwamba msimu uliopita, Mugalu hakuwa akifahamiana na wenzake na hawakujua mikimbio yake wala wapi hasa anataka mpira uwekwe ili afanye yake. Sasa wenzake wameanza kumfahamu. Anachohitaji ni kuwa fiti tu na mengine yatakaa kwenye mstari,” kilisema chanzo hicho.

MwanaSpoti limeambiwa pia kwamba Mugalu mwenyewe amejiwekea ratiba ngumu ya mazoezi ambapo kwanza hufanya na wenzake asubuhi uwanjani na baada ya kupata kifungua kinywa, huingia gym kwa ajili ya mazoezi binafsi.

Kabla ya mazoezi kuanza, mara nyingi Mugalu hukimbia kwa kuzunguka uwanja kwa takribani raundi 20 na baada ya hapo ndio huenda kujiunga na wenzake kwenye mazoezi ya timu nzima.

Mugalu pia anatarajiwa kufanya makubwa kwa sababu anazungumza lugha nne; Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa na Kilingala, hivyo anaweza kuwasiliana bila matatizo na karibu wachezaji wote waliopo Simba kwa sasa.