Mastaa Prisons wampagawisha Adolf unaambiwa

Muktasari:

  • Akizungunza jijini hapa kocha huyo alisema tangu apewe majukumu ya kuiongoza Prisons anaona mabadiliko ambayo kimsingi yanampa matumaini ya kukwepa kushuka daraja kutokana na vijana wake wanavyopambana.

Mwanza.LICHA ya Prisons kuwa katika nafasi mbaya katika msimamo wa Ligi Kuu, Kocha wake, Mohamed Rishard ‘Adolf’ amefunguka mwenendo walionao hivi sasa haoni kinachoweza kuwashusha daraja.

Kocha huyo mpya ambaye ameiongoza Prisons katika mechi tatu,ameisaidia kuvuna pointi nne na kuitoa mkiani na kupanda hadi nafasi ya 19 ikiwa na alama 16 sawa na African Lyon lakini zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.

Akizungunza jijini hapa kocha huyo alisema tangu apewe majukumu ya kuiongoza Prisons anaona mabadiliko ambayo kimsingi yanampa matumaini ya kukwepa kushuka daraja kutokana na vijana wake wanavyopambana.

Rishard alisema hata hivyo, timu hiyo haikuwa vibaya kiufundi, isipokuwa ilikosa bahati katika kupata matokeo mazuri. Jambo ambalo kwa sasa anaona wazi mambo yanapendeza.

“Mapungufu yapo lakini pia kuna mengine mazuri kwahiyo naangalia kipi nikiongeze na nipunguze nini. Ila kwa jumla timu ipo vizuri na ishu ya kushuka daraja haipo, vijana wanabadilika,” alisema Rishard.

Kocha huyo aliongeza mkakati wake mbali ni kurekebisha safu ya ushambuliaji ambayo ndio inahusika na ufungaji mabao lakini atafanyia kazi maeneo mengine ili kufikia malengo yao.

Aliwataka mashabiki wa timu hiyo kutokata tamaa isipokuwa waendelee kuiunga mkono na kuwatoa hofu kuwa Prisons itabaki Ligi Kuu msimu ujao tena kwenye nafasi nzuri.

“Sehemu nitakayofanyia marekebisho hasa ni ushambuliaji japokuwa wachezaji wote nitawapa maelekezo ili kufikia malengo yetu. Lakini mashabiki wasikate tamaa,timu lazima ibaki Ligi Kuu,” alisema kocha huyo.