Mastaa 21 Yanga, Simba mtegoni

Muktasari:

  • Fainali za Afcon zitafanyika mwakani nchini Cameroon ambapo zitashirikisha jumla ya timu za taifa 24 ambazo zitagawanywa katika makundi sita yenye timu nne kila moja

Wachezaji 21 wa Simba na Yanga leo na kesho watakuwa na kibarua kigumu cha kuhakikisha wanaweka hai matumaini ya timu zao za taifa kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) pale zitakaposhuka uwanjani katika mechi zitakazochezwa katika nchi tofauti barani Afrika.

Ushindani uliopo kwenye makundi ambayo timu zao za Taifa zipo katika harakati za kuwania tiketi ya kwenda Cameroon mwakani, unawalazimisha nyota hao leo kupambana kwa machozi, jasho na damu kuzitafutia ushindi timu zao vinginevyo zinaweza kujikuta zikikosa rasmi nafasi kwenye fainali zijazo za Afcon ikiwa zitapoteza mechi za leo na baadhi kutoka sare.

Jijini Malabo, Guinea ya Ikweta, nyota 15 wa Simba na Yanga watakuwa na jukumu zito la kuhakikisha Taifa Stars inaibuka na ushindi wa ugenini dhidi ya wenyeji wao ambao utaifanya ifikishe pointi saba na kusogea hadi nafasi ya pili katika J linaloongozwa na Tunisia yenye pointi 10 ambayo tayari imeshakata tiketi ya kushiriki Afcon mwakani.

Ikiwa itapata ushindi, Stars itahitajika kuifunga Libya katika mchezo wa mwisho nyumbani, Machi 28 ili ifuzu lakini ikiwa itatoka sare leo, timu ya Taifa ya Tanzania itatakiwa kupata ushindi katika mechi ya mwisho dhidi ya Libya na kuombea Guinea ya Ikweta ifungwe au itoke sare na Tunisia kwenye mechi ya mwisho ili yenyewe ifuzu.

Lakini Stars ikipoteza mechi ya leo, ndoto za kushiriki Afcon mwakani zitakufa rasmi kwani haitoweza kufikia pointi 10 ambazo Guinea ya Ikweta itafikisha hata kama itapata ushindi katika mchezo wa mwisho dhidi ya Libya.

Wachezaji hao 15 waliopo katika kikosi cha Stars kitakachocheza mechi hiyo itakayoanza saa 4.00 usiku kwa muda wa Afrika Mashariki kwenye Uwanja wa Malabo ni makipa Metacha Mnata na Aishi Manula, mabeki Bakari Mwamnyeto, Yassin Mustapha, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Erasto Nyoni na Kennedy Wilson.

Viungo ni Hassan Dilunga, Feisal Salum, Mzamiru Yassin, Jonas Mkude na Deus Kaseke wakati washambuliaji ni John Bocco na Farid Musa.

Kiungo wa Yanga, Mukoko Tonombe yeye leo atakuwa kibaruani kuiwakilisha DR Congo itakapocheza ugenini dhidi ya Gabon.

Ikiwa DR Congo itapoteza mechi hiyo, inaweza kukosa rasmi tiketi ya kwenda Cameroon iwapo Gambia nayo itashinda nyumbani dhidi ya Angola.

Kule Kenya, beki wa Simba, Joash Onyango atakuwa na jukumu zito la kuhakikisha timu yao ya Taifa inaibuka na ushindi dhidi ya Misri ili wabaki angalau na matumaini kidgo ya kwenda Afcon kwani watafikisha pointi tano na kushika nafasi ya tatu kwenye kundi G lakini kama wakipoteza au kutoka sare, ndoto zao zitazimwa rasmi.

Nyota watatu wa Simba, Rally Bwalya, Clatous Chama na Peter Muduwa wao leo watakuwa kibaruani kuziwakilisha Zimbabwe na Zambia katika michezo ya kundi H.

Zambia yenye Chama na Bwalya, inatahitajika kushinda nyumbani dhidi ya Algeria leo ili iweke hai matumaini ya kufuzu kwani itafikisha pointi saba lakini ikiwa itapoteza, inaweza kukosa rasmi tiketi ya Afcon mwakani iwapo mojawapo kati ya Zimbabwe anayochezea Muduwa na Botswana itashinda katika mechi yao inayochezwa huko Francistown, Botswana.

Kesho, mshambuliaji wa Yanga, Saido Ntibazokinza atakuwa na kibarua cha kuiwakilisha timu yake ya taifa ya Burudni itakayokuwa nyumbani kuikaribisha Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Burundi wanahitajika kupata ushindi katika mchezo huo lakini ikiwa watafungwa na Mauritania ikapata ushindi nyumbani dhidi ya Morocco, itashindwa kufuzu Afcon.