Mastaa 20 Simba tayari kuivaa Ahly

Muktasari:

  • Simba na Al Ahly katika miaka ya hivi karibuni zimekutana mara sita kwenye michuano ya CAF ambapo kila timu imeshinda mechi mbili ilizokuwa nyumbani, na kutoa sare mbili mfululizo katika mechi mbili za mwisho za mashindano mapya ya African Football League (AFL) mwaka jana ilianza sare ya mabao 2-2 kwa Mkapa kisha 1-1, Misri.

JIONI ya leo Simba imefanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa tayari kwa mchezo wa mkondo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri utakaopigwa kesho Machi 29, kuanzia saa 3:00 usiku uwanjani hapo.

Timu hiyo inayoongozwa na kocha Mualgeria, Abdelhack Benchikha imefanya mazoezi hayo ikiwa na kikosi cha wachezaji 20, wakiwamo watano kati ya sita waliokuwa katika timu zao za taifa huku kipa Aishi Manula akikosekana kutokana na majeraha.

Nyota, Mzambia Clatous Chama, Mrundi Saidi Ntibanzokiza 'Saido', na Watanzania Kibu Denis, Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr' na  Kennedy Juma waliokuwa kwenye timu zao za taifa wamefanya mazoezi hayo sambamba na wengine.

Ally Salim, Ayoub Lakered, Israel Mwenda, David Kameta, Hussein Bakari, Henock Inonga, Che Malone Fondoh, Babacar Sarr, Mzamiru Yassin, Sadio Kanoute, Fabrice Ngoma, Pa Omary Jobe, Freddy Michael, Willy Onana na Hussein Abel walikamilisha idadi ya wachezaji 20 kwenye kikosi hicho.

Katika mazoezi hayo benchi la ufundi chini ya Benchikha na wasaidizi wake Farid Zemiti na Seleman Matola walikuwa wakielekeza mbinu mbalimbali kwa wachezaji wa Simba ambao walikuwa makini kusikiliza na kutenda.

Baada ya mechi ya kesho, timu zote zitasafiri hadi Cairo, Misri kwaajili ya mechi ya marudiano itakayopigwa Aprili 5, nchini humo na mshindi wa jumla atatinga hatua ya nusu fainali.

Simba na Al Ahly katika miaka ya hivi karibuni zimekutana mara sita kwenye michuano ya CAF ambapo kila timu imeshinda mechi mbili ilizokuwa nyumbani, na kutoa sare mbili mfululizo katika mechi mbili za mwisho za mashindano mapya ya African Football League (AFL) mwaka jana ilianza sare ya mabao 2-2 kwa Mkapa kisha 1-1, Misri.