Mashujaa mdogo mdogo, yabeba tatu nyingine

MASHUJAA FC ya Kigoma jioni ya leo imeendelea kuvuna pointi tatu katika mechi za Ligi Kuu Bara baada ya kuinyoosha JKT Tanzania kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika ukiwa ni ushindi wa pili mfululizo za ligi hiyo.

Bao pekee la Mashujaa lililofungwa dakika ya saba lililowekwa kimiani na Balama Mapinduzi 'Kipenseli' limeifanya wageni hao wa Ligi Kuu Bara, kuchupa kutoka nafasi ya 14 hadi ya 11 ikifikisha pointi 21 baada ya mechi 19, huku JKT ikishuka kutoka nafasi ya 13 hadi ya 14 ikisaliwa na pointi 19.

Mashujaa iliyopanda Ligi Kuu msimu huu wikiendi iliyopita ilipata ushindi wa kwanza baada ya mechi tisa kwa kuifunga Namungo kwa bao 1-0  na kocha wa timu hiyo, Abdallah Mohammed 'Baresi',  amesema mara baada ya mchezo huo kuwa wamefurahia matokeo na kuondoka na pointi tatu za ushindi na kuwapongeza vijana wake kwa kucheza vizuri na kufata maelekezo aliyowapatia.

Msemaji wa JKT Tanzania, Masau Bwire amesema wamepoteza mchezo na kuzikosa pointi tatu muhimu ugenini na kuahidi kwenda kufnyia kazi mapungufu yaliyosababisha kupoteza mchezo.

“Binafsi wanawapongeza vijana wangu wamepambana na kuonesha kiwango cha juu sana wakati wa mchezo lakini bahati haikuwa upande wetu,” amesema Bwire

Amesema katika mchezo huo ameona unyumbani zaidi, kuwa ukiwa nyumbani unafaida ya kushinda hata kama haustahili kushinda kwani kila mmoja aliyetazama mchezo huo ameweza kuliona hilo.

Akizungumzia kuhusu maendeleo ya mchezaji Edward Songo aliyeumia uwanjani wakati mchezo huo ukiendelea , Masau amesema mchezaji huyo yupo chini ya uangalizi maalumu katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kigoma Maweni.
Amesema taarifa za awali za madaktari zinaonesha kuwa mchezaji huyo amepata jeraha baada ya  kuvunjika mfupa kwenye fuvu chini ya jicho.

Kocha msaidizi wa timu ya JTK Tanzania, George Mketo amesema wachezaji wake walifata maelekezo na kutengeneza nafasi ya kufunga lakini bahati haikua upande wao, na kuwapongeza  Mashujaa kwa kuchukua alama tatu.

Mechi ijayo kwa Mashujaa itakuwa ugenini kuvaana na Simba siku ya Machi 15, ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa bao 1-0 lililofungwa kwa Saido Ntibazonkiza kwenye mchezo wa kwanza ulippigwa Februari 3 ikiwa mjini hapa.