Mashine za kazi zitakazotia njaa kali msimu huu

Muktasari:

Mpango wa Zahera ukawa kuwajaza upepo mashabiki wao ili kuhakikisha wanatunisha mfuko wa fedha za usajili na sasa ameshakusanya mastaa kibao wapya ambao anawaleta kuja kufanya kazi ili msimu unaoanzia karibuni wachukue taji.

Kuelekea msimu wa Ligi Kuu Bara 2019/20 moja ya klabu ambayo itaingia na sura mpya kuwania taji hilo, Yanga imefanya usajili mkubwa.

Yanga ni mabingwa wa kihistoria wa ligi hiyo, lakini wamepishana na kombe hilo kwa misimu miwili mfululizo na mbaya zaidi wakishuhudia watani zao wa jadi, Simba wakibeba ndoo. Hata hivyo msimu huu wamesuka kikosi chao upya.

Msimu uliopita Yanga haikuwa na kikosi imara licha ya kuongoza ligi kwa muda mrefu, lakini baadaye iliishiwa nguvu na kujikuta ikiachwa njiani na kupitwa na Simba ambapo akili yao kubwa kupitia kocha wao Mwinyi Zahera ikawa kufumua kikosi hicho.

Mpango wa Zahera ukawa kuwajaza upepo mashabiki wao ili kuhakikisha wanatunisha mfuko wa fedha za usajili na sasa ameshakusanya mastaa kibao wapya ambao anawaleta kuja kufanya kazi ili msimu unaoanzia karibuni wachukue taji.

Fedha za usajili zilichangwa kwa wingi, kwa kauli mbiu ya ‘wawekezaji ni wananchi’ ambapo haraka usajili Yanga ulianza mapema kwa mastaa kibao kutua na kuanza kusainishwa mara tu baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu 2018/2019.

Mastaa wapya 15

Mpaka Yanga inafunga dirisha la usajili ilijikuta tayari imeshasajili timu kamili na wachezaji wanne wa akiba, ikiingiza jumla ya sura mpya 15 katika timu yao tayari kwa msimu ujao huku jina la mwisho kusajiliwa likiwa mshambuliaji David Molinga.

Yanga ilisajili kila eneo kuanzia golini, mabeki, kiungo hadi washambuliaji ambapo katika usajili huo iliingiza jumla ya wachezaji wa kigeni tisa ambao ni kipa Farouk Shikhalo (Kenya); mabeki wakiwa ni Lamine Moro (Ghana), Mostapha Seleman (Burundi) ilhali washambuliaji ni Maybin Kalengo (Zambia), Issa Bigirimana, Patrick Sibomana (wote Rwanda), Juma Balinya, Sadney Urikhob (Namibia) na Molinga (DR Congo).

Wazawa walioingia katika usajili mpya wa Yanga walikuwa sita ambao ni pamoja na kipa Metacha Mnata; mabeki ni Ally Ally, Ally Mtoni, Muharami Issa ‘Marcelo’ huku viungo wakiwa ni Mapinduzi Balama na Abdulaziz Makame.

Katika usajili huo, Yanga iliachana na wachezaji wasiopungua 10 kwa sababu mbalimbali ikiwemo kuuzwa, kushuka viwango na wengine kutimkia timu zingine.

Kambi wiki mbili Moro

Baada ya usajili huo, Yanga ilikuwa na maandalizi ya mwanzo wa msimu ambapo kama kawaida yao walikimbilia mkoani Morogoro na kujifua kwa wiki mbili bila ya kocha wao mkuu, Zahera ambaye hata hivyo alijiunga mwishoni akitokea kwake Ufaransa alikokwenda kwa mapumziko baada ya kutoka katika Fainali za Mataifa Afrika (Afcon).

Wakiwa kambini Moro, mastaa hao wa Jangwani walikuwa na mazoezi makali ya asubuhi na jioni chini ya kocha msaidizi, Noel Mwandila ambaye hata hivyo alikuwa na mawasiliano ya karibu na bosi wake, Zahera huku pia baadaye wakawa na michezo ya kirafiki na kufanikiwa kushinda yote.

Yarejea Kimataifa

Katika hali ya kushtua, Yanga ilijikuta ikianza msimu mpya wakiwa na zawadi kubwa baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuitangaza timu hiyo kurejea anga za kimataifa kufuatia mabadiliko yaliyofanywa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuongeza idadi ya timu shiriki, na klabu hiyo kongwe kujikuta inaangukia Ligi ya Mabingwa Afrika.

Tofauti na misimu iliyopita ambayo ligi ya ndani imekuwa ikianza kabla ya mashindano ya CAF, msimu huu Yanga ilishaanza kampeni yake ya Ligi ya Mabingwa ikianza na sare ya bao 1-1 nyumbani dhidi ya Township Rollers ya Botswana.

Zahera matumaini kibao

Akizungumzia timu aliyonayo, Kocha Zahera alisema msimu ujao atakuwa na timu tofauti itakayokuwa na sura za kushindania mataji tofauti na msimu uliopita.

Zahera alisema usajili alioufanya katika dirisha kubwa la usajili, uongozi wa klabu yake, wanachama na mashabiki wamefanya kazi kubwa kufanikisha usajili huo na sasa kazi aliyonayo ni kuunda timu itakayokuwa na sura za ushindani.

“Nimewaangalia hawa wachezaji wapya na hawa tuliowaongeza naona kama msimu ujao tutakuwa na timu bora kiushindani kuliko hata ile ya msimu uliopita, tutakuwa na ubora wa kushindana kupata mataji,” alisema Zahera.

“Niwapongeze mashabiki, wanachama na viongozi na kila mmoja aliyeshiriki katika mchakato wetu amefanya kazi kubwa, sasa kazi inaendelea kuunganisha timu ili tuweze kufikia malengo.”

Nahodha mpya huyu hapa

Baada ya kuondokewa na aliyekuwa nahodha wao, Ibrahim Ajibu aliyemaliza mkataba na kurejea klabu yake ya zamani, Simba, msimu ujao Yanga itaingia na nahodha mpya ambaye ni kiungo Mkongomani Pappy Kabamba ‘Tshishimbi.

Tshishimbi, nyota aliyekipiga katika klabu hiyo msimu ulipita atakuwa na kazi ya kuhakikisha anawaongoza wenzake kuwa na morali ya ushindani akisaidiana na beki Juma Abdul ambaye amehakikishiwa nafasi yake.

Tshishimbi alisema msimu ujao kutakuwa na ushindani mkubwa, na Yanga iko tayari kushindana kutokana na usajili wa kipekee ambao wameufanya na kwamba, wachezaji wenzake walioongezwa watarudisha uhai wa timu yao.

“Wachezaji wapya waliosajiliwa naona kila mchezaji ana ubora mkubwa, nawapongeza makocha na viongozi, sasa kazi iliyopo ni kuunganisha timu na kucheza kwa kuelewana,” alisema Tshishimbi.

Wakati Yanga ikiwa na matumaini kibao kwa ajili ya msimu ujao, kwa sasa macho yake yapo huko Gaborone, Botswana ambako inatarajia kucheza na Rollers, wiki hii.