Mashine tano noma kwa mashuti makali

Muktasari:

Yale mabao manne aliyofunga Mohamed Salah kwenye mechi moja, yamemfanya aweke gepu la mabao manne dhidi ya Harry Kane, kwenye nafasi ya pili.

LONDON, ENGLAND

MBIO za Kiatu cha Dhahabu kwenye Ligi Kuu England zinazidi kunoga kweli kweli.

Yale mabao manne aliyofunga Mohamed Salah kwenye mechi moja, yamemfanya aweke gepu la mabao manne dhidi ya Harry Kane, kwenye nafasi ya pili.

Mo Salah kwa sasa ndiye kinara kwenye Ligi Kuu England baada ya kupachika 28, huku Kane amefunga 24 na Sergio Aguero yupo kwenye nafasi ya tatu na mabao yake 21. Lakini, kila kitu kinaonekana kuwa kizuri kwa Salah kutokana na wapinzani wake kwenye mbio hizo kuwa wagonjwa na yeye ndiye aliyebaki pekee akiwa fiti. Lakini, unajua kuna wachezaji hao wamelenga golini mara nyingi na kama mashuti yao yote yangetinga wavuni, basi stori kwa sasa ingekuwa tofauti. Hii ndiyo orodha ya wachezaji wanaoongoza kwa mashuti yao kulenga magoli ya wapinzani kwenye Ligi Kuu England.

Supastaa wa Manchester City, Kevin De Bruyne ni miongoni mwa wachezaji waliopiga mashuti mengi yaliyolenga goli baada ya kupiga 34 kwenye Ligi Kuu England. De Bruyne hajafunga mabao mengi, lakinin amelenga goli mara nyingi. Straika wa Manchester United, Romelu Lukaku amefunga mabao 14 kwenye Ligi Kuu.

Fowadi huyo ameongoza pia kwa kupiga mashuti yaliyolenga goli la wapinzani baada ya kufanya hivyo mara 37 na kuwa kwenye orodha ya mastaa watano ambao mashuti yao mengi yamelenga magoli ya wapinzani katika mikikimikiki ya ligi hiyo.

Sergio Aguero ameonyesha kuwa ni moto msimu huu, ukiweka kando mabao yake 21 aliyotupia wavuni kwenye Ligi Kuu England hadi sasa, habari ingekuwa tofauti kama mashuti yake 41 aliyopiga kulenga goli yangetinga wavuni. Supastaa wa Liverpool, Salah anakenua tu kwa kufunga mabao 28 hadi sasa, lakini fowadi huyo aliyepachikwa jina la Messi wa Misri, angeweza kufunga mara nyingi zaidi kwenye ligi hiyo kama mashuti yake 57 aliyopiga kulenga magoli ya wapinzani yangetinga kwenye nyavu.

Fowadi wa Tottenham, Harry Kane ndiye mchezaji aliyepiga mashuti mengi zaidi kulenga magoli ya wapinzani baada ya kufanya hivyo mara 67. Kwenye Ligi Kuu amefunga mabao 24, hivyo makipa wa timu pinzani pamoja na mabeki wamefanya kazi kubwa ya ziada kuzuia mashuti yake 67 yaliyolenga kwenye goli yasitinge kwenye wavu na kufanya awe amefunga mabao hayo tu ambayo kwa sasa wanamfanya ashike namba mbili kwenye kilele cha wanaongoza kwa kufunga kwenye Ligi Kuu England msimu huu.