Mashabiki waiponza JKT Tanzania

Muktasari:
- Ligi Kuu Tanzania Bara ilirejea rasmi Juni 13 baada ya kusimama kwa miezi mitatu kwa ajili ya tahadhari ya virusi vya Corona.
TIMU ya JKT Tanzania imepewa adhabu ya kucheza bila mashabiki katika michezo yake yote ya nyumbani ya Ligi Kuu msimu huu kwa kosa la kukiuka miongozo ya serikali, adhabu itakayoanza leo.
Kosa hilo ni kushindwa kudhibiti idadi ya mashabiki waliojitokeza katika uwanja wa Jamhuri, Dodoma jana katika mchezo wao wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.
Taarifa iliyotolewa leo na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imeeleza kuwa adhabu hiyo imeelekezwa kwa JKT Tanzania kwa sababu wao ndio walikuwa timu mwenyeji.
"Katika mchezo huo na. 288 uliochezwa jana Jumatano, Juni 17, 2020, mashabiki walijazana uwanjani na kukaa bila kuzingatia Kanuni ya 2.0.2 (iii) inayosisitiza kuachiana mita moja.
Pamoja na hatua mbalimbali za kiafya kuzingatiwa, uchunguzi umebaini kuwa wawakilishi wa timu mwenyeji ambao ndio waliokuwa wakidhibiti mageti hawakutekeleza majukumu yao ipasavyo na badala yake waliruhusu mashabiki wenye tiketi na wasio na tiketi kuingia uwanjani ovyo na kuharibu mpangilio wa ukaaji ambao mpaka saa nane mchana ulikuwa umezingatiwa vyema.
Hatua hii inalenga kuvikumbusha vilabu mwenyeji, wasimamizi wa michezo na wadau wengine kote nchini kuendelea kusimamia kkamilifu mwongozo wa afya na taratibu nyingine michezoni hadi serikali itakapojiridhisha kuwa ugonjwa wa Covid-19 umekwisha kabisa hapa nchini," ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ya Wizara imesisitiza kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua kali zaidi kwa wale watakaoendelea kukaidi miongozo mbalimbali inayotolewa wakati huu wa changamoto za ugonjwa wa Covid-19 unaotokana na virusi vya Corona.