Mashabiki Betis wamshangilia Messi akiwapiga tatu

Muktasari:

Miamba hao wa Catalunya wanaongoza La Liga kwa tofauti ya pointi 10 kileleni baada ya Atletico Madrid kupoteza mechi yao ya wikiendi huku Real Madrid ikiwa nyuma kwa pointi 12 kwa Barca.

Madrid, Hispania. Lionel Messi amewashukuru mashabiki wa Real Betis kwa kusimama na kumpigia makofi kufuatia kuwafunga goli kali alipotupia ‘hat-trick’ dhidi yao katika ushindi wa Barcelona usiku wa kuamkia leo.

Messi alikamilisha ‘hat-trick’ yake ya 33 kwenye LaLiga kwa kuudokoa mpira uliopita juu ya kipa Pau Lopez na kugonga ‘besela’ kabla ya kutua wavuni na kukamilisha ushindi wa 4-1 kwenye Uwanja wa Benito Villamarin Jumapili usiku.

Amebakisha ‘hat-trick’ moja kuifikia rekodi unayoshikiliwa na Cristiano Ronaldo ya kufunga ‘hat-trick’ 34 katika Ligi Kuu ya Hispania.

Nahodha huyo wa Barca alishangazwa na pongezi ambayo hakuitarajia kutoka kwa mashabiki waliohudhuria kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Benito, ambao walionekana kupagawishwa na ‘vitu’ vya gwiji huyo Muargentina.

"Ukweli ni kwamba sikumbuki (jambo kama hili kunitokea)," Messi aliiambia Movistar baada ya kufunga ‘hat-trick’ yake hiyo ya 33 katika LaLiga.

"Nimefurahishwa na walichofanya mashabiki hawa. Kila tunapokuja kwenye uwanja huu huwa wa wanatupokea vyema, nimefarijika sana na ninafurahia ushindi huu, muhimu kwetu.”

Barca walitawala mpira kwa asilimia 43.9 tu, kiwango cha chini zaidi kwao tangu Opta ilipoanza kuweka rekodi za soka msimu wa 2004-05.

Miamba hao wa Catalunya wanaongoza La Liga kwa tofauti ya pointi 10 kileleni baada ya Atletico Madrid kupoteza mechi yao ya wikiendi huku Real Madrid ikiwa nyuma kwa pointi 12 kwa Barca.