Mapya yaibuka ishu ya kigogo Tabora United

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • "Hata baada ya kuandika barua yake, tumemtaka kabla ya kumkubalia uamuzi wake wa kujiuzulu kwanza atukabidhi ofisi na atuthibitishie hayo malipo yote ya hizo fedha, akifanya hivyo tutaachana naye kwa kuwa ilikuwa ndiko tunakokwenda kuachana naye."
     

SAA chache tu tangu kuenea kwa taarifa za Ofisa Mtendaji wa klabu ya Tabora United, Thabit Kandoro kutangaza kujiuzulu, mapya yameibuka baada ya kuelezwa mabosi wa juu ya klabu hiyo wamemgomea huku wakiweka bayana fyagia fyagia inayoendelea klabuni hapo kwa sasa.

Bosi wa juu wa timu hiyo, ameliambia Mwanaspoti mabadiliko yote ya kuondoka kwa wafanyakazi wake yalikuwa yanafahamika ndani ya klabu yao kutokana na sababu mbalimbali.

Akizungumzia kujiuzulu kwa Kandoro, bosi huyo amesema kigogo huyo alikuwa njiani kutimuliwa baada ya kubainika kwa tuhuma mbalimbali za fedha kiasi cha Sh20 milioni ambazo alitakiwa kuzithibitisha.

"Kuna mambo ya fedha za klabu tulibaini mambo ambayo hatukuyaelewa, tukamwita na kumtaka atuthibitishie hayo matumizi yake kwa kuwa zilipita kwenye mikono yake, baada ya kumtaka kufanya hivyo tukashtuka anasema anajiuzulu kwa kutuandikia barua," amesema bosi huyo.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

"Hata baada ya kuandika barua yake, tumemtaka kabla ya kumkubalia uamuzi wake wa kujiuzulu kwanza atukabidhi ofisi na atuthibitishie hayo malipo yote ya hizo fedha, akifanya hivyo tutaachana naye kwa kuwa ilikuwa ndiko tunakokwenda kuachana naye."

Hata hivyo, akijibu tuhuma hizo, Kandoro amesema; "Bado sijakabidhi ofisi, hivyo siwezi kusema lolote kwa sasa, kila kitu kina taratibu zake."

Akizungumzia kuondoka kwa kocha Henry Mkanwa, bosi huyo wa juu wa Nyuki amesema kocha huyo hakuwa muajiriwa wa Tabora United na kwamba alikuwa klabuni hapo kwa maombi ya kupata nafasi ya kujifunza kwenye benchi lao la ufundi.

"Huyu Mkanwa kwanza muulizeni ana mkataba na Tabora? Huyu alikuja kwetu baada ya kuomba kupata nafasi ya kupata uzoefu kwa kujifunza, tulipobadili makocha na kuleta makocha wapya tukaona tutakuwa na watu wengi kwenye benchi letu, tukasema mafunzo yake yaishie hapo kwani tulishaanza kuona viashiria vya mvurugano," amesema kigogo huyo ambaye jina lake tunalo.

Kwa ishu ya kocha wa makipa, Razack Siwa, bosi huyo alifafanua kuwa baada ya mzunguko wa kwanza wa ligi kumalizika ilikuja tathimini ya kuporomoka kwa viwango vya makipa akiwamo kipa John Noble.

"Kuhusu Siwa (Razack) hata nyie waandishi jiulizeni uwezo ambao kipa Noble (John) alioanza nao ligi ndio huu alionao sasa? Sisi tuna vikao vyetu vya tathmini ya timu, vilibaini kwamba makipa wetu uwezo unashuka kwa kasi," amefafanua kigogo huyo na kuongeza;

"Noble ambaye tulimleta akiwa kwenye kiwango kikubwa kiasi cha kutakiwa na klabu kubwa mbalimbali lakini sasa ukiona kiwango chake unasikitika, kwahiyo hatua ya kwanza timu inapofanya vibaya anawajibishwa kocha na hiki ndicho tulichofanya, tukasema tuachane na huyu Siwa labda kiwango chake cha ufundishaji kimefikia mwisho."

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Akijibu ishu za malipo ya wachezaji bosi huyo amesema hakuna mchezaji wa Tabora anayedai mishahara ambapo kama kuna madai yoyote yanaweza kuwa ni malipo ya ada za usajili ambayo yatalipwa kwa mujibu wa mikataba.

"Ndugu yangu hakuna mchezaji anayeweza kuvunja mkataba wake kwa kutokulipwa ada ya usajili, nakuthibitishia kuwa haya ndio malipo pekee ambayo yanaweza kuwa yamebaki na yatalipwa kwa mujibu wa mikataba lakini suala la mchezaji anadai mishahara hilo halipo na hatuwezi kujibu kila uzushi wa mitandaoni."

Awali, Ofisa Habari wa Tabora, Christina Mwangala alikanusha taarifa kwamba makocha wapya wa timu hiyo, Denis Laurence na msaidizi Masoud Djuma kuwa wanataka kuondoka kwa kile kinachoelezwa hawajaridhishwa na mazingira, huku ikielezwa pia hawakusaini mkataba na kusema ni uzushi.

Christina amesema kocha mkuu Denis na Djuma aliyempendekeza kuja kufanya kazi naye wamesaini mkataba ndio maana wanaendelea kupiga mzigo kuiandaa timu kwa mechi za Ligi Kuu Bara zijazo.

"Hili linafahamika wazi, mtu anapoanza kufanya kazi maana yake ni kwamba tayari walishakubaliana na mwajiri, hivyo kusema makocha hao wanaweza kuacha kazi na hawakusaini ni uzushi na uongo. Tunaomba mzipuuze," amesema Christina aliyefafanua pia kwamba kwa sasa timu inaendelea kujifua kujiandaa na michezo ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Singida FG na ile ya Ligi Kuu iliyokuwa imesimama kupisha mechi za kalenda ya FIFA.

Tabora inayoshiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza baada ya kupanda daraja kutoka Ligi ya Championship ilikokuwa ikitumia jina la Kitayosce, kwa sasa inashika nafasi ya 13 katika msimamo ikiwa na pointi 21 katika mechi 13 ilizocheza ikijiweka kwenye mstari wa kushuka daraja kwa play-off.