Maproo Yanga kutua Ijumaa kujiandaa na Wiki ya Wananchi

Muktasari:
Sherehe zitaanza Julai 21 kwa mashabiki na wanachama wa Yanga watafanya kazi mbalimbali za kijamii kabla ya kilele Julai 27
Dar es Salaam. Wachezaji wapya wa kimataifa wa Yanga wanatarajiwa kuwasili nchini Ijumaa tayari kwa maandalaiizi ya Wiki ya Wananchi itakayofikia kilele Julai 27.
Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla alisema wachezaji hao watawasili Julai 5 na Julai 7 watakwenda Mkoani Morogoro kambini.
"Tayari tumekwisha watumia tiketi wachezaji wote na wote watawasili nchini Julai 5," alisema Msolla.
Wachezaji hao ni mabeki, Lamine Moro (Ghana) na Mustapha Seleman (Burundi). Washambuliaji, Sadney Ukhob (Benin), Issa Bigirimana (Burundi), Patrick Sibomana (Rwanda), Juma Balinya (Uganda) na Kalengo Maybin (Zambia).
Akizungumzia maandalzi ya wiki ya Wananchi, Msolla alisema sherehe zitaanza Julai 21 ambapo mashabiki na wanachama wa Yanga watafanya kazi mbalimbali za kijamii kabla ya kilele Julai 27.
"Tutatembelea na kutoa misaada katika vituo vya watoto Yatima, kuchangia damu na kufanya usafi katika maeneo mbalimbali nchini," alisema Msolla.
Alisema kilele cha Wiki ya Wananchi watacheza mechi ya Kimataifa na mojawapo ya timu kutoka Misri, Morocco au Guinea.