Mapema tu! Simba yaiteka Gaborone, shangwe kama lote...

Sunday October 17 2021
simba botswana pic
By Waandishi Wetu

SIMBA wanarudi tena katika anga za kimataifa watakapokuwa ugenini mjini Gaborone, Botswana kumalizana na Jwaneng Galaxy, huku kikosi kikielezwa kina mzuka kama wote wa kumaliza kazi mapema kutokana na sapoti kubwa iliyopata kutoka kwa Watanzania waliopo huko.

Wawakilishi hao pekee wa Ligi ya Mabingwa Afrika, watashuka uwanjani 9:00 alasiri kwa saa za Botswana ambazo ni sawa na saa 10 jioni Tanzania kuanza mchakato kwenda kwenye makundi ya msimu huu mbele ya wenyeji wao ambao inaelezwa walihama mji kwa muda kujichimbia kujiandaa na mchezo huo.

Tangu Simba itue mjini Gaborone juzi Ijumaa imepata mapokezi makubwa toka kwa Watanzania waishio huko ambao wameifanya ijione kama ipo nyumbani, huku wachezaji wakielezwa wana mzuka mkubwa wa kutaka kuwapa zawadi ya mapokezi hayo kwa kutoka na ushindi mjini humo.

Ushindi wa ugenini dhidi ya Jwaneng leo bila shaka utaiweka Simba katika nafasi nzuri ya kuandika rekodi mpya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa vipindi viwili tofauti.

Rekodi hiyo ni ile ya kutinga hatua ya makundi na kuwa ni mara ya pili mfululizo ambayo sio wao tu, bali hakuna timu yoyote Tanzania iliyowahi kufanya hivyo katika historia.

Msimu uliopita Simba ilitinga makundi na kuvuka hadi robo fainali na kukwamishwa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, lakini ilishatinga awali hatua kama hiyo 2003, lakini msimu ulioifuata ilitolewa hatua ya awali na Zanaco ya Zambia kwa jumla cha mabao 3-2, kisha ikarudia tena 2018-2019 na kuvuka hadi robo fainali ikazuiwa na TP Mazembe ya DR Congo kwenda nusu fainali. Hata hivyo msimu wa 2019-2020 ilitolewa raundi ya awali na UD Songo ya Msumbiji kwa faida ya bao la ugenini, kufuatia timu hizo kufungana bao 1-1, Dar es Salaam baada ya kutoka sare tasa huko Msumbiji.

Advertisement

Hivyo, leo Simba itataka kutengeneza mazingira ya kuandika historia mpya ikianzia ugenini kwa kushinda kabla ya kumaliza kazi nyumbani wiki ijayo, ingawa itakuwa na kibarua kutokana na ubora na ufanisi wa wapinzani wao kimbinu na kiufundi hasa inapocheza uwanja wa nyumbani.

Kwa mujibu wa kocha wa Simba, Didier Gomes, Jwaneng imekuwa ikicheza soka la kutumia mabavu na wao wamejiandaa kukabiliana nao kwa vile anataka kushinda ugenini ili kumrahishia kazi nyumbani.

“Tumewatazama Jwaneng Galaxy kupitia video. Ni timu nzuri inayoshinda mipira ya kugombea na soka la kutumia nguvu, hivyo tunapaswa kuwa makini na kucheza kwa tahadhari, lakini niwatoe hofu mashabiki wetu tumejiandaa kupata matokeo mazuri,” alisema.

Katika kudhihirisha amewasoma vyema wapinzani wake, kocha Gomes na benchi lake la ufundi wamekuwa wakielekeza wachezaji mbinu ya kuubana uwanja na kupasiana kwa haraka pindi wanapoelekea kushambulia katika mazoezi yao ya mwisho kabla ya juzi kutimka kwa ndege ya kukodi.

Simba imekuwa haina historia nzuri pindi inapocheza ugenini dhidi ya timu kutoka kusini mwa Afrika ambapo mara nyingi imekuwa ikipoteza pointi ama kwa kutoka sare au kufungwa.

Hata hivyo benchi la ufundi la Simba linaamini kwamba historia hiyo itakuwa chachu kwa kikosi chao kufanya vizuri. “Lakini tumepata ushindi ugenini dhidi ya timu ngumu za AS Vita ya DR Congo na Plateau ya Nigeria,” alisema Gomes.

Simba katika mchezo huo itawakosa wachezaji saba ambao hawajasafiri na timu hiyo kwa sababu mbalimbali akiwamo Pape Sakho na Chris Mugalu (majeruhi), Jonas Mkude, Kibu Denis, Jeremiah Kisubi na Abdulswamad Kassim (kiufundi) wakati Yusuph Mhilu jina lake lilichelewa kuingizwa katika orodha ya wanaoshiriki michuano hiyo.

Pamoja na kuwakosa wachezaji hao, nahodha wa Simba, John Bocco alisema wamejipanga kupata ushindi

“Tunatambua kile ambacho tunakihitaji na malengo yetu ni kufika hatua za juu zaidi hivyo tutahakikisha tunapambana ili tupate ushindi,” alisema Bocco, huku kipa Aishi Manula akisema hawataki kurudia makosa ya nyuma wakitaka mafanikio makubwa zaidi msimu huu.


KILA KITU POA

Mratibu wa timu hiyo, Ali Abbas Seleman alisema Simba haijakutana na figisu ugenini hadi jana wakijiandaa kupiga tizi la mwisho Uwanja wa Taifa baada ya mchezo wa kimataifa uliotarajiwa kuchezwa jioni kati ya Orapa United dhidi ya Coton Sport ya Cameroon.

“Hatuna sababu wala kisingizio, kwani ni kama tupo nyumbani. Timu ipo tayari kwa mchezo huo...tunaomba dua kwa Watanzania,” alisema.

Imeandikwa na Charles Abel na Clezencia Tryphone

Advertisement