Manula achomolewa Simba

TAARIFA mpya ni kwamba kipa wa Simba, Aishi Manula amechomolewa kikosini na kuna uwezekano mkubwa atazikosmechi zote za Wekundu hao msimu huu.

Awali ilielezwa kipa huyo aliyekuwa na timu ya taifa iliyoenda kushiriki michuano maalumu ya Fifa Series iliyofanyika Baku, Azerbaijan angezikosa mechi mbili za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa, lakini taarifa zilizopatikana juzi zinaelezwa kwamba kipa huyo huenda asionekane tena uwanjani.

Ipo hivi. Manula aliyeanzishwa katika mchezo wa michuano ya Fifa Series kati ya Taifa Stars na timu ya taifa ya Bulgaria iliyoshinda baa 1-0, alishindwa kumaliza mchezo huo kutokana na kilichoelezwa kuumia nyonga. Kipa huyo namba moja wa Tanzania, ametoka kupona majeraha ya mwanzo aliyoyapata Aprili mwaka jana katika pambano la robo fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Ihefu, lililopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, uliopo Chamazi.

Katika mchezo huo Manula alishindwa kumaliza dakika 90 kwa kutolewa na kuwa nje ya uwanja kwa muda wa miezi sita baada ya kufanyiwa upasuaji na alirejea uwanjani katika pambano la Kariakoo Derby lililpogwa Novem,ba 5 mwaka jana na kutunguliwa mabao matano wakati Simba ikifa 5-1.

Tangu pambano hilo, lililomfukuzisha kazi aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mbrazili Roberto Oliveira ‘Robertinho’, kwani hakuwahi kurejea tena kwenye kiwango chake akipigishwa benchi klabuni na makipa Ally Salim na Ayoub Lakred na kuumia kwake akiwa Stars ndiko kulikomtibulia zaidi.

Inaelezwa kilichomponza zaidi ni presha ya mashabiki na viongozi wa Si9mba waliokuwa na hamu ya kurejea uwanjani kabla hajapona haraka na kukutana na derby iliyomweka matatani, kiasi ya kutimika mechi moja tu kati ya sita za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu Ayoub akifukia mashimo.

Taarifa zilizopatikana jana ni kuwa, Manula huenda asionekane tena msimu huu hadi tatizo lake la nyonga litakaposhughulikiwa, huku akiwa tayari kocha Abdelhak Benchikha akimchomoa katikia mipango ya michuano ya CAF mbali na ya Ligi Kuu kutokana na kiwango kilichoonyeshwa na Ayoub.

Taarifa zaidi zinasema kipa huyo alifanyiwa vipimo akiwa na Stars mjini Baku, lakini tatizo halikuonekana na ilikuwa inasubiriwa kufanyiwa vipimo zaidi kabla ya klabu kutoa taarifa rasmi kwa umma kuhusu nyota huyo wa zamani wa Azam aliyeirejesha Simba mataji kwa misimu minne mfululizo.


WASIKIE MADAKTARI

Daktari wa Yanga, Moses Etutu, amezungumzia juu ya majeraha ya nyonga na kusema mchezaji akifanyiwa upasuaji wa nyonga unaweza kuchukua wiki sita hadi nane kukaa nje kutokana na ukubwa wa tatizo.

Alisema mazoezi ya kumrudisha kwenye utimamu wa kimwili baada ya kufanyiwa upasuaji ‘post surgery rehabilitation program’ ni muhimu sana katika kupunguza muda wa utimamu kwa wanamichezo.

“Inategemeana ni aina gani ya upasuaji uliofanyika na rehabilitation program yake itakavyokua. Kwa ishu ya nyonga kuna patholojia nyingi tofauti wanazopata wanamichezo na muda wake wa kuhakikisha mchezaji anapona kabisa na kadhalika,” alisema  Dk Etutu na kuongeza;

“Mara nyingi huchukua sio chini ya wiki sita au nane hadi miezi minne kutegemeana alichoumia na kwa ukubwa gani kati ya hivyo vitu nlivyovitaja hapo juu ambavyo vyote huweza sababisha maumivu ya nyonga kwa wanamichezo.”

Daktari wa zamani wa Yanga, Dk Shecky Mngazija alisema mchezaji aliyefanyiwa upasuaji wa nyonga inategemea kuna upasuaji wa njia ya matundu na upasuaji huo.

“Hivyo itategemea na ukubwa wa tatizo lake na usahihi wa tiba aliyofanyiwa, umri pia na namna anavyofuatilia masharti aliyopewa na daktari wakati wa matibabu,” alisema Dk Mngazija na kuongeza; “Mfano kama jeraha ni dogo na ni la matundu pia siwezi kusema atakaa muda mfupi wakati hana tiba sahihi ya kutumia, lishe bora, ama umri alionao kama mkubwa na hafuati masharti aliyopewa.”

Mngazija alisema mgonjwa wa nyonga sharti kubwa na la kuzingatiwa ni kutofanya tendo la ndoa kwa muda ili kuweza kurudi haraka ikiwa ni pamoja na kuzingatia kuacha kufanya mazoezi kwa muda na kula chakula bora.

Kwa upande wa daktari wa Simba, Dk Edwin Kagabo alisema hakuna muda maalumu kuthibitisha kuhusiana na mchezaji kufanyiwa upasuaji wa nyonga kwa sababu inategemea na aina ya jeraha.

“Kwa kuwa majeraha ni mengi na tofauti kwenye eneo hilo hivyo muda hutofautiana ili kuzungumzia kila eneo la nyonga la mchezaji inahitaji muda mrefu kwa ajili ya kuelezea kila ugonjwa ulio eneo hilo.” Alipoulizwa swali kuhusiana na jeraha la Manula ambaye awali alienda Afrika Kusini kufanyiwa upasuaji hakutoa jibu lolote.