Manji ana mchezaji mmoja Yanga

Muktasari:

  • Manji alikuwa Uwanja wa Mkapa Jumamosi iliyopita akiishuhudia Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba na kukaribia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, baada ya kufikisha pointi 58 kwenye michezo 22.

MFADHILI na Mwenyekiti wa zamani wa Yanga, Yusuf Manji amesema kwake staa mkubwa ni mmoja tu kwa sasa. Stephane Aziz Ki.

Manji ambaye amewahi kuiongoza timu hiyo kwa mafanikio makubwa amesema amefanikiwa kuifuatilia Yanga kwa muda mrefu, lakini kiungo mshambuliaji Stephane Aziz Ki raia wa Burkina Faso amemuelewa.

Manji alikuwa Uwanja wa Mkapa Jumamosi iliyopita akiishuhudia Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba na kukaribia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, baada ya kufikisha pointi 58 kwenye michezo 22.

Yanga ilifanikiwa kuibuka na ushindi kwa mara ya pili dhidi ya Simba msimu huu, baada ya mchezo wa kwanza kuichapa mabao 5-1 kwenye uwanja huo.

Akizungumza na Mwanaspoti kwenye mahojiano maalumu, Manji alisema ameona mechi kadhaa za timu hiyo msimu huu, ikiwemo ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns pamoja na Dabi ya Kariakoo, lakini anaupongeza uongozi wa Yanga kwa kumsajili Aziz Ki.

“Nilifanikiwa kuutazama mchezo ule wa Yanga kule Afrika Kusini dhidi ya Mamelodi ambao Yanga ilifungwa kwa penalti, niliwaona wamecheza vizuri sana, lakini kuna mchezaji mmoja nilimuona ana nywele za Blonde (blichi), alionyesha kiwango cha juu sana na nimemuona pia kwenye mechi ya Dabi.”

Sijamfahamu vizuri jina lake, unajua siku hizi siyo kama zamani, sasa navaa miwani na umri umeenda,” Alipoonyeshwa picha tofauti za wachezaji wa Yanga alipomuona Aziz Ki alisema:“ Huyohuyo ndiye ninamaanisha huku akicheka, anakwenda uwanjani akijua nini anakwenda kufanya, ndiye ananivutia sana akiwa na Yanga nafikiri kila mmoja atakubaliana nami.”

Ki ndiye mchezaji staa wa Yanga na Ligi Kuu Bara msimu huu hadi sasa akiwa ndiye kinara wa kupachika mabao baada ya kuwa nayo 15, lakini akiwa pia na asisti saba zinazomfanya awe amehusika kwenye mabao 22.

Manji aliendelea kusema kuwa ameona mabadiliko makubwa kwenye kikosi cha Yanga na wachezaji wanaonyesha uwezo wa juu uwanjani.

“Nimefanikiwa kuwaona wachezaji wote, wanaonyesha kiwango cha juu uwanjani pamoja na kwamba huyo niliyemtaja ndiye bora lakini wengine wote wamenifurahisha wanavyocheza, timu inacheza vizuri sana,” alisema mwenyekiti huyo wa zamani wa Yanga.

Manji ambaye aliwahi kusajili mastaa wakubwa kwenye kikosi cha Yanga kama kiungo Mnyarwanda Haruna Niyonzima, alisema anafurahi kuona timu hiyo inafika sehemu ambayo ilikuwa ndoto yake.


KWANINI ALIGOMEA  MAMILIONI?

Manji ameeleza sababu iliyomfanya wakati akiwa Mwenyekiti wa Yanga agomee kitita cha fedha za udhamini kilichokuwa kikitolewa na chombo kimoja cha Televisheni.

Chombo hicho ambacho kinaonyesha michezo ya Ligi Kuu kwa sasa, kiliingia mkataba na timu za Ligi Kuu ikiwemo Yanga na Simba ambapo inadaiwa kilikuwa kikitaka kutoa kitita cha shilingi 100, kwa timu zote.

Klabu nyingine ikiwemo Simba zilikubaliana na dili hilo, lakini Yanga ikiwa chini ya Manji iligomea fedha hizo kwa kauli moja tu kuwa ni kiasi kidogo kutokana na ukubwa wa timu hiyo.

“Tulikaa mezani mara kadhaa tukazungumza, lakini nilichokuwa nataka ni kuona timu za Simba na Yanga kwa kuwa zina mashabiki wengi, basi kiwango chao kiwe tofauti na timu nyingine za ligi.


“Hili lilikataliwa lakini sisi tuliendelea kushikilia msimamo kuwa hatuchukui na wakati wote nilipokuwa kiongozi hatukuchua fedha hizo alisema Manji.

“Unajua wakati huo Azam FC ilikuwepo kwenye ligi, wakati huohuo kampuni mama ikawa inataka kudhamini ligi niliona kuwa kutakuwa na mgongano wa kimaslahi, ilikuwa jambo moja aidha kampuni isidhamini au waondoe timu kwenye ligi,” alisema Manji ambaye kwa sasa anaishi majuu.

Hata hivyo, Manji alisema hakupinga suala la mashabiki kuangalia mpira kwenye televisheni kwa kuwa ni maendeleo makubwa kwenye soka la Tanzania, lakini aliona kuna mambo mengi hayaendi sawa kwenye yale makubaliano.


“Mfano, sijui kama hilo leo lipo, lakini nilitaka kuona kama mechi ya Simba inachezwa Dar es Salaam, basi televisheni isionyeshe mechi hizo hapa jijini bali kwenye mikoa mingine, lakini hata kama Mtibwa inacheza Arusha pale mechi isionyeshwe kwenye televisheni.

“Kufanya hivyo kutawafanya mashabiki kwenda uwanjani kwa kuwa timu zote zinategemea viingilio, kuuza jezi, skafu na vitu vingine vya klabu, sasa ukionyesha kwenye mkoa husika watu watabaki majumbani, huwezi kuufanya mchezo huu ukaendelea kuwa wa furaha na watu kukutana viwanjani,” alisema Manji ambaye kiasili  ni mfanyabiashara mkubwa duniani.

Manji ambaye alichukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne akiwa na Yanga na kipindi chote timu ilienda Ligi ya Mabingwa Afrika, amesema anafurahi kuona ndoto zake zinatimia kwenye timu hiyo.


UTARUDI YANGA?

Alipoulizwa kama anaweza kurudi Yanga au kuwa mwekezaji alisema; “Kwa sasa siwezi kwanza umri umeenda siwezi zile pilika pilika za kusimamia timu.

“Unajua hata kama utakuwa ofisini, tabia yangu ni kwamba napenda kufanya kazi zote nikiwa karibu, naweza kuwa na viongozi wengine lakini nitalazimika kusafiri na wachezaji, nahakikisha kila kitu chao kinaenda vizuri, ukweli kwa kipindi hiki sitakuwa na uwezo tena wa kufanya hivyo wanatakiwa kufanya vijana,” alisema Manji aliyeiongoza Yanga kwa miaka minne.

Mfanyabiashara huyo amesema yeye alikuwa akichukulia soka kama mchezo wa jamii ndiyo maana alikuwa anafanya vitu vingi kama sehemu ya kuifurahisha jamii badala ya kuwaza fedha.


“Nilianzisha mfumo wakati mwingine wa kununu tiketi zinaenda kugawiwa kwenye matawi ya Yanga kwa kuwa nilitaka kurudisha kwa jamii, kama unakumbuka mchezo wa Yanga na TP Mazembe kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza mashabiki waliingia bure.

“Pale haikuwa bure kama ambavyo inafanyika sasa bali nilinunua tiketi zote zikagawiwa kwa mashabiki wa Yanga kupitia kwa viongozi wa matawi yao, nia ilikuwa ni kuhakikisha mchezo huu unarudi kwa jamii yetu,” alisema Manji ambaye alihudhuria mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Yanga na Simba Jumamosi iliyopita.

Manji ambaye aliingia madarakani siku chache baada ya Yanga kuchapwa mabao 5-0 na Simba, anasema nia yake ya kwanza ilikuwa kutafuta muafaka kwa makundi yaliyokuwepo Yanga ambayo ni Yanga Asili, Yanga Kampuni na Yanga Akademia.


“Moja ya jambo ambalo nakumbuka nililifanya na kuisaidia Yanga hii kufika hapa ni kuweka umoja, wakati naingia nilikuta migogoro mingi kulikuwa na makundi matatu, nakumbuka moja liliitwa Yanga Asili, lingine Yanga Kampuni na moja liliitwa Yanga Akademia.

Nilitumia ushawishi wangu wote na kuhakikisha haya makundi yanaisha na Yanga ikasimama, nafikiri imewasaidia hadi leo ndiyo maana kuna umoja,” alisema Manji ambaye ,” alisema Manji

Manji aliajiri makocha kadhaa wakubwa Yanga wakiwemo Konstadian Papic, Milutin Sredojevic Micho, Sam Timbe, Ernest Brandts na Tom Santifiet.