MANICHE: Mahanjumati yamenidatisha
Awadh Juma akiwa na mkewe na mtoto wao
Muktasari:
Mabao yake adimu na muhimu ndiyo yamekuwa chachu ya mafanikio ya Simba, rejea kwenye michezo ya Nani Mtani Jembe ya miaka ya 2013 na 2014, bila shaka utamkumbuka alivyosaidia kuipa timu yake ushindi dhidi ya Yanga.
KWA mashabiki wa soka wanaofuatilia mambo ya uwanjani, wengi wanamfahamu Awadh Juma ‘Maniche’. Ni yule kiungo mahiri wa Simba anayetokea visiwani Zanzibar. Kipaji chake cha kusakata soka na uwezo wa kufunga mabao, ndiyo vimemfanya awe maarufu.
Mabao yake adimu na muhimu ndiyo yamekuwa chachu ya mafanikio ya Simba, rejea kwenye michezo ya Nani Mtani Jembe ya miaka ya 2013 na 2014, bila shaka utamkumbuka alivyosaidia kuipa timu yake ushindi dhidi ya Yanga.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, bao lake pekee lilitosha kufuta uteja wa Simba katika mechi za Tamasha lao la Simba Day walipoizabua SC Villa.
Mwanaspoti limeamua kukuletea habari za maisha yake ya nje ya uwanja tofauti na mlivyomzoea kwenye soka, tunamaanisha maisha yake ya nyumbani. Anapokuwa na familia yake, Maniche huwa mtu wa aina gani na nini ndoto zake za maisha?
Mwandishi wa makala haya alimzukia nyumbani kwake maeneo ya Sinza White Inn, jijini Dar es Salaam. Jamaa anakaa mitaa ya Ngamia na akiishi hapo pamoja na familia yake; yaani mkewe (Hawa Masoud) pamoja na mtoto wao wa kwanza aitwaye, Harshan. Anasema ni jina lenye asili ya Kiarabu na maana yake ni Furaha.
Anasema aliamua kumpa jina hilo mtoto wake huyo kwa sababu anaona amekuja na bahati kwani tangu mkewe aliposhika ujauzito, amekutana na matukio mengi ya furaha na hata alipojifungua mambo yalikuwa hivyo na ndiyo maana akamwita jina hilo.
Pia anaishi na shemeji yake anayeitwa, Fatuma Masoud.
Mwanaspoti lilipofika nyumbani hapo lilikaribishwa na mkewe kwa sababu Awadh alikuwa na majukumu kwenye timu na hata aliporudi nyumbani, waliungana na mkewe kumpa ushirikiano mwandishi wetu.
NYUMBANI
Awadh: Karibu hapa ndiyo nyumbani na jisikie kwako. Tunaishi hapa ndiyo kama unavyotuona, mimi, mke wangu, mwanetu Harshan na shemeji yangu Fatuma amekuja kututembelea.
Mwanaspoti: Kitu gani kilivutia ukachagua kuishi mahali hapa?
Awadh: Ni mahali tulivu, hakuna kelele wala fujo, pia upo usalama wa kutosha.
Mwanaspoti: Nani aliwachagulia kuishi mahali hapa na ni nyumba ya ngapi kuishi tangu mlipohamia Dar es Salaam?
Awadh: Ni nyumba ya kwanza tangu tuhamie Dar es Salaam na hapa alitutafutia jamaa yetu mmoja.
Mwanaspoti: Mbali na familia yako ni nini hukuburudisha unapokuwa nyumbani, pia ni shughuli gani za nyumbani ambazo huwa unazifanya kumsaidia mkeo?
Awadh: Huwa naangalia televisheni inapokuwa mechi, filamu au muziki hasa R&B.
Movie ninazopenda kuangalia ni zile za kawaida siyo komedi. Kwa Bongo msanii ninayempenda ni JB. Kuhusu kazi za nyumbani, huwa natengeneza juisi ndiyo kazi yangu haswa, napenda sana kutengeneza juisi kwa sababu naipenda. Hizo nyingine kama kufua, kupika na kusafisha nyumba siku nikifurahi nazifanya ili kumfurahisha mke wangu.
MALAVIDAVI
Mwanaspoti: Hongera una mke mzuri, lakini unakumbuka ni namna gani ulivyompata?
Awadh: Sina kumbukumbu, ila tulikuwa shule ya sekondari, yeye alisoma Kipondo nami Tumekuja, lakini tulikuwa tunakutana kwenye masomo ya jioni. Kwanza tulikuwa kama marafiki tu, baadaye nikavutiwa naye na kumweleza hisia zangu na mambo yakawa sawa. Ukweli kunikubalia ombi langu halikuwa jambo rahisi na ilichukua kama miezi mitatu hivi.
Mwanaspoti: Kitu gani kilivutia ukampenda Hawa na si mwingine?
Awadh: Ni kwa sababu ya tabia yake, ana nidhamu na nilipomchunguza kwa umakini, nikagundua huyu anaweza kuwa mama bora wa familia yangu, lakini namfurahia zaidi anapokuwa jikoni, siyo kama najisifu, mke wangu anajua sana kupika, kila anachokipika huwa kitamu na anapopika biriani ndiyo ananimaliza kabisa kwa mahanjumati.
Mwanaspoti: Mna mtoto mmoja, malengo yenu ni kuwa na wangapi? Pia ni zawadi gani ukimletea mke wako huifurahia zaidi?
Awadh: Mambo mengine huwa ni mipango ya Mungu, ila mapenzi yangu ni kuwa na watoto wanne. Juu ya zawadi, hufurahia sana ninapomnunulia baibui la bei ghali.
Mwanaspoti: Kitu gani kilikufurahisha zaidi katika maisha yako?
Awadh: Ni siku nilipofunga ndoa na mke wangu Hawa pamoja na siku tulipopata mtoto kwa sababu katika maisha yangu nilitamani sana kuwa na mtoto.
MKE ALONGA
Mwanaspoti: Ehee...Nipe ukweli uhusiano wenu ulianzaje?
Hawa: Kweli kabisa, tulikutana shule na yeye alikuwa akinisaidia masomo kwa sababu alikuwa kichwa darasani, alijua sana masomo ya Biologia na Kiingereza ndiyo mwisho wa siku tukapendana.
Mwanaspoti: Na wewe ulikuwa unampenda au alikulazimisha na kwa nini ulichelewa kumkubalia.
Hawa: Kweli kabisa nilikuwa na nampenda sana, sikulazimishwa na mtu yeyote zaidi ya mapenzi yangu. Sababu kubwa ya kuchelewa kumkubalia ombi lake ni kwa sababu mimi mwanamke lazima nidengue, lakini kikubwa nilikuwa napenda namna alivyokuwa ananibembeleza, mimi nilikuwa nasikia raha.
Mwanaspoti: Wewe ni mpenzi wa soka na unapomwona Awadh uwanjani unajisikiaje?
Hawa: Mimi siyo mpenzi wa soka, nimeanza kupenda kwa sababu yake, ninapomwona anacheza huwa nafurahi sana na hasa anapofunga bao.
HISTORIA/MALENGO
Awadh ni Mtanzania mwenye asili ya Zanzibar, amezaliwa na kukua katika Kisiwa cha Unguja, Zanzibar mahali panapoitwa Mpendae. Amesoma masomo ya awali na msingi katika Shule ya Jang’ombe na Sekondari alisoma Tumekuja, alipofika Kidato cha Tatu alihamishiwa Makongo, Dar es Salaam.
Alianza soka tangu alipokua mdogo na kuendelea shuleni. Baadaye akachaguliwa na kituo cha soka cha TSA na baadaye kaenda Mtibwa kabla ya kuingia Simba.
Ni wa pili kuzaliwa katika familia ya watoto saba, ndugu zake wengine Ahlam na Zailam ambao ni wa kike, wakati madume wenzake ni Sabri, Tahil, Hamid na Nurdin.
Malengo yake ni kucheza soka la kulipwa, pia kufika mbali katika soka la kimataifa na hasa kuiwakilisha Tanzania akiwa na uzi wa Taifa Stars.