Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Man United ilianza kufa tangu 2009

Man United ilianza kufa tangu kwenye majira ya kiangazi mwaka 2009 chini ya kocha Sir Alex Ferguson, kabla hata Moyes hajatua Old Trafford kubeba mikoba ya kuinoa timu hiyo mwaka jana.

Muktasari:

  • Ni pengo kubwa sana na nafasi waliyopo ni mbaya pia baada ya kucheza mechi 22. Lakini, itakuwa kosa kubwa kumbebesha lawama kocha mpya David Moyes.

MANCHESTER, ENGLAND

MANCHESTER United ipo nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu England msimu huu, lakini hilo likiwa halitoshi pia ipo nyuma ya vinara Arsenal kwa tofauti ya pointi 14.

Ni pengo kubwa sana na nafasi waliyopo ni mbaya pia baada ya kucheza mechi 22. Lakini, itakuwa kosa kubwa kumbebesha lawama kocha mpya David Moyes.

Man United ilianza kufa tangu kwenye majira ya kiangazi mwaka 2009 chini ya kocha Sir Alex Ferguson, kabla hata Moyes hajatua Old Trafford kubeba mikoba ya kuinoa timu hiyo mwaka jana.

Hadi kufikia Mei 26, 2009 Man United ilikuwa na kikosi chenye nguvu sana, pengine kuliko misimu yote ya hivi karibuni tangu kile cha mwaka 1999.

Kipindi hicho, Man United walikuwa mabingwa England, Ulaya na Dunia. Ulikuwa ni mwaka waliotwaa taji lao la tatu mfululizo la Ligi Kuu England na walitinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu wa pili mfululizo.

Wakitokea kuifunga Chelsea kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 2008, mwaka 2009 miamba hiyo ya Old Trafford ilifika fainali nyingine ya Ulaya, safari hii walicheza na Barcelona mjini Rome, Italia.

Kubadilika kwa kikosi chao kilichoanza kwenye fainali hiyo tofauti na kile kilichonyakua ubingwa mbele ya Chelsea kulianza kutoa ishara ya kutosha kwa mashabiki wa timu hiyo kwamba imeanza kushuka.

Kikosi kile cha mwaka 2008 kilikuwa na wachezaji 11 makini, nyota wa viwango vya dunia waliokuwa kwenye ubora wa nguvu na uwezo wa kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Hata hivyo, kikosi cha sasa anachokirithi Moyes kimeachwa kwa mbali sana na kile cha 2008 na 2009.

Wachezaji makini waliokuwa kwenye vikosi hivyo baadhi wameuzwa, kuna waliostaafu na wengine umri umewatupa mkono, wamezeeka. Mbaya zaidi wachezaji waliokuja kuchukua nafasi zao si wapambanaji, waoga wanacheza wakiwa hawajiamini.

Mwaka 2009, Man United ilikuwa na mchezaji bora wa dunia, Cristiano Ronaldo, lakini ilikubali kumwacha aende Real Madrid japo kwa uhamisho ulioweka rekodi ya dunia wa Pauni 80 milioni.

Wengi waliamini kwa pesa hizo zilizopatikana, Man United ingeweza kumpata mbadala wa Ronaldo mwenye kipaji kikubwa, lakini badala yake kocha Ferguson alisafiri umbali mfupi tu hadi Wigan Athletic kumsainisha Antonio Valencia kwa Pauni 17 milioni.

Tangu Ronaldo alipoondoka Old Trafford amefunga mabao 232 huko Real Madrid, wakati kwa kipindi hicho Valencia amefunga mabao 21 tu Man United.

Kwenye safu ya kiungo kipindi hicho, Man United ilikuwa kwenye ulinzi wa Waingereza watatu makini, Owen Hargreaves, Paul Scholes na Michael Carrick, aliyekuwa kwenye ubora wake.

Kiungo hiyo haifanani na hii ya sasa, inayomhusisha ‘babu’ Carrick, Tom Cleverley, Marouane Fellaini, Nani na Ashley Young. Kuna pengo kubwa sana la ubora wa viungo kwa kikosi kile cha msimu wa 2008-09 na hiki cha sasa.

Kocha Ferguson amefanya kosa kubwa sana kwa kushindwa kununua kiungo makini wa kati kwa miaka sita ya hivi karibuni na hilo limeifanya timu hiyo kufa sehemu ya katikati ambayo ndiyo injini.

Mwaka 2008 na 2009, Man United ilikuwa na mabeki wasiopitika kirahisi, walikuwa kwenye ubora wao na umri pia ulikuwa ukiwabeba, walikuwa bado vijana wenye nguvu ya kupambana; Wes Brown, Rio Ferdinand, Nemanja Vidic na Patrice Evra. Hawa walitengeneza ukuta mgumu sana.

Hata hivyo, kwa sasa, Brown amekwenda Sunderland, wakati Evra, Ferdinand na Vidic bado wapo Man United, lakini umri umewatupa mkono na viwango vyao vimeshuka sana jambo ambalo halitashangaza kama wakitimuliwa mwisho wa msimu.

Ferguson alijaribu kuingiza vijana kwenye safu ya ulinzi baada ya kuwapandisha Rafael, Fabio na Jonny Evans na kisha kuwanunua Phil Jones na Chris Smalling, lakini mabeki hao wameshindwa kupanda viwango na kufikia wale waliowatangulia.

Sehemu pekee unaweza kuamini Man United imepata mtu makini walau wa kulingana na kikosi kile cha mwaka 2008 na 2009 ni kipa David de Gea, aliyerithi mikoba ya Mdachi Edwin van der Sar, licha ya kwamba Mhispaniola huyo ana kazi kubwa ya kufanya kufikia ubora wa mtangulizi wake.

Kwenye safu ya ushambuliaji ya sasa Wayne Rooney na Robin van Persie unaweza kuamini kwamba wanaweza kuifikia safu ile ya mwaka 2008 na 2009 iliyokuwa na Rooney na Carlos Tevez. Lakini, ukweli utabaki palepale Tevez si Van Persie.

Hivyo ni kitu kinachopingika kwamba Man United imeanza ‘kufa’ msimu huu kama wachezaji wa ubora ule wa miaka minne iliyopita, hawapo tena kikosini.

Si kitu kizuri kumlaumu Moyes, wakati ukweli upo bayana kwamba Ferguson anapaswa kubeba lawama zote kwa kushindwa kukibadili kikosi kipya kwa ubora ule ule kama ilivyokuwa mwaka 2008 na 2009.