Mambo yameanza kuiva Yanga

Mambo yameanza kuiva Yanga

Muktasari:

  • Yanga imepokea rasimu ya awali ya mchakato wa mabadiliko na kukabidhiwa mwenyekiti wa klabu hiyo Dk Mshindo Msolla ambayo imeandaliwa na kampuni ya La liga ya Hispania.

Yanga hawatanii bwana kwani tayari wameshapata rasimu ya awali ya mabadiliko  ambayo imekabidhiwa kwa mwenyekiti wa klabu  hiyo Dk Mshindo Msola kutoka kampuni ya La liga ya Hispania.

Katika hafla iliyofanyika leo Jumatano katika Hoteli ya Serena,Mwenyekiti wa Kamati ya mabadiliko ya klabu hiyo Wakili Alex Mgongolwa amekabidhi rasimu hiyo kwa mwenyekiti wa Yanga Dk Msola ikiwa ni hatua ya kwanza ya mchakato huo.

Akizungumza katika makabidhiano hayo Mgongolwa amesema baada ya vikao vingi na kampuni ya La liga ambao ndio waliopewa kazi ya kuishauri Yanga katika mabadiliko hayo ripoti hiyo imewasili na sasa kazi inayofuata ni kuifanyia kazi.

Mgongolwa amesema ripoti hiyo yenye kurasa 400 inakabidhiwa kwa uongozi wa klabu hiyo ikiwa ni hatua ya kuanza kufanyiwa kazi kulingana na ushauri ambao La liga walichopendekeza baada ya kuona jinsi Yanga inavyojiendesha.

"Dhamira kubwa ilikuwa ni kutazama mfumo mzuri utakaoweza kutumika katika kuipa dira ya maendeleo klabu hii,tuliona kuna haja ya kutafuta mtaalam na hatimaye tukawapata La liga ambao tulishirikiana nao katika vikao mbalimbali na sasa kazi wameikamilisha,"amesema Mgongolwa.

"Wameshauri mambo mengi katika ripoti hii na sasa tumeipokea ripoti yao na tunaikabidhi hii leo kwa uongozi wa klabu ili nao waipitie na kuangalia kipi kinachitakiwa kufanyika na wakati huo kamati yetu bado ipo tukisubiri wapi watahitaji msaada wetu ili nasi tufanye kazi yetu."

Akizungumza mara baada ya kupokea rasimu hiyo Msolla amesema baada ya kupokea ripoti hiyo sasa itakabidhiwa kwa mshauri wa mambo ya kiungozi Senzo Mbata ambaye atakwenda kuipitia akishirikiana na kamati yao ya utendaji.

"Tulimchukua Senzo pia kwa kazi hii,ripoti hii tutamkabidhi yeye na ataipitia akishirikiana nasi kamati ya utendaji lakini pamoja na sekretarieti na hapo atatushauri juu ya kipi tunatakiwa kukifanya." amesema Mgongolwa

Naye Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM,mhandisi Hersi Said ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo ya mabadiliko na aliyekwenda kuichukua ripoti hiyo nchini Hispania amesema ripoti hiyo mpaka kukamilika kwake kutaifanya Yanga kuwa klabu iliyopitia njia sahihi katika kubadilisha mfumo wake.

"Naamini kupitia ripoti hii pia zipo klabu sio tu hapa Tanzania bali hata Afrika zitakuja kuitafuta Yanga na kutaka kujifunza hatua hii ya mabadiliko,"amesema Hersi.

............................................

Na Khatimu Naheka