Prime
Mambo sita yaliyomng’oa Pedro Yanga
MWISHO wa safari ya Kocha Pedro Goncalves Yanga umefika baada ya mabosi wa klabu hiyo kuamua kuvunja naye mkataba kutokana na presha kubwa ya matokeo pamoja na hali ya sintofahamu iliyokuwa ikiendelea katika kikosi hicho.
Pedro alitambulishwa Yanga Oktoba 25, 2025 akiwa na wasifu wa kufundisha timu za taifa, lakini maisha ya klabu yenye presha kubwa kama Yanga yameonekana kumshinda katika siku 172 hadi Mei 6, 2026.
Pamoja na kuwa Yanga inaendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara, lakini bado kulikuwa na mambo mengi yaliyokuwa yakiwatesa mashabiki pamoja na viongozi wa timu hiyo jambo lililopelekea uamuzi wa kumuondoa kuchukuliwa.
Hapa kuna mambo sita yanayotajwa kuchangia uamuzi wa viongozi wa Yanga kufikia kumfuta kazi Pedro kama ambavyo taarifa yao ya Mei 6, 2026 iliyotolewa na Mtendaji Mkuu, Andre Mtine ilivyoeleza.
“Uongozi wa Klabu ya Young Africans unapenda kuutaarifu umma kuwa umemfuta kazi kocha mkuu wa kikosi cha kwanza Pedro Gonçalves. Uongozi wa Klabu unamshukuru Kocha Pedro Gonçalves kwa mchango wake alioutoa ndani ya klabu yetu na unamtakia kila la kheri katika majukumu yake yajayo.
“Katika kipindi hiki kikosi chetu kitakuwa chini ya uongozi wa Kocha Abdihamid Moalin pamoja na Kocha Patrick Mabedi hadi mwisho wa msimu,” ilieleza taarifa hiyo.
WACHEZAJI
Moja ya mambo yanayotajwa kumuweka Pedro kwenye wakati mgumu ni taarifa za baadhi ya wachezaji kutokuwa sawa na mfumo wake wa kazi pamoja na namna alivyokuwa akiendesha timu.
Ndani ya kikosi hicho, ilielezwa kulikuwa na nyota waliokuwa wakionekana kutofurahishwa na baadhi ya uamuzi wake hasa kwenye upangaji wa kikosi pamoja na mbinu zake za uchezaji.
Hali hiyo ilianza kuonekana hata uwanjani ambapo baadhi ya mastaa walionekana kupoteza morali na kushindwa kucheza kwa kiwango chao halisi kama ilivyokuwa mwanzo wa msimu.
Katika timu yenye mastaa wengi wenye majina makubwa kama Pacome Zouzoua, Allan Okello, Maxi Nzengeli, kushindwa kuwaweka wote kwenye mstari mmoja ni jambo ambalo linaweza kumuangusha kocha haraka sana.
USAJILI
Usajili wa mshambuliaji Laurindo Aurelio ‘Depu’ pamoja na Buba Jammeh pia umeonekana kuwa sehemu ya matatizo yaliyomponza Pedro ndani ya Yanga, kwani ndio mastaa aliowataka kwenye usajili wa dirisha dogo Januari 2026.
Wachezaji hao walikuja kwa matarajio makubwa ya kuongeza nguvu kwenye kikosi hicho, lakini kiwango chao hakikuendana na matarajio ya mashabiki wengi wa timu hiyo.
Licha ya kushindwa kuonyesha ubora wa kutosha, Pedro aliendelea kuwaamini na kuwapa nafasi mara kwa mara jambo ambalo lilikuwa likiwakasirisha mashabiki pamoja na baadhi ya wadau wa soka.
Katika baadhi ya mechi muhimu, safu ya ushambuliaji ya Yanga ilishindwa kutumia nafasi nyingi za mabao hali iliyoongeza lawama kwa mastaa hao pamoja na benchi la ufundi.
Wapo mashabiki walioamini Pedro alikuwa analazimika kuwachezesha mastaa hao kutokana na mazingira ya usajili wao jambo lililoonekana kuathiri ushindani katika kikosi, ukiachilia majeraha ambayo yalimweka nje Depu.
Kadri presha ya matokeo ilivyokuwa ikiongezeka, ndivyo lawama juu ya matumizi ya Depu na Buba zilivyozidi kuwa kubwa Yanga.
Hata hivyo, Depu ameonyesha kupambana kwani kuingia kwake dirisha dogo hakukumzuia kutikisa nyavu hivi sasa akiwa na mabao sita, manne nyuma ya kinara Feisal Salum mwenye kumi.
MACHAGUO
Jambo lingine linalotajwa kumponza Pedro ni uchaguzi wake wa kikosi ambao mara nyingi ulikuwa ukizua mjadala mkubwa kwa mashabiki.
Katika baadhi ya mechi, Pedro alikuwa akiwaacha benchi baadhi ya nyota waliokuwa kwenye kiwango kizuri huku akiwapa nafasi wengine ambao hawakuwa kwenye ubora mkubwa.
Maamuzi hayo yalifanya mashabiki wengi kuanza kuhoji uwezo wake wa kusoma mechi pamoja na kufanya maamuzi sahihi ya kiufundi.
Katika timu yenye ushindani mkubwa wa nafasi kama Yanga, kosa dogo la uchaguzi wa kikosi linaweza kubadili kabisa matokeo ya mchezo.
Wadau wengi wa soka waliamini Pedro hakuwahi kupata kikosi chake bora cha kwanza jambo lililoifanya Yanga kushindwa kuwa na muendelezo mzuri wa kiwango kwenye baadhi ya mechi.
Pia hata namna ya kuziingia mechi kubwa, Pedro alionekana kujaza viungo wengi wa kukaba ikitafsiriwa anakwenda na mpango wa kuzuia kwanza kabla ya kushambulia.
Katika siku za mwisho za kuifundisha Yanga, Pedro alifanya mabadiliko ya wachezaji yaliyoonekana kuigharimu timu hiyo, hiyo ilitokea kwenye fainali ya Kombe la Muungano na ndani ya dakika 30 za nyongeza, mabadiliko yake yalifanya Yanga kufungwa 1-0.
MATOKEO YA SIMBA
Lakini jambo ambalo lilionekana kumwongezea presha kubwa zaidi ni matokeo dhidi ya Simba kwenye Dabi za Kariakoo.
Mashabiki wengi wa Yanga walikuwa wanahitaji ushindi dhidi ya watani wao hao wa jadi, lakini Pedro alishindwa kufanya hivyo kwenye mechi mbili zilizochezwa katika muda mfupi.
Sare mbili dhidi ya Simba kwenye ligi na kichapo kutoka kwa Wekundu hao wa Msimbazi kilichofanya Yanga kuvuliwa ubingwa wa Kombe la Muungano, ilianza kuwafanya mashabiki wengi kupoteza imani naye huku wakiamini timu ilikuwa na uwezo wa kupata ushindi.
Tangu Pedro ajiunge na Yanga, alikutana na Simba kwenye mechi tatu tofauti za mashindano mawili ambayo ni ligi na Kombe la Muungano ambako Wekundu walitwaa ubingwa kwa kuifunga Yanga bao 1-0, huku ikitoka sare ya 2-2 na 0-0 katika mechi mbili za ligi msimu huu.
BENCHI LA UFUNDI
Pia maisha yake katika benchi la ufundi hayakuwa mepesi kutokana na namna alivyokuwa akifanya kazi na wasaidizi wake.
Taarifa mbalimbali zilieleza kuwa kulikuwa na tofauti za kimawazo ndani ya benchi hilo jambo lililoonekana kuathiri baadhi ya uamuzi wa kiufundi wa timu.
Ingawa tofauti ya mawazo ni jambo la kawaida kwenye soka katika Yanga hali hiyo ilianza kuonekana kuwa kubwa kutokana na presha ya matokeo.
Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti, benchi la ufundi halikuwa na mshikamano mkubwa jambo lililochangia timu kushindwa kucheza kwa mwendelezo mzuri. Hali hiyo nayo ilitajwa kuwa sehemu ya sababu zilizochangia mabosi wa Yanga kuona kuna umuhimu wa kufanya mabadiliko ya haraka kabla ya msimu kuharibika zaidi.
HISTORIA
Mbali na yote hayo, historia ya Pedro nayo iliwekwa mezani ikitajwa kuchangia hali hiyo.
Pedro alikuwa na uzoefu mkubwa kwenye timu za taifa, lakini hajawahi kufundisha klabu huku akianza na yenye presha ya matokeo ya kila siku kama Yanga.
Tofauti kati ya timu ya taifa na klabu ni kubwa sana kwani kwenye klabu kocha anaishi na presha ya mashabiki, viongozi pamoja na vyombo vya habari kila siku.
Timu ya taifa, wachezaji hukai nao muda mrefu, bali ni kwa kipindi fulani cha mashindano, lakini presha yake si kubwa sana kulinganisha na klabu. Wapo walioamini Pedro alikuwa bado anajifunza mazingira ya soka la klabu huku wengine wakiona ukubwa wa Yanga ulimzidi mapema.
Mwisho wa siku, mambo hayo yote yaliungana na kupelekea uamuzi wa mabosi wa Yanga kuamua kumaliza safari yake ndani ya kikosi hicho cha wananchi katika mechi dhidi ya KMC ambapo Yanga ilishinda bao 1-0, Mei 6, 2026.
Rekodi zinaonyesha makocha wenye uzoefu na timu za taifa, wanapata wakati mgumu wakifundisha klabu, hilo pia limemtokea Marcio Maximo ambaye hakufanya vizuri akiwa Yanga, pia alipoifundisha KMC, pia hakuwa na wakati mzuri tofauti na ilivyokuwa Taifa Stars.
Pedro rekodi zinaonyesha kabla ya kutua Yanga, kuanzia 2018 hadi 2025 alifundisha timu za taifa ambazo ni Angola U17 (2018–2019), Angola U20 (2018–2019) na timu ya taifa ya Angola (2019–2025), ndipo akatua Yanga.
Kabla ya hapo, alipita klabu akiwa msaidizi katika timu za Amora ( 1996–1997) na Cova da Piedade (1997–2000), skauti wa Sporting CP (2000–2001) na kusimamia soka la vijana Sporting CP (2001–2015) na Primeiro de Agosto (2015–2018).