Mambo haya manne kuirudisha Yanga kwenye mstari

Muktasari:

Akizungumza na Mwanaspoti, Msumi alisema hana wasiwasi na wagombea waliochukua fomu lakini kubwa analotamani kuona linafanywa na wagombea hao au viongozi watakaopata nafasi ya kuiongoza Yanga ni kuvunja makundi, kufuata sheria za Baraza la Michezo Tanzania (BMT), kufuata mwongozo wa katiba ya klabu, ubunifu wa kutafuta vyanzo vya mapato na kuandaa timu imara na kuisimamia.

KUELEKEA uchaguzi wa klabu ya Yanga, Mohammed Msumi ametaja mambo manne ambayo wagombea nafasi mbalimbali za uchaguzi mkuu wa klabu hiyo yatakayorudisha hadhi ya klabu yao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Msumi alisema hana wasiwasi na wagombea waliochukua fomu lakini kubwa analotamani kuona linafanywa na wagombea hao au viongozi watakaopata nafasi ya kuiongoza Yanga ni kuvunja makundi, kufuata sheria za Baraza la Michezo Tanzania (BMT), kufuata mwongozo wa katiba ya klabu, ubunifu wa kutafuta vyanzo vya mapato na kuandaa timu imara na kuisimamia.

Alisema mambo hayo makuu manne yakifuatwa timu ya Yanga atarudi katika mstari na kuwa miongoni mwa timu zitakazokuwa na ushindani wa hali ya juu ndani na nje ya nchi na kuongeza kuwa wakipatikana viongozi imara hayo yote yanawezekana.

“Yanga iliundwa kwa misingi minne, kufahamiana, kukutana kupanga mikakati, kualikana kwenye sherehe na kusaidiana na kujumuika katika tatizo la misiba hayo yote yamekufa, sasa hivi klabu imegawanyika makundi, hivyo kuirudisha kwenye mstari ni kufanya hayo mambo manne niliyoyasema.”

“Yanga imeyumba inapitia kipindi kigumu lakini napenda kuwapongeza wanachama wa Dodoma kwa kitu kikubwa walichokifanya cha kuichangia klabu yao ni mwanzo mzuri na naamini tunaweza kuiendesha klabu yetu kwa kujichangisha wenyewe na sio kumtegemea kiongozi mmoja kwani anaweza akafa na klabu ikabaki na ndio maana kulikuwa na viongozi waliondoka na Yanga bado ipo tumeikuta.”

Msumi aliongeza kuwa wanachama ambao wamechukua fomu wakiwa na lengo la kujinufaisha wenyewe, hawana nafasi na amewaomba wanachama wa timu hiyo kuachana na tamaa za fedha za muda mfupi waangalie maslahi ya klabu yao kwa kuwa makini wakati wa uchaguzi.