Makocha wabishana kutimuliwa Zahera

Muktasari:

Kwa sasa mikoba ya Zahera amekabidhiwa aliyekuwa mchezaji, kocha na Katibu Mkuu, Boniface Mkwasa kwa muda. Zahera ameondolewa baada ya kuinoa Yanga kwa kipindi cha takribani msimu mmoja na nusu.

BAADA ya Yanga kusitisha mkataba wa Kocha Mkongo, Mwinyi Zahera, makocha mbalimbali wamezungumzia uamuzi huo kwa mitazamo tofauti.

Kwa sasa mikoba ya Zahera amekabidhiwa aliyekuwa mchezaji, kocha na Katibu Mkuu, Boniface Mkwasa kwa muda. Zahera ameondolewa baada ya kuinoa Yanga kwa kipindi cha takribani msimu mmoja na nusu.

MECKY MAXIME

Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime alisema: “Yanga hawakutakia kumwacha Zahera katika kipindi hiki kwanza kwangu ni mwalimu mzuri, ni matokeo tu ambayo angeweza kuyaweka sawa katika siku zijazo.”

“Ilitakiwa wamvumilie kwa sababu mechi za ligi bado kabisa unamhukumu kwa kitu gani,” alisema Maxime.

Alisema, Yanga ni kama wamefanya maamuzi ya haraka bila kuangalia mbele zaidi na walihitaji kuwa na subira.

ABDALLAH MOHAMMED ‘BARES’

Kocha wa JKT Tanzania, Mohammed Abdallah ‘Bares’ alisema, maamuzi waliyofanya ni mapema mno.

“Walitakiwa kumpa muda. Wamefanya maamuzi mapema mno kama ni Ligi Kuu bado changa na mshindano ya nje, Yanga ina timu changa ambayo ilitakiwa kukaa pamoja kwa kipindi kirefu ili wapate matokeo mazuri,” alisema Bares.

PATRICK MWANGATA

Kocha wa makipa wa Mtibwa Sugar, Patrick Mwangata amesema, si kitu sahihi ambacho Yanga wamekifanya kwa kumwondoa Kocha Mwinyi Zahera.

“Hivi mtabadilisha makocha mpaka lini, wamechunguza na kujua tatizo lililopo kwenye timu kama wameona yeye ndio tatizo sawa. Kama unamjaji kwa matokeo, Ligi Kuu bado na wao hawajacheza mechi nyingi na kama ni Ligi ya Mabingwa, Yanga haikuwa kwenye programu ya mashindano hayo,” alisema Mwangata.

“Katika Ligi ya Mabingwa hawakufanya hayo maandalizi kwa sababu hawakuwa kwenye programu ikatokea wameingia kwa bahati tu. Binafsi naona si sahihi na maamuzi hayo yanaweza kuwapa faida wapinzani wao kama Simba.”

IDD PAZI

Kipa na kocha wa zamani wa Simba, Idd Pazi amesema, Yanga walitakiwa kumpa muda Zahera.

“Wangempa muda mpaka dirisha dogo. Anaweza kuwa amefanya makosa lakini alikuwa na muda wa kurekebisha kama kukaa na timu yake kwa sababu ni mpya na kuitengeneza.”

“Wangemwachia dirisha dogo afanye mabadiliko na kutengeneza kikosi chake kwa sababu inaonekana mwanzo ni kama alifanya makosa kwa baadhi ya wachezaji na alikuwa anarekebisha,” alisema Pazi.

“Makosa aliyofanya ni kuwatoa wachezaji kama Mrundi Amissi Tambwe na Mzimbabwe Thabani Kamusoko ambao katika ligi ya Tanzania wanaimudu.”

MOHAMMED TAJDIN

Kocha wa zamani wa Alliance FC, Mohammed Tajdin alisema kumalizana na kocha huyo inategemea na makubaliano yao kama mwaka jana walivumiliana na kumaliza kwa matokeo hayo inawezekana msimu huu kuna mambo waliyokuwa wamepanga.

“Mbali na makubaliano binafsi binafsi Zahera alikuwa anakwenda kinyume na maadili ya ukocha katika baadhi ya mambo kama kubishana, kukosoa mamlaka kama TFF au wachezaji wake hadharani,” alisema Tajdin.

HASSAN BANYAI

Kocha wa zamani wa Geita Gold inacheza Ligi Daraja la Kwanza, Hassan Banyai alisema, suala la Yanga na Mwinyi Zahera linategemea na mambo mengi.

“Kwanza makubaliano yao baada ya msimu kumalizika. Inawezekana vitu ambavyo walikubaliana havikwenda sawa na ndio maana wakaamua kuachana naye,” alisema Banyai.

“Alikuwepo kwenye usajili wa dirisha kama wachezaji walioingia ni mapendekezo yake anastahili kuondoka, lakini kama aliopendekeza hawakuingia hastaili kulaumiwa.”

HEMED MOROCCO

Aliyekuwa kocha msaidizi wa Taifa Stars, Hemed Morocco alisema, “Kusitishwa kwa mkataba kunategemea na mambo mengi binafsi ningeweza kuzungumza zaidi kama ningejua makubaliano yao.”