Makocha: Dabi hii haina mwenyewe

Muktasari:

  • Timu hizo zitavaana kuanzia saa 11:00 jioni likiwa ni pambano la 112 katika Ligi Kuu tangu kuasisiwa kwa Ligi ya Bara mwaka 1965, huku matokeo ya mechi za duru la kwanza yakiwa mabaya kwa Simba kwa kuchapwa mabao 5-1 na watani wao wanaoongoza msimamo wa ligi hiyo kwa sasa.

MASHABIKI wa soka nchini wameanza kuhesabu siku kabla ya kuzishuhudia Simba na Yanga zikivaana katika mechi ya marudiano ya Kariakoo Derby ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa Jumamosi ya wikiendi hii Kwa Mkapa.

Timu hizo zitavaana kuanzia saa 11:00 jioni likiwa ni pambano la 112 katika Ligi Kuu tangu kuasisiwa kwa Ligi ya Bara mwaka 1965, huku matokeo ya mechi za duru la kwanza yakiwa mabaya kwa Simba kwa kuchapwa mabao 5-1 na watani wao wanaoongoza msimamo wa ligi hiyo kwa sasa.

Wakati presha ya mechi hiyo ikianza mapema kwa makocha na wachezaji, wadau mbalimbali wa soka hususani makocha wametoa maoni na mitazamo yao kwa kusema wanaiona dabi ya tofauti safari hii, kwani bado haina mwenyewe, licha ya Simba kuonekana kuchechemea zaidi kwa sasa kulinganisha na watani wao, Yanga.

Makocha hao waliliambia Mwanaspoti Dabi ya Aprili 20 ambayo Yanga ndio wenyeji itatawaliwa zaidi na mbinu na ufundi wa makocha, kuamua mchezo tofauti na matokeo ya mechi iliyopita iliyomfuta kazi kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ baada ya kichapo cha 5-1 cha mechi ya Novemba 5 mwaka jana.

Makocha na wachezaji wa zamani wa soka nchini, licha ya kukiri Yanga inaonekana kuwa vizuri na kuwa na asilimia kubwa ya kuibuka na ushindi, lakini hawaoni kama dabi inazoeleka, hivyo wanaamini lolote linaweza likatokea Kwa Mkapa.

Kocha Meja Mstaafu, Abdul Mingange alisema katika maisha yake hajawahi kuiona dabi nyepesi na anachokitarajia ni kuona mbinu za makocha Abdelhak Benchikha (Simba) na Miguel Gamondi (Yanga) zikiamua mchezo huo.

“Ukiangalia morali ya mashabiki wa Simba ipo chini, tofauti na Yanga, lakini mfano mzuri nani alitarajia Yanga ingeweza kuonyesha ushindani mkali dhidi ya Mamelodi Sundowns FC ama Simba licha ya kufungwa na Al Ahly lakini ilicheza vizuri,” alisema kocha huyo wa zamani wa Mbeya City, Ndanda na Azam FC na kuongeza;

“Wakati Simba inachukua mataji kwa mfululizo, Yanga ilikuwa inajipanga, vivyo hivyo Simba inatakiwa ijipange wakati huu Yanga inavyofanya vizuri, lakini haina maana kwamba dabi itakuwa rahisi.”

Staa wa zamani wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ alisema ingawa Simba katika mechi ya mzunguko wa kwanza ililala kwa mabao 5-1, hilo haliwezi kuufanya mchezo wa Aprili 20, uchukuliwe poa.

“Yanga wasije wakaingia uwanjani kwa kujiamini na kuidharau Simba, kiufundi siyo mbaya ingawa ipo kwenye upepo wa kupata matokeo ya kuwafurahisha mashabiki wake na tangu nilivyokuwa nacheza hadi leo sijawahi kuona dabi nyepesi,” alisema.

Mmachinga alisema ikumbukwe Simba ilichukua ubingwa wa Ligi Kuu mara nne mfululizo kabla ya Yanga kupindua meza msimu wa msimu wa 2021/22 na 2022/23.

Mchezaji mwingine wa zamani aliyezungumzia hilo ni kipa wa zamani wa Simba na Yanga, Ivo Mapunda alisema: “Dabi haizoeleki, anayejipanga vizuri kwa siku husika ndiye anayeshinda.”

Katika mechi 111 zilizopita za Kariakoo Derby katika Ligi ya Bara tangu 1965, rekodi zinaonyesha Yanga imeshinda mara 39, huku ikipoteza 32 mbele ya Simba na michezo 40 ilimalizika kwa sare tofauti.

Katika mechi hizo Yanga imevuna jumla ya mabao 118 na kufungwa 104, lakini vipigo vikubwa zaidi vikiwa ni vya mabao 5-0 Yanga ikiifumua Simba mwaka 1968, kabla ya Simba kujibu mapigo kwa kuinyoosha Yanga 6-0 mwaka 1977 na kurudia tena mwaka 2012 ilipoitandika mabao 5-0 na mwaka jana Yanga ikalipa kisasi kwa 5-1.

Timu hizo zitakutana Jumamosi zikuwa katika nafasi tofauti, Yanga ikiongoza msimamo na Simba ikishika nafasi ya pili na zote zikitoka kucheza na timu zinazofanana majina, Simba ikicheza na Singida Black Stars (zamani Ihefu) wakati Yanga ikitoka kuumana na Singida Fountain Gate iliyohamia Mwanza kutoka Singida.