MAKOCHA 45 WAOMBA KAZI YANGA, MASTAA WATATU KUFYEKWA

YANGA ilitumia dakika zisizozidi 15 juzi usiku kumfuta kazi Kocha Cedrick Kaze. Waliingia tu hotelini wakakutana dakika chache wakakubaliana kumuita na kumtakia kila la heri kisha wakafuata wasaidizi wake kwa staili hiyo.

Uongozi umethibitisha kwamba kabla ya wikiendi watakuwa wameshapata Kocha Mkuu lakini Mwanaspoti linajua kwamba kuna wazawa wawili na Mkenya mmoja wanachuana vikali kupewa jukumu la kusimamia kwa muda.

Kabla ya mabosi wa Yanga hawajaenda kula jana walishapokea majina ya Makocha 45 wakiomba kazi lakini wamekubaliana timu itakaa chini Adolf Rishard(Kocha wa zamani wa Prisons) au Mecky Maxime(Kocha wa zamani wa Kagera) ambao ni wazawa pamoja na Mkenya, Ben Mwalala(Kocha wa zamani wa Bandari) ambaye ni straika wa zamani wa Yanga aliyewafutia uteja kwa Simba katikati ya miaka ya 2000.

Licha ya kwamba Yanga wamekuwa wasiri kuweka wazi majina kwa madai kwamba hawajamalizana nao lakini Mwanaspoti limepenyezewa kwamba watatu hao yoyote anaweza kula shavu kwavile wanaijua vilivyo Yanga.

Taarifa za uhakika ambazo Mwanaspoti imezipata ni kwamba Yanga inataka kuanza na kocha ambaye anaijua klabu hiyo kwa ndani au ligi ya Tanzania ingawa hata uwezekano wa Juma Mwambusi kurudi bado ni mkubwa kwani inaelezwa yupo Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Yanga Dominic Albinius ameliambia Mwanaspoti kwamba wanataka mchakato huo kumalizika haraka ndani ya wiki moja.

“Haya ni maamuzi mazito na sasa lazima tupate Kocha wa haraka ambaye atakuja kuchukua nafasi ya makocha ambao tumewaondoa,” alisema Albinius.

Mastaa wa timu hiyo, waliamshwa juzi usiku kambini wakikumbushwa kila mchezaji amekuja peke yake katika klabu hiyo.

Wapo pia wachezaji wasiopungua watatu watawekwa kitimoto mara baada ya timu hiyo kurejea jijini Dar es Salaam kwa makosa ya kinidhamu.

Kauli hiyo pia imethibitishwa na Albinius ambaye alisema; “Tumeanza tu makocha kwa kuwa katika hali kama hii timu inapokosa utulivu wa matokeo mazuri wa kuwajibishwa ni makocha lakini tukimaliza hapa tutawafuata na wachezaji huko tutaangalia nidhamu na uwajibikaji, tunawalipa kila kitu wachezaji lakini wapo ambao wameshindwa kuonyesha uwezo.”