MAKALA MAALUM: Kwa Mkapa patanoga - 2

KATIKA toleo lililopita tuliona jinsi kamati maalum yakukagua maandalizi ya michuano ya Super 8 ya CAF, itakayozihusisha klabu kubwa zinazofanya vizuri Afrika na zenye mashabiku wengi, ikiwemo Simba kutoka Tanzania, ilibaini upungufu mkubwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kutoa mapendekezo ya uboreshwaji. Endelea nayo


DAWA ZA KUONGEZA NGUVU
Kamati hiyo ya Caf, imeshauri pia uwanja huo unatakiwa kuwa na ofisi maalum kwa ajili ya kupima matumizi ya dawa za kuongeza nguvu michezoni.
Kamati hiyo inataka ofisi hiyo iwe karibu na vyumba vya kubadilishia nguo vya wachezaji.
Inatakiwa kuwa na sehemu maalumu kwa ajili ya wagonjwa kusubiri ambayo inaweza kumudu kuwa na watu nane kwa wakati mmoja, pia inashauriwa kuwa na choo cha kujitegemea kikiwa na funguo maalum, kunatakiwa kuwa na televisheni, vinywaji ambavyo havina kilevi, friji maalum pia maji yenye madini, sehemu ya kuweka taka, karatasi pamoja na chupa.
Kiongozi kwenye ofisi hiyo anatakiwa kuwa na meza moja ambayo itakuwa imezungukwa na viti vinne, beseni moja la kunawia mikono au matumizi mengine, ofisi hiyo inatakiwa kuwa na kabati maalum lenye ufunguo maalamu, maji yanatakiwa kuwepo muda wote kuwe na kioo maalum.


MAJUKWAA YA UWANJA
Uwanja wa Mkapa ambao una viti 60,0000 inatajwa kuwa mmoja kati viwanja bora hapa nchini, hata hivyo kamati hiyo maalum ya Super8 imesema unatakiwa kuwa na mabadiliko makubwa sana kwenye majukwaa.
Imesema viti vinatakiwa kubadilishwa vyote baadhi ya viti ni vya zamani na vimebaduka rangi hivyo havina rangi yake halisi, lakini vingine vimelegea hivyo vinatakiwa kufanyiwa marekebisho.
Wanasema mamlaka zinahusu majanga ya moto ni lazima zitoe kibali kwenye uwanja kwa ajili ya usalama wa mashabiki waliopo uwanjani.


CHOO
Caf wanasema kwenye eneo la choo kwa ajili ya mashabiki kunahitaji mabadiliko makubwa, kunatakiwa kubadilisha masinki, mfumo wa maji ubadilishwe ikiwa ni pamoja na kufungwa mabomba mapya kwa kuwa yaliyopo yameharibika.
Huduma ya kwanza:
Uwanja wa Mkapa unatakiwa kuwa na ofisi za huduma ya kwanza kwenye kila eneo, yaani mzunguko, vip A,B,C na sehemu nyingine za uwanja huo, ikiwemo gari la wagonjwa wakati wa mechi.


VIP NA VVIP
Caf wanataka Uwanja wa Mkapa ufungwe viti maalum kwa ajili ya mashabiki au viongozi wanaokaa kwenye eneo hili na hawataki viti vya kuwekwa na kutolewa kama ambavyo inafanyika kwenye baadhi ya michezo kwa sasa.
Wanasema viti hivyo vinatakuwa kuwa na umbali ambao hauwezi kumsumbua mtu kupita, lakini lazima viwe kiwango cha juu chenye hadhi ya eneo lenyewe.


SEHEMU YA WAANDISHI WA HABARI
Kamati hiyo chini ya Caf imesema wazi sehemu hii haina viwango vinavyotakiwa na Shirikisho hilo, hivyo kunatakiwa mabadiliko makubwa kabla Super8, haijanzaa.
Imesema pamoja na mambo mengine, kunatakiwa kuwa na ofisi moja ambayo itakuwa na televisheni, inteneti, meza pamoja na simu ya mezani ambayo itakuwa ya hapo hapo.
Wanashauri inteneti iliyopo hapa inatakuwa kuwa pia kwenye sehemu ya waandishi wa habari ya kufanyia mahojiano.
Wanasema pia hawajaridhishwa na sehemu ya kufanyia mahojiano na hivyo kunatakiwa kufanyika mabadiliko makubwa kabla ya michuano hiyo.
Kamati imeshauri eneo hilo linatakiwa kuwa na viti 50 au zaidi kwa ajili ya waandishi, panatakiwa kuwa na sehemu maalum ya kuweka camera, kuwe na viti pamoja na meza maalumu kwa ajili ya makocha zile ambazo zimepitishwa na Shirikisho la Soka Caf. Pia wameshauri mazingira mazuri ya kuchuja sauti tofauti na hali ilivyo kwa sasa.


WAPIGAPICHA
Kamati hiyo maalumu ilishauri kuwa nyuma ya magoli ndiyo iwe sehemu maalum kwa wapigapicha, lakini panatakiwa kuwa na sehemu ya kuchomeka kamera kwenye chaji, kuwe na intaneti  ya uhakika muda wote.


VIWANJA VYA MAZOEZI
Caf wanasema pamoja na baadhi ya viwanja vimeanza kufanyiwa marekebisho na serikali, lakini wanaamini kuwa bado kuna sehemu viwanja hawavijakaa vizuri na wanapendekeza:
Wanapendekeza kuwa kwenye kila kiwanja cha mazoezi kunatakiwa kuwa na gari la kubebea wagonjwa muda wote wa mazoezi.
Kuwa na angalau chumba kimoja cha kubadilishia nguo na mabenchi yenye viwango cha Caf, pia nyasi ziwe kwenye kiwango kinachotakiwa.


HOTELI
Hata hivyo, kamati hiyo iliridhishwa na hoteli zilizopo nchini na hawakuwa na jambo lolote la kushauri kwenye eneo hili.