MAKALA: Kaa mbali na Simba
Muktasari:
Mabao yao saba yalifungwa kutoka pande zote za uwanja. Mabao matatu yalitokea katikati, mabao mengine mawili kushoto na mengine kulia.
SIMBA wamekuwa watamu kwelikweli. Wamefungua pazia la Ligi Kuu Bara kwa kutoa kifurushi cha wiki kwa Ruvu Shooting ya Pwani. Kuna kipi zaidi unachoweza kusema zaidi? Simba imerudi.
Usajili wa wachezaji 13 uliofanyika msimu huu pengine utaacha makovu makubwa kwa timu shiriki za Ligi Kuu. Mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu wanacheza soka la kasi, pasi fupi na ndefu huku wakitengeneza mashambulizi kupitia pande zote za uwanja.
Mabao yao saba yalifungwa kutoka pande zote za uwanja. Mabao matatu yalitokea katikati, mabao mengine mawili kushoto na mengine kulia. Hakuna shaka kwamba Simba iko vizuri sasa uwanjani.
Safu ya ulinzi ya Simba imeonyesha iko imara sana. Nahodha Method Mwanjali ametengeneza kombinesheni nzuri na Salim Mbonde. Katika mechi ya juzi, Kocha Joseph Omog alijaribu pia kuanza kumtumia Juuko Murshid katika kipindi cha pili.
Yote kwa yote, wiki ya kwanza ya ligi imeonyesha mambo mengi. Achana na mechi ya Yanga na Lipuli jana, mechi saba za Jumamosi zimeonyesha msimu huu huenda ukawa na ushindani mkali. Kwanza hakukuwa na mechi iliyomalizika kwa sare.
OKWI KATIKATI
Kasi ya Emmanuel Okwi imepungua kidogo, uwezo wake wa kupiga chenga umepungua pia lakini bado anafahamu vizuri kufunga. Ameonyesha anaweza kufanya vizuri zaidi akicheza kama straika wa kati na siyo winga.
Tazama mabao yake manne ya mechi ya juzi dhidi ya Ruvu, yote alifunga akitokea katikati. Akili ya Okwi inafanya kazi. Ni mjanja na anajua namna ya kuwachomoka mabeki na kufunga. Anajua namna ya kukwepa mtego wa kuotea pia. Kiungo wa Simba, Mzamiru Yassin naye ameonyesha kuwa anajua kumchezesha Okwi vizuri. Pamoja na yote, Erasto Nyoni pia yuko vizuri.
AZAM BADO WAMO
Nani anasema Azam imefulia? Mwambie yaliyotokea huko Mtwara, Azam imeifunga timu sumbufu ya Ndanda bao 1-0. Azam haitazamwi kama timu yenye nguvu tena baada ya kuwaachia mastaa wake John Bocco, Shomary Kapombe, Erasto Nyoni na Aishi Manula kutua Simba.
Hata hivyo, Kocha Aristica Cioaba ameiunda Azam mpya. Inatengeneza mashambulizi kupitia pande zote. Straika Mghana, Yahya Mohammed amezidi kuimarika na bao lake pekee la ushindi limeifanya Azam kuanza kwa ushindi.
NDAYIRAGIJE NI KOCHA
Mbao bado ipo, tena sana tu. Imeanza kwa kuishangaza Kagera Sugar kwa kuifunga bao 1-0 tena kwao, Kaitaba.
Nani alitegemea hili linaweza kutokea? Mbao hii haina Salimin Hoza, Pius Buswita, Jamal Mwambeleko, Emmanuel Mseja wala Benedict Haule.
Ni Mbao ambayo imeondokewa na mastaa wake wote, lakini bado inaupiga mpira mwingi sana.
Silaha kubwa ya Mbao ni kocha wake Mrundi, Etienne Ndayiragije. Anafahamu namna ya kuifanya timu icheze bila kutegemea staa mmoja. Inacheza soka la pasi fupi, inabana uwanja na inacheza kwa kujiamini. Kagera mpaka sasa haiamini kilichotokea.
SINGIDA KARIBU
Matokeo ya kushtua yalikuwepo mkoani Shinyanga pale Singida United ilipofungwa mabao 2-1 na Mwadui. Singida siyo timu ya mchezomchezo kabisa bana.
Imesajili wachezaji 16 wapya, tena wa viwango vya juu. Inafundishwa pia na kocha mwenye mafanikio, Hans Van Pluijm lakini iliambulia kipigo katika mchezo wa kwanza tu.
Yote kwa yote mchezo huo ulionyesha Mwadui inazidi kuimarika. Kitendo cha kuwabakisha wachezaji wake muhimu kama Hassan Kabunda, Razack Khalfan, Awadhi Juma na Paul Nonga kinaendelea kuifanya iwe timu ya ushindani. Singida iendelee kujipanga, pengine itachanganya baadaye.
BARES AMEANZA
Kocha wa Prisons, Abdallah Mohammed ‘Bares’ naye ameonyesha alihitaji muda kidogo kuitengeneza Prisons mpya. Kama hujagundua ni kwamba, Prisons ndio timu pekee iliyopata ushindi ugenini wikiendi hii baada ya kuifunga Njombe Mji mabao 2-1.
Bares, ambaye aliisaidia Prisons isishuke daraja msimu uliopita, ameanza kupata mchanyato wa kikosi anachokihitaji baada ya kusimamia usajili wote na kuiandaa timu vizuri.
Pengine msimu huu Prisons inaweza kurejea kwenye ushindani tena.
KATWILA AMEANZA
Msimu uliomalizika haukuwa mzuri sana kwa Kocha wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila. Kocha huyo alijikuta akipata matokeo yasiyoridhisha punde baada ya kuachiwa timu na Salum Mayanga.
Hata hivyo, baada ya kufanya usajili na kuiandaa timu kuendana na mfumo wake, Mtibwa imeanza kwa kuichapa Stand United bao 1-0. Pengine Katwila ameanza kupata aina kikosi alichokitazamia. Tumpe muda kidogo kuona kama ana mapya zaidi.
HUKO MBEYA
Mpaka sasa bado sijafahamu Mbeya City ni imara ama Majimaji ni dhaifu? Mbeya imeifunga Majimaji bao 1-0 lakini matokeo hayo hayanifanyi kuamini timu hiyo ni imara sana.
Kocha Mohammed Kijuso amefanikiwa kupata matokeo mazuri katika mechi yake ya kwanza, lakini bado ana safari ndefu kwelikweli. Kuifunga Majimaji siyo jambo la kujisifu sana kwani, bado hawako vizuri sana.