Majeraha yamtesa Boateng

Muktasari:

  • Beki huyo Mjerumani alikuwa ni nguzo muhimu katika safu ya ulinzi wa Bayern kwa muda wote alikuwa na kikosi hicho.

Beki kisiki wa timu ya Bayern Munich, Jerome Boateng amekata tamaa ya kurejea uwanjani kutokana na majeraha.

Libero huyo amevurugwa baada ya kupata majeraha anayodai yanaweza kuzima ndoto yake ya kuitumikia Bayern Munich katika majira ya kiangazi.

Hata hivyo, alisema atakuwa pamoja na kocha wake Jupp Heynckes katika kampeni ya kuwania ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ujerumani.

Alisema hafikirii kurejea uwanjani mapema kutokana na majeraha aliyopata. Beki huyo alikwenda kuteta na vigogo wa bodi ya klabu hiyo kujua hatima yake.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani, alijiunga na Bayern Munich mwaka 2011 kutoka Manchester City na amekuwa tegemeo katika kikosi cha kwanza.

Boateng amecheza mechi 13 za Ligi Kuu Ujerumani chini ya kocha Carlo Ancelotti kabla ya Mtaliano huyo kutupiwa virago wiki chache zilizopita.

"Nimezungumza na wakurugenzi kuhusu hatima yangu katika majira ya kiangazi, lolote linaweza kutokea kwa sababu naona kama sikupati ushirikiano sijui kwa sababu sijacheza mechi nyingi kutokana na majeraha au vinginevyo," alisema Boateng mwenye miaka 29.

Beki huyo aliibua mzozo na Ancelotti akidai kutotumika kikamilifu katika mechi za Ligi Kuu ikiwemo dhidi ya Paris Saint Germain (PSG) waliochapwa mabao 3-0.