Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Majaliwa: Makocha wanaojua Kiswahili wapewe kipaumbele

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (katikati) akiwa na Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Dk Damas Ndumbaro (kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera wakati kongamano la nne la Idhaa za Kiswahili Duniani lililoanza jana Machi 18 na kuhitimishwa Ijumaa wiki hii jijini Mbeya

Muktasari:

  • Kongamano hilo ni la nne tangu kuanza kwake mwaka 2007, ambapo mwaka huu lilikuwa na kauli mbiu ya 'Tasnia ya Habari na Fursa za Ubidhaishaji Kiswahili Duniani' ambalo limefanyika jijini Mbeya.

Mbeya. Ili kuhakikisha lugha ya Kiswahili inaendelea kuenezwa na kutangazwa ndani na nje ya nchi, waandishi wa habari za michezo nchini wametakiwa kufanya mahojiano na makocha wanaojua lugha hiyo ili kuwapa haki walaji wa habari.

Akizungumza jijini hapa jana Machi 18, katika kongamano la nne la Idhaa za Kiswahili Duniani, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema waandishi wanaofanya habari za michezo lazima kutumia makocha wanaojua Kiswahili ili kuwapa haki walaji.

Amesema zipo timu ambazo zinao makocha wa kigeni ambao hawaijui lugha ya Kiswahili, hivyo kufanya mahojiano kwa lugha ya kigeni ni kuwanyima haki wasikilizaji.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema wanafurahia kuona baadhi ya timu zinazosajili wachezaji wa kimataifa ambao wanapofika huanza kujifunza Kiswahili akisema hiyo ni hatua kubwa.

"Waandishi mnaokuwa kwenye michezo baada ya mechi kama kocha ni wa kimataifa hajui Kiswahili tumieni wasaidizi ili kumpa mlaji haki yake, lakini tunaipongeza Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo kwa kazi nzuri," amesema Majaliwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Wizara hiyo, Dk Damas Ndumbaro amesema michezo imekuwa sehemu iliyochangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza luga ya Kiswahili.

Dk Ndumbaro ametoa baadhi ya maneno ambayo hutumika kutangaza michezo ikiwa ni 'kujenga kibanda' akimaanisha kuotea na 'kumwaga maji' akimaanisha kupiga krosi.

"Juzi nilikuwa Tanga katika mashindano ya Odo Ummy Cup mtangazaji akasema mchezaji tayari amejenga kibanda, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akauliza ndio nini nikamjibu anamaanisha kuotea," amesema na kuongeza:

"Lakini wengine utasikia wanasema Lomalisa (Joyce) anamwaga maji wakimaanisha kupiga krosi, hii ni namna ambavyo michezo inakuza na kusambaza kiswahili," amesema Dk Ndumbaro.

Waziri huyo ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya awamu ya sita wamefanikiwa kufanya kongamano hilo kwa miaka mitatu mfululizo (2022, 2023 na 2024), na pia kufungua vituo vya Kiswahili kufikia 44 kutoka 38 nje ya nchi.

Ameongeza kuwa kwa sasa lugha ya Kiswahili imeanza kutumika kwa watu takribani 50 milioni duniani na kwamba Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo Bara wanaendelea kushirikiana na Wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo Zanzibar kuendelea kutekeleza mikakati ya kukikuza na kukiendeleza Kiswahili.

"Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) wewe umekuwa Profesa katika michezo, unayo leseni ya ukocha inayotambuliwa na Caf, haya mafanikio tuliyonayo kwa sasa ni kutokana na wewe, yale madini tunayochota kwako.

"Wizara yangu kwa kushirikiana na wizara Zanzibar tutaendelea kutekekeza maelekezo ya viongozi wetu kuhakikisha lugha hii inafika mbali na kutumika rasmi duniani kama ambayo Rais wetu Samia Suluhu Hassan anavyoelekeza," amesema Waziri huyo.