Mahakama yampa siku 21 Mwakinyo kujibu hoja

Muktasari:

  • Novemba 13, 2023 Mahakama hiyo ilielekeza bondia huyo kupelekewa wito wa kufika mahakamani kupitia gazeti la Mwananchi,  baada ya Mwakinyo kukataa kupokea hati ya wito wa kufika mahakamani iliyowasilishwa kwake na msambaza nyaraka wa Mahakama.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imempa siku 21 Bondia maarufu nchini, Hassan Mwakinyo, kujibu hoja za madai zilizowasilishwa mahakamani hapo na Kampuni ya PAF Promotion.

Hatua hiyo inatokana na Mwakinyo kuiomba Mahakama hiyo impesiku 21 ili aweze kuleta majibu kuhusiana na kesi madai aliyofunguliwa na Kampuni ya PAF Promotion.

Mwakinyo kupitia Wakili wake, Azadi Athumani, alitoa ombi hilo, jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Amiri Msumi, baada ya kuitikia wito wa Mahakama.

Mwakinyo anakabiliwa na kesi ya madai namba 227/2023 aliyofunguliwa na Kampuni ya PAF Promotion, ambayo imewasilisha mahakamani hapo madai nane, likiwemo la kumtaka bondi huyo kuilipa Sh 150 milion ikiwa ni madhara ya jumla waliopata baada ya bondia huyo kushindwa kupanda ulingoni tofauti na mkataba wake aliosaini.

Kampuni hiyo imemfungulia Mwakinyo kesi hiyo baada ya kushindwa kupanda ulingoni katika pambano lililoandaliwa na kampuni hiyo,  lililopangwa kufanyika Septemba 29, 2023 jijini hapa kwa kile alichonukuliwa akisema ni waratibu hao kukiuka masharti ya makubaliano.

Novemba 13, 2023 Mahakama hiyo ilielekeza bondia huyo kupelekewa wito wa kufika mahakamani kupitia gazeti la Mwananchi,  baada ya Mwakinyo kukataa kupokea hati ya wito wa kufika mahakamani iliyowasilishwa kwake na msambaza nyaraka wa Mahakama.

Awali, Wakili anayewakilisha kampuni hiyo, Herry Kauki alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na kuangalia kama taarifa ya wito iliyotolewa kwenye gazeti la Mwananchi imemfikia Mwakinyo.

Wakili Kauki alidai kuwa wamepata taarifa kuwa taarifa imemfikia Mwakinyo na tayari ametuma wakili wake mahakamani hapo.

Kauki baada ya kueleza hayo, ndipo mahakama ilipompa nafasi wakili wa Athuman.

Katika maelezo yake, wakili Athuman kutoka Kampuni ya uwakili ya Cosmic Attorneys, alidai kuwa taarifa ya wito wameipata na ndio maana leo amekuja mahakamani.

Athuman alidai kutokana na hoja zilizotolewa na wadai, anaomba mahakama impe siku 21 ili aweze kuja kujibu hoja zilizowasilishwa na Kampuni ya PAP Promotion.

Hakimu Msumi baada ya kusikiliza hoja za pande zote, alikubaliana na ombi la Mwakinyo na kuahirisha kesi hiyo hadi Desemba 11, 2023 itakapotajwa.

Nje ya mahakama:

Baada ya kesi hiyo kuahirishwa, nje ya mahakama wakili wa Mwakinyo na wakili wa PAP Promotion walikutana na kujadiliana na kwa pamoja wamekubaliana kufanya usuluhishi nje ya mahakama.

"Kama majadiliano yatakwenda vizuri, tutaifahamisha mahakama na tarehe ijayo ya kutajwa kwa kesi, tunaweza kuiondoa kesi hii mahakamani na kuisikiliza nje ya mahakama" alidai Kauki.

Kwa mujibu wa hati ya madai, Kampuni hiyo inaiomba Mahakama hiyo, kwanza itamke kwamba bondia huyo amevunja mkataba wa kupigana.

Pili inaomba Mahakama kumtaka Mwakinyo aombe radhi kwa kuichafua kutokana na kutoa taarifa za uongo kupitia Vyombo vya Habari alivyotumia kuichafua Kampuni na Wakurugenzi wake.

Tatu, PAF inaomba ilipwe fidia ya Sh 142,500,000 kutokana na hasara ya kukosa mapato iliyotegemea kutoka kwa wadhamini.

Nne, inaomba Mahakama imwamuru Mwakinyo arejeshe  Dola za Marekani 3,000 alizopewa kuelekea pambano hilo alilotakiwa kupigana.

Tano, PAF inaomba kurejeshewa Sh 8milioni yakiwa ni malipo ya kulipia ukumbi.

Sita, inaomba kurejeshewa Sh 1,287,500 ikiwa ni gharama za malazi ya mpinzani wa bondia huyo.

Saba, kampuni hiyo, inaomba Mwakinyo kurejeshewa Sh 3,832,000 ambazo ni gharama za tiketi za ndege za mpinzani wake pamoja na wasaidizi wake.

Nane, PAF inaomba Mwakinyo kuilipa kampuni hiyo jumla ya Sh 150milioni ikiwa ni madhara ya jumla waliopata baada ya bondia huyo kushindwa kupanda ulingoni tofauti na mkataba wake aliosaini.