Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maguire beki ghali duniani,kufunga kufuli Trafford

Muktasari:

Jina la Maguire limekuwa kubwa zaidi baada ya fainali za Kombe la Dunia mwaka jana nchini Russia. Ni nani huyu Harry Maguire?

MANCHESTER, ENGLAND . HATIMAYE Manchester United imefanikiwa kuvunja rekodi ya uhamisho kwa walinzi kwa kumnasa mlinzi wa Leicester City, Harry Maguire kwa dau la pauni 80 milioni.

Jina la Maguire limekuwa kubwa zaidi baada ya fainali za Kombe la Dunia mwaka jana nchini Russia. Ni nani huyu Harry Maguire?

Mzaliwa wa Sheffield, aanzia Sheffield United

Jina lake kamili ni Jacob Harry Maguire na alizaliwa katika jiji la Sheffield, Yorkshire nchini England Machi 5, 1993. Maguire alianza kucheza soka katika klabu maarufu ya Sheffield United kama kinda na kisha kwenda katika timu ya wakubwa.

Mechi yake ya kwanza timu ya wakubwa ilikuwa Aprili 2011 katika pambano dhidi ya Cardiff City ambapo katika pambano hilo alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi. Baadaye akacheza mechi nne zaidi, lakini timu hiyo ikashuka kutoka Ligi Kuu kwenda Daraja la Kwanza.

Msimu uliofuata Maguire alikuwa mchezaji wa kudumu katika kikosi cha Sheffield ambapo alifunga bao katika pambano la kwanza la msimu wa 2011-12 dhidi ya Oldham Athletic huku wakishinda mabao 2-0. Baadaye Sheffield waliongeza mkataba wake mpaka mwaka 2015.

Mwishoni mwa msimu alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka na mchezaji bora kijana ndani ya klabu hiyo huku BBC wakimchagua katika kikosi cha msimu cha Ligi Daraja la Pili 2011–12. Msimu uliofuata aliendelea kuwa nguzo katika timu na alifunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Notts County Oktoba 17, 2012.

Mpaka kufikia Februari 2013, Maguire alikuwa ameichezea Sheffield mechi 100 akiwa na umri wa miaka 19 tu. juni 21, 2014 klabu za Hull City, Wolves zilionyesha nia ya kumtaka Maguire huku Wolves wakienda mbali kwa kukataliwa dau la Pauni 1 milioni.

Hull City yamnasa

Julai 29, 2014 Maguire alijiunga na klabu ya Hull City kwa dau la Pauni 2.5 milioni akisaini mkataba wa miaka mitatu. Alicheza mechi ya kwanza kwa Hull City katika pambano la mtoano michuano ya Europa dhidi ya Lokeren ya Ubelgiji ambacho walichapwa 1-0.

Alicheza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Desemba 20 katika pambano dhidi ya Swansea City akiingia dakika 13 za mwisho kuchukua nafasi ya Curtis Davies. Hull City walichapwa 1-0. Hata hivyo, baada ya mechi sita alipelekwa kwa mkopo wa mwezi mmoja kwenda Wigan Athletic ya Ligi Daraja la Kwanza Februari 2015.

Alicheza mechi yake ya kwanza wiki moja baadaye wakishinda bao 1-0 dhidi ya Reading. Februari 28 akafunga bao jingine la kichwa kufuatia krosi ya Jermaine Pennant katika ushindi wa mabao 3-1 ugenini dhidi ya Blackpool. Baada ya kuvutiwa na kiwango chake Wigan waliongeza kipindi chake cha mkopo mpaka mwisho wa msimu.

Wakati akiwa bado kwa mkopo Wigan, klabu yake Mama Hull City ilishuka kutoka Ligi Kuu na kwenda Daraja la Kwanza. Mei 2016 walifanikiwa kurudi tena Ligi Kuu baada ya kushinda bao 1-0 katika pambano la mtoano dhidi ya Sheffield Wednesday kwenye Uwanja wa Wembley. Bao lao lilifungwa na kiungo wa kimataifa wa Mali, Mohamed Diame.

Msimu wa 2016–17, Kocha wa Hull, Mike Phelan alimfanya Maguire kuwa mchezaji wa kudumu katika kikosi cha kwanza cha klabu hiyo. Alifunga bao lake la kwanza katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Bristol City Kombe la Ligi Oktoba 25, 2016.

Maguire alikuwa nahodha katika ushindi wa Hull City wa mabao 4-2 dhidi ya Middlesbrough Aprili 5, 2017. Siku hiyo alifunga bao la kwanza. Mwishoni mwa msimu Hull ilishuka daraja tena lakini Maguire alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka.

Atinga Leicester City, atamba

Juni 15, 2017, Maguire alinaswa na klabu ya Leicester City kwa dau la Pauni 12 milioni ambalo lingepanda mpaka Pauni 17 milioni kutokana na kiwango chake. Alisaini mkataba wa miaka mitano. Alicheza mechi yake ya kwanza Agosti 11 huku Leicester wakichapwa 4-3 na Arsenal.

Siku tu baadaye aliifungia Leicester bao la kwanza katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Brighton akiunganisha kwa kichwa mpira wa kona wa Riyad Mahrez. Msimu wa 2017-18 alicheza kila mechi na kuchaguliwa kuwa mwanasoka bora wa msimu wa klabu.

Katika dirisha kubwa la mwaka jana, United walimsaka vilivyo Maguire baada ya staa huyo kutamba katika michuano ya Kombe la Dunia na kikosi cha England pale nchini Russia. Hata hivyo, kocha Claude Puel aliwathibitishia mashabiki wake kwamba staa huyo atabakia klabuni.

Msimu ulioisha Maguire aliendelea kutamba katika kikosi cha Leicester City ambacho kilikuwa kinawapa wakati mgumu vigogo na katika dirisha hili United wameamua kuvunja rekodi ya uhamisho ya klabu kwa kutoa dau la Pauni 85 milioni kumnasa Maguire baada ya dau la kwanza la Pauni 70 milioni kukataliwa.

Atesa kombe la dunia Russia

Maguire ameichezea England katika ngazi zote za soka la vijana akianzia katika kikosi cha chini ya umri wa miaka 21 ambapo Novemba 2012 aliitwa katika kikosi kilichokuwa kinajiandaa kucheza na pambano la kirafiki dhidi ya Ireland Kaskazini.

Katika pambano hilo aliingia uwanjani dakika ya 60 kuchukua nafasi ya Andre Wisdom huku England wakishinda mabao 2-0 katika Uwanja wa Bloomfield Road. Agosti 24, 2017 kocha wa England, Gareth Southgate alimuita Maguire kwa mara ya kwanza katika kikosi cha wakubwa kwa ajili ya kujiandaa na mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2018 dhidi ya Malta na Slovakia.

Alicheza mechi yake ya kwanza kwa England dhidi ya Lithuania wakishinda 1-0 na kutinga katika michuano ya Kombe la Dunia. Maguire alichaguliwa katika kikosi cha wachezaji 23 wa England ambacho kingeshiriki michuano hiyo nchini Russia. Alikuwa beki wa kudumu katika kikosi cha Southgate ambapo alipika bao la ushindi la Harry Kane dhidi ya Tunisia. England ilishinda 2-1. Akafunga bao lake la kwanza kwa England Julai 7, 2018 katika pambano la robo fainali dhidi ya Sweden ambapo aliunganisha mpira wa krosi wa Ashley Young. England walishinda 2-0.