Mafunzo yaing'oa Mwembe Makumbi kileleni ZPL baada ya miezi mitatu

Muktasari:
- Mwembe Makumbi iliyokaa kileleni mwa Ligi Kuu ya Zanzibar kwa takribani miezi mitatu, imeng'olewa baada ya Mafunzo kushinda jioni ya leo.
MAAFANDE wa Mafunzo imetwaa usukani wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) baada ya kuibamiza Uhamiaji bao 1-0, kwenye Uwanja wa Mao B, mjini Unguja.
Mafunzo iliyocheza mechi 24 kwa sasa imefikisha pointi 47, moja zaidi na ilizonazo waliokuwa vinara wa ZPL Mwembe Makumbi yenye pointi 46 iliyocheza mechi 23.
Maafande hao sasa wamebakiwa na mechi sita kuhitimisha msimu dhidi ya Zimamoto, Malindi, JKU, Mwembe Makumbi, Junguni na Chipukizi.
Mafunzo imeing'oa Mwembe Makumbi iliyopanda daraja msimu huu iliyokaa kileleni takribani miezi mitatu.
Bao liliizamisha Uhamiaji, lilifungwa na Said Etoo dakika ya nane na kudumu hadi mwisho wa pambano hilo, lililokuwa na ushindani mkubwa kwa timu zote.
Katika mechi nyingine uliopigwa Mao A, Maafande wa JKU iliipigishwa kata Mabaharia wa KMKM kwa mabao 2-0.
Bao la mapema liliwekwa kimiani na Yakoub Amour dakika ya nane ambalo limedumu hadi mapumziko kabla ya Freddy Suleiman kupachika la pili dakika ya 54 na kuifanya JKU kufikisha pointi 43 katika mchezo 24.
Sambamba na hayo, mechi zilizoshindwa kuendelea jana Alhamisi kutokana na mvua kubwa iliyonyesha visiwani hapa, zilipigwa saa 4 asubuhi ya leo Ijumaa.
Mechi hizo zilipigwa kwa dakika 45 za kwanza kabla ya kuahirishwa na leo viporo hivyo vilimalizwa kwa Mlandege kulala 1-0 mbele ya JKU, huki Inter Zanzibar ikinyukwa mabao 3-2 na New City iliyofikisha pointi 22 na kuzidi kujiweka pazuri kukwepa janga la kushuka daraja.
Inter Zanzibar na Tekeleza zilizopanda daraja msimu huu tayari zimeshashuka mapema kutokana na idadi ya pointi ilizonazo.