Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mafua, homa tishio Ligi Kuu Bara

HALI za kiafya kwa wachezaji wa baadhi ya timu za Ligi Kuu Bara imeibua hofu baada ya mchezo wa Simba na Kagera Sugar uliotakiwa kuchezwa Desemba 18, kuahirishwa kutokana na baadhi yao kuugua mafua na vifua.

Simba leo inatarajia kuondoka Dar es Salaam kwenda Tabora ambako itacheza na KMC ambao ni wenyeji ingawa hadi jana mabosi walikuwa na kikao juu ya safari.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya viongozi wa klabu hizo walieleza hali kutokuwa shwari kwa wachezaji na wengine wakiwekwa kwenye uangalizi.

Uongozi wa Yanga ulithibitisha kuwa hali si shwari ndani ya kikosi chao na kuweka wazi kuwa benchi zima la ufundi pamoja na wachezaji wanasumbuliwa na mafua makali na kikohozi.

Meneja wa klabu hiyo, Hafidh Saleh ambaye alipoulizwa na gazeti hili juu ya hali za wachezaji waliokuwa wanaumwa ndani ya timu aliweka wazi kuwa si wachezaji pekee, bali hadi benchi la ufundi.

Alisema wachezaji wapo kambini kwa ajili ya uangalizi wa karibu na kama wataamka vizuri leo wataanza mazoezi kujiandaa na mchezo wa ligi dhidi ya Biashara United utakaochezwa Jumapili. “Hali sio nzuri kwa timu nzima hadi benchi la ufundi. Taratibu za matibabu zinaendelea, kesho (leo) mambo kama yataenda sawa asubuhi timu itafanya mazoezi,” alisema.

Katibu mkuu wa Coastal Union, Rashid Mgweno alisema wachezaji watatu walishindwa kucheza mchezo na Biashara United kutokana na mafua yanayoambatana na homa pamoja na kikohozi. “Wengi walikuwa hawapo kwenye wakati mzuri, ila tunashukuru walipambana na kupata matokeo chanya ingawa ni jambo la kuliangalia kwa jicho la tatu,” alisema Mgweno.

Naye mwenyekiti wa Mtibwa Sugar, Nassoro Aboubakary alisema walisikitishwa na Bodi ya Ligi (TPLB) kushindwa kusogeza mechi yao ya jana dhidi ya Polisi Tanzania kwa kile alichodai wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza wanaumwa mafua na wamejitenga.

“Tuliambatanisha ripoti nzima ya mganga mkuu wa Mkoa wa Morogoro kwenda TPLB, lakini bahati mbaya tumeambiwa tucheze hivyo hivyo na sehemu ambayo kuna upungufu tuwaongeze wachezaji chini ya miaka 20, kitu ambacho kimetusikitisha sana,” alisema Nassoro.

Vilevile taarifa zilieleza kuwa kipa Metacha Mnata na wachezaji watano wa Polisi Tanzania jana walishindwa kusafiri kwenda kucheza na Mtibwa Sugar kutokana na kukumbwa na changamoto hiyo.

Kwa upande wake, ofisa habari wa Biashara United, Ben Bago alisema wanasubiri taarifa mpya ya daktari baada ya mchezo na Coastal Union kwisha kwani hakukuwa na mchezaji aliyekuwa anasumbuliwa na tatizo hilo.

Katika timu ya Azam FC, ofisa habari, Thabit Zacharia ‘Zaka Zaka’ alisema tangu mechi iliyopita kikosi chao kilikuwa na wachezaji zaidi ya watano waliokuwa wanasumbuliwa na hali hiyo, ingawa baadhi walicheza lakini kati yao hawakumaliza kwani hali ilikuwa si nzuri na waliomaliza baada ya mechi walilazimika kurudishwa hospitali.

“Wachezaji kama Idris Mbombo, Paul Katema, Wilbol Maseke na Zubeir Foba pamoja na Prince Dube bado wanaumwa mafua na homa na baadhi yao walicheza mechi iliyopita,” alisema Zaka.

“Wengine waliokuwa wanaumwa na wameanza mazoezi ni Zulu (Justine), Sospeter (Bajana), (Nicolaus) Wadada, Fini, Frank Domayo, Amoah (Daniel) na Kola (Rogers), lakini namna gani tutafanya ni suala la viongozi wa juu pengine wanaweza kuwasiliana na Bodi ya Ligi kama hali hii itaendelea kuwa mbaya. Vinginevyo waliopo wanaendelea na mazoezi kwa ajili ya mechi ijayo na Ruvu Shooting.”

Kocha mkuu wa Mbeya City, Mathias Lule alisema hakuna mchezaji mwenye tatizo kiafya na kwa sasa wanajiandaa na mchezo dhidi ya Coastal Union.

Daktari wa Mbeya Kwanza, Stanley Kayombo alisema hadi jana wachezaji wote na benchi la ufundi walikuwa salama kiafya wakijiandaa na mechi ya leo dhidi ya Kagera Sugar ingawa alisisitiza kuchukua hatua zote za kiafya zinazotakiwa ikiwemo kuvaa barakoa na kunawa na maji tiririka.

Kocha wa Namungo, Hemed Suleiman ‘Morocco’ alisema katika timu yake pia kuna tatizo hilo, lakini alisisitiza kuwa lazima mechi dhidi ya Dodoma Jiji itakayochezwa Ilulu, Lindi leo itachezwa.



(Imeandikwa na Olipa Assa, Charity James, Saddam Sadick na Daud Elibahati)