Maelfu wamzika Maradona

Friday November 27 2020
maradona pic

WAKATI ulimwengu wa soka ukiwa umejawa na huzuni kufuatia kifo cha mkongwe wa tasnia hiyo duniani Diego Armando Maradona aliyefariki Jumanne wiki hii, maelfu ya waombolezaji jana Alhamis walijumuika mjini Buenos Aires Argentina kumuaga na kutoa heshima za mwisho kwa mwanasoka huyo.

Maradona alifariki kwa kile  kilichoelezwa ni kupatwa na shambulio la moyo wiki mbili na baada ya kuruhusiwa kutoka  kwenye moja ya hospitali nchini kwao Argentina alikokuwa akipatiwa matibabu hali ilibadilika.

Katika shughuli ya kumuaga nguli huyo, kuliwepo na viongozi mbalimbali wa Serikali, soka, wachezaji na mashabiki wa soka ambao wengi wao walikuwa wamevalia Fulana za rangi ya bluu na nyeupe zilizochapishwa namba 10 na jina la Maradona kama kumbukumbu na heshima kwa mwanasoka huyo aliyetangulia mbele za haki.

Sambamba na hilo timu na mashirikisho mbalimbali ulimwenguni zimeonekana kutoa salamu za rambirambi kwa familia ya Maradona wakionesha ni kwa namna gani alichangia kwenye ukuaji na maendeleo ya soka ulimwenguni kwa ujumla.

Nahodha wa sasa wa Argentina, Lionel Messi ambaye  ndiye anavaa jezi namba 10 iliyokuwa ikivaliwa na mwanasoka huyo ameonesha masikitiko yake kufuatia kifo cha Maradona na kuandika kwenye kurasa yake ya Instagram maneno haya;

"Ni siku mbaya sana na ya kukumbukwa kwa wanasoka na Argentina kwa ujumla, ametutoka kimwili lakini bado tupo naye kiroho, nakumbuka nyakati zote tulizokuwa pamoja naye na nitumie nafasi hii kutoa salamu zangu za pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wote wa Maradona," 

Advertisement

Wakati wa uhai wake Maradona aliwahi kuchezea klabu za Barcelona, Napoli, Argentinos Juniors, Boca Juniors,  Sevilla na Newell's Old Boys kwa nyakati tofauti tofauti pamoja na timu ya taifa ya Argentina ambapo baadae alikuja kuwa kocha wa timu hiyo. 

Dunia itamkumbuka  Maradona kama Bingwa wa Kombe la Dunia mwaka 1986 akiwa na timu ya taifa ya Argentina pia kama mchezaji aliyekuwa na uwezo mkubwa wa kukimbia na mpira na kucheza soka kwa ujumla.

Licha ya waombolezaji wengi kufurika kwenye mji wa Buenos Aires kumuaga Maradona lakini ni familia na marafiki wa karibu wachache walioruhusiwa kuingia kwenye eneo la Jardin Bella Vista Cemetary kufanya mazishi ya mwanasoka huyo ambaye amezikwa jana pembeni ya makaburi ya wazazi wake Dalma (Mama) na Diego (Baba).

Maradona amefariki akiwa na umri wa miaka 60 na mazishi yake yamefanyika nchini kwao Argentina.

Na RAMADHAN ELIAS

Advertisement