Machupa atoa neno Kariakoo Dabi

Muktasari:

  • Machupa ambaye aliichezea Simba kuanzia 1999-2011 amesema kwa uzoefu wake wa kucheza dabi nyingi, matokeo ya mechi hiyo yanakuwa ya kushangaza tofauti na matarajio ya wengi na ndio sababu ya watu kuzimia uwanjani na wengine kupoteza maisha.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Athuman Machupa, ameizungumzia Kariakoo Dabi ya Aprili 20, anaiona itaamuliwa na ukomavu na mbinu za mastaa na makocha wa klabu hizo kongwe.

Machupa ambaye aliichezea Simba kuanzia 1999-2011 amesema kwa uzoefu wake wa kucheza dabi nyingi, matokeo ya mechi hiyo yanakuwa ya kushangaza tofauti na matarajio ya wengi na ndio sababu ya watu kuzimia uwanjani na wengine kupoteza maisha.

"Presha ya dabi ipo kwa mashabiki na viongozi, hao ndio wanaoweza kuwajenga wachezaji ama kuwatoa mchezoni, kutokana na maneno wanayokuwa wanawaambia," amesema na kuongeza;

"Timu unayoiona ipo vizuri ndio inayoweza kupoteza mechi ama ikashinda, kifupi dabi ni dabi hao ni watani wa jadi, kikubwa wachezaji wajipange kutetea nembo zao."

Machupa ambaye baada ya kutoka Simba alikwenda Sweden kuichezea klabu ya Vasaluns mwaka 2011, amesema dabi zinapandisha thamani ya mchezaji au kumshusha, kulingana na kiwango anachokuwa anakionyesha.

"Japokuwa kuna tofauti ya zamani na sasa kila kitu kimebadilika, umuhimu umebakia palepale wa kushinda mechi, maana nyakati zetu gate collection (mapato ya mlangoni) na ahadi chache zilikuwa zinatupa mzuka, ila sasa wanaahidiwa mamilioni ya pesa," amesema.