Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Machupa atangaza viongozi wapya Simba,amgeuka Aveva

Muktasari:

“Kwa sasa Simba hakuna viongozi, naamini wale waliotakiwa kuongoza Simba wapo wengi sana kama Suleiman Yelstin (aliwahi kuwa katibu mkuu) na Hayaz Mruma (aliwahi kuwa mwenyekiti), hao ni baadhi ya watu wanaoweza kuisaidia Simba kuvuka hapo ilipo na siyo hao waliopo sasa, Simba inatakiwa kuwa na viongozi wenye misimamo mikali kwa maendeleo ya klabu.”

KUNA mastraika ambao huwezi kuzungumzia historia ya Simba ukawaacha. Athumani Machupa ni mmoja wao. Ameifanyia Simba mambo ya maana kwenye Ligi ya ndani pamoja na michuano mbalimbali ya Kimataifa.

Ni aina ya mchezaji ambaye alikuwa akijua umuhimu wake na maana ya nafasi aliyopewa na kocha wake. Mashabiki wa Simba walimheshimu kwa vile alikuwa akijituma kila sekunde uwanjani, ni aina ya wachezaji waliokuwa na vipaji halisi vya soka, alikuzwa kwenye klabu maarufu ya Friends Rangers yenye maskani yake Magomeni Kagera jijini Dar es Salaam.

Simba ilimsajili mshambuliaji huyo msimu wa 1999 na aliichezea timu hiyo kwa misimu minane mpaka pale alipoamua kwenda kucheza soka la kulipwa nchini Sweden mwaka 2007 ingawa kuna wakati alikwenda kujaribu bahati nchini Dubai kati ya mwaka 1999 na 2002.

Kwa sasa mchezaji huyo bado yupo nchini Sweden anafanya shughuli zake binafsi baada ya kumaliza mkataba wake na timu ya Armeinska Syrianska inayoshiriki Ligi Daraja la Pili. Mwanaspoti limefanya mahojiano na mshambuliaji huyo ambaye ameelezea mambo mbalimbali ya soka lake pamoja na soka la Tanzania ikiwemo mwenendo wa timu yake ya zamani ya Simba na akasisitiza uongozi wa sasa ni tatizo.

“Kwa sasa Simba hakuna viongozi, naamini wale waliotakiwa kuongoza Simba wapo wengi sana kama Suleiman Yelstin (aliwahi kuwa katibu mkuu) na Hayaz Mruma (aliwahi kuwa mwenyekiti), hao ni baadhi ya watu wanaoweza kuisaidia Simba kuvuka hapo ilipo na siyo hao waliopo sasa, Simba inatakiwa kuwa na viongozi wenye misimamo mikali kwa maendeleo ya klabu.”

 

Amzungumzia Aveva

“Uongozi wa Aveva kwa ukweli umefeli kwa sababu viongozi wengi katika uongozi wa sasa hawaelewi soka, hawajui nini maana ya soka, nini thamani ya mchezaji, kifupi wengi hawajacheza soka ndiyo maana wanaendesha timu ili mradi iende tu.

“Nakerwa sana na matokeo mabovu wanayoyapata Simba kwa sasa, inaonekana hakuna kinachoeleweka ndani ya Simba na ndiyo maana najaribu kuelezea hisia zangu kupitia mitandao mbalimbali kwamba wataona na kuyafanyia kazi yale watakayoona yanafaa. Simba ya sasa imepoteza mwelekeo siyo ile yenye ushindani ambayo ilikuwa hata ikifungwa ni lazima wapinzani wafanye kazi ya ziada.

“Kama napata bahati ya kukutana na kuzungumza na Aveva nitamshauri kuendesha klabu kisasa na si kama miaka 20 iliyopita, hii ni karne ya kisasa. Kwangu Aveva ni msimamizi tu mzuri ila si kiongozi mzuri, kiongozi mzuri ni yule mbunifu ambaye nilitarajia kuwa ataibadili Simba kutoka tegemezi ya wafadhili na kujitegemea kwani Simba inaweza kujiendesha pasipo kumtegemea mtu,” anaelezea.

 

Simba kurudi katika ubora

Machupa anasema kama Simba inataka kurudi katika bora wake, mabadiliko yafanyike kuanzia ngazi ya utawala, “Baadhi ya wachezaji wa Simba nawafahamu ni wazuri, ila kiutawala Simba inaharibiwa na viongozi waliodumaa kifikra na kimtazamo, tunahitaji sura mpya katika uongozi, lakini kama mabadiliko yatafanyika, inaweza ikaleta ari mpya na kufikia mafanikio yetu japo si makubwa ila yataheshimika sana.”

“Kipindi chetu timu ilikuwa na mchanganyiko wa wachezaji, damu changa walikuwepo lakini ilikuwa mpaka ujitume sana ndipo upate nafasi, vinginevyo haikuwa rahisi, hicho ndicho kitu pekee kilichosaidia kutufikisha pale kila mmoja alijua jukumu lake ni lipi, tulijitambua na kuwa na malengo,”

“Ili Simba irudi kucheza michuano ya kimataifa, viongozi wa Simba waache ubabaishaji na hasa wakati wa usajili ili waweze kutengeneza timu nzuri, timu yetu ilikaa muda mrefu pamoja na aliyesajiliwa basi ujue timu nzima ilikuwa inamkubali kiuwezo na si kusajili kwa matakwa ya kiongozi,” anasema Machupa.

 

Timuatimua ya makocha na wachezaji

“Kutimua makocha ni sahihi kwa sababu klabu inasaka mafanikio, sasa mwenendo ukiwa mbovu lazima wafanye mabadiliko tena ya haraka ili kunusuru timu lakini kufukuza wachezaji siyo sahihi kwa sababu viongozi ndiyo wanaowasajili wachezaji bila matakwa ya kocha ama benchi la ufundi.

 

Soka limeshuka

“Nafuatilia kwa karibu soka la Bongo lakini kwangu naona limeshuka sana kwa sababu timu hazichezi kwa viwango vyao, wengi wanategemea kununua mechi na kuhonga waamuzi, hata mafanikio kwa nchi kwa jumla hatujafanikiwa kwani soka linazidi kushuka kuanzia kwenye klabu. Kitu pekee kinachoweza kunusuru soka Tanzania ni kuwa na misingi imara kuanzia chini, wanaopokea na kutoa rushwa wakikamatwa wachukuliwe hatua kali, hapo naamini tunaweza kupiga hatua,” anaeleza.

 

Akumbuka ubingwa wa 2003/04

Machupa anasema aliichezea Simba katika michuano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa na mchango wake ulionekana pale alipoifanya Simba kutwaa ubingwa mbalimbali, lakini tukio moja kati ya yote anayoyakumbuka katika maisha yake ni kutwaa ubingwa wa msimu wa 2003/04.

“Matukio mengi sana yalitokea kwa wakati huo ila moja ambalo siwezi kulisahau ni pale tulipotawazwa mabingwa wa Ligi Kuu kabla msimu wa 2003/04 haujaisha. Wachezaji wote tuliofanikisha hilo tulijitambua na tulikuwa na lengo moja tu,” anasema Machupa.

 

Ushirikina

“Imani za kishirikina zipo kila mahali, ingawa binafsi huwa siamini mambo hayo japo pia sikatai kama hayafanyiki, ila ni imani tu na si kwamba yanaleta ushindi. Hata kwa wachezaji kuwa wanalogana napo kupo sana katika timu ila huwa hayafanyi kazi kama watu wanavyodai, dawa ya ushindi na mafanikio ni mazoezi, kujitambua kile unachofanya na kusikiliza malekezo ya kocha tu,” anasema Machupa.

 

Wachezaji wa kigeni

Machupa anasema hakuna haja katika kikosi kujaza wachezaji wa kigeni, ni vyema ufanyike utaratibu wa kuwatumia wachezaji wasiozidi wawili ili wazawa wapewe nafasi.

“Wachezaji wa kigeni hawana msaada sana kwa sababu hakuna tofauti kubwa kati yao na wazawa, kwangu wawili tu wanatosha kucheza kikosi cha kwanza, wapewe nafasi wazawa, naamini wanaweza ila viongozi hawawathamini na kuwaamini tu,”.

 

Viongozi kusajili wachezaji

“Usajili wa Tanzania unafanywa kiholela sana, makocha hawana nafasi ya kutoa mapendekezo yao na hata yakitolewa hayafanyiwi kazi, ndiyo maana hata kwenye uamuzi wa kutimua wachezaji wanaotoa ni viongozi wenyewe na si kocha, hivyo katika suala la usajili bado litazisumbua sana timu za Tanzania kupata wachezaji ambao si sahihi kwa matumizi ya wakati huo,” anasema Machupa.

 

Makocha wa Kizungu

“Sisi hatukufundishwa na Wazungu, lakini napenda kusema kwamba makocha wa Kizungu wanafaa ila waletwe kwa manufaa ya Simba na si ya mtu binafsi na aletwe mkufunzi wa maana atakayewasaidia kuwapa ujuzi makocha waliolelewa na Simba.”

 

Benchi la Ufundi la Simba?

“Kusema ukweli katika benchi la ufundi kwa sasa namfahamu kocha msaidizi Seleman Matola lakini Simba wanapaswa kumsomesha Matola kama kweli tuna nia ya kweli ya kuifanya Simba isonge mbele, Matola anatakiwa pia kuachana na kunakili afanye kazi kwa mazingira yanayomruhusu.”

Machupa anasema kati ya wachezaji wote waliosajiliwa Simba anaowafahamu ni Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, William Lucian ‘Gallas’, Said Ndemla, Ivo Mapunda, Shaban Kisiga na Nasoro Masoud ‘Chollo’ ambao hata hivyo alisema bado si wachezaji wa kuiletea Simba mafanikio wanatakiwa kuwa na wachezaji wenye uzoefu.

 

Tofauti ya soka la Tanzania na Ulaya

Machupa anasema kuwa ili soka la Bongo lifikie katika hatua ya kuwa soka la kulipwa, lazima zifanyike jitihada za makusudi kuanzia ngazi ya klabu mpaka shirikisho vinginevyo Tanzania itaendelea kuwa nchi wasindikizaji kwenye michuano ya kimataifa.

“Kuna tofauti kubwa sana ya soka letu na huku, wenzetu wanachukulia soka kama kazi nyingine na wanajali sana wachezaji wao na masilahi pia ni mazuri, ndiyo maana soka lao linakuwa kwa haraka, ukiangalia kwa Tanzania bado hatujafikia hata robo ya mafanikio hata kwa nchi za Afrika tu, bado tuna safari ndefu kufikia malengo ya kimataifa katika soka,” anasema Machupa na kuongeza kuwa katika kipindi chake cha soka kuna mafanikio aliyapata lakini si kipindi alichocheza Simba.

“Kusema kweli nikiwa Simba mafanikio yalikuwa ni ya kawaida tu ambayo siwezi kuyaita kama mafanikio bali kwa upande wangu mwenyewe mafanikio makubwa ni ya kiuchezaji. Hiyo ni tofauti na nilivyoondoka Simba kuja huku ambako naona mafanikio yangu yamepanda, yote hii ni kutokana na juhudi zangu binafsi nilizozifanya nikiwa huku.”

 

Kurudi Tanzania

“Nina mpango wa kurudi nchini wakati wowote, nitacheza soka lakini siyo Simba nitarudi kwenye timu yangu ya Friends Rangers, mpira wa Simba utanishinda kwa sababu viongozi waliopo ni wale wanaopenda kunyenyekewa na mimi siwezi kumsujudia binadamu mwenzangu ndiyo maana nasema nitacheza pale na naheshimika na kuhitajika kama Friends Rangers,” anasema Machupa.

Machupa anasema wachezaji wengi wa Kitanzania wanashindwa kucheza soka la kulipwa kwa sababu walio wengi bado hawajajitambua, hivyo wanaona maisha ya Ulaya ni magumu kwao.

“Wachezaji wa Tanzania wanashindwa kucheza soka la kulipwa kwa sababu wanapenda kulewa sifa za kwenye magazeti pale wanapoandikwa kwa kusifiwa bila kukosolewa, pia watu tofauti wakiwemo viongozi wanawafanya wachezaji washindwe kufanya vizuri kutokana na jinsi wanavyoishi nao.

Mbwana Samatta

“Mshambuliaji Mbwana Samatta peke yake ndiye mchezaji ambaye anaweza kucheza soka Ulaya muda wowote kwa sababu nidhamu yake ni kubwa na uwezo wake ni mkubwa huwezi kumlinganisha na yoyote hapo Bongo kwa sasa na anajitambua. Hao wengine itawachukua muda mrefu sana kufikia mafanikio ya Samatta kwani hawajajitambua,” anasema Machupa.

Machupa ambaye kwa sasa ni mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na timu ya Armeinska Syrianska inayoshiriki Ligi Daraja la Pili, anasema muda ukifika wa kurudi nchini atarudi na atatumia muda huo pia kufunga na ndoa na mama watoto wake.

“Kwa sasa nipo huru kwani nimemaliza mkataba, ila huwa nacheza tu na kufanya shughuli zangu na nafanya kazi katika mgahawa wa kimataifa wa Macdonalds Sweden,” anasema Machupa ambaye ni shabiki mkubwa wa Liverpool.

 

Taifa Stars vs TFF

“Stars ipewe hadhi ya kila mchezaji anayeitwa kuitumikia timu hiyo, kila mchezaji pia aelewe thamani yake na ya timu lakini sijaona sababu ya TFF (Shirikisho la Soka nchini) kuanzisha Stars Maboresho, bado inaonekana hatujajipanga vizuri kuhusu mpangilio wa timu zetu za Taifa, unaweza kuwa na timu 100 za taifa lakini maendeleo hakuna. Hakuna makali ya Stars kwa sasa hiyo yote ni kutokana na mfumo mbovu wa wasimamizi wa timu hiyo, bado safari yetu ni ndefu mno.”

 

Ushauri kwa Juma Kaseja

“Namshauri azungumze na meneja wake amtafutie timu nje aachane na soka la Bongo kwa sasa halina faida kwake tena. Bado ana uwezo wa kucheza kwa kiwango cha juu,”

 

Nafasi ya wazee na wanachama

“Zamani wazee na wanachama walikuwa na nafasi yao lakini soka la sasa haliwahitaji watu wa aina hiyo, soka la sasa ni la kisasa zaidi, wawepo tu kutoa ushauri ingawa sasa hivi mambo yanakwenda vibaya na hatuoni zile busara zao walizokuwa wanatumia miaka hiyo, wamekaa kimya,” anasema Machupa.