Mabosi wa Azam wamtega Ibenge
Muktasari:
- Azam imeweka kambi ya maandalizi ya Ligi Kuu Bara, Kombe la FA na Kombe la Shirikisho Afrika wilayani Karatu, Arusha chini ya Ibenge aliyejiunga nao Julai 5 mwaka huu akitokea Al Hilal ya Sudan.
MABOSI wa Azam FC wamemtega kimtindo kocha mkuu wa timu hiyo, Florent Ibenge baada ya kuweka bayana malengo ya msimu wa 2025-26 kwamba ni kupiga hatua kubwa katika mashindano yote watakayoshiriki badala ya kuzingatia mataji tu.
Azam imeweka kambi ya maandalizi ya Ligi Kuu Bara, Kombe la FA na Kombe la Shirikisho Afrika wilayani Karatu, Arusha chini ya Ibenge aliyejiunga nao Julai 5 mwaka huu akitokea Al Hilal ya Sudan.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Azam, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ akizungumza na Mwanaspoti alisema mipango ya timu ni kuona timu inapiga hatua kubwa katika mashindano yote wanayoshiriki.
Zaka alisema uongozi umepanga kuimarisha ufanisi wa timu, bila kujiwekea shinikizo la kutafuta mataji ambayo mwisho huipa timu presha na kuifanya ishindwe kufikia malengo iliyojiwekea.
“Katika majukumu aliyopewa mwalimu, haizungumzi taji sana, unajua wakati mwingine ni kutengeneza presha isiyo na maana,” alisema Zakazi na kuongeza;
“Sisi tunataka tupige hatua kubwa zaidi ambazo tumewahi kupiga hapo kabla, ndio kitu cha maana ambacho amekabidhiwa kocha Ibenge.”
Pia aliweka wazi msimu uliopita 2024-25 timu ilimaliza Ligi na pointi 63, msimu wa nyuma yaani 2023-2024 ilimaliza kwa 69 na sasa malengo yao ni kuvuka hapo na kufikia angalau pointi 75 au 78.
“Kama tutamaliza Ligi na pointi 79, hata kama hatutakuwa mabingwa, tutakuwa tumepiga hatua kubwa sana, jambo ambalo ndilo tunalenga,” alifafanua Zaka.
Alisema wakati mwingine maendeleo ya timu yanapimwa kwa njia nyingine zaidi na si vikombe pekee, akiwakumbusha mashabiki wa soka nchini, msimu wa 2021/22 Ligi Kuu Engaland, Manchester City na Liverpool zilipambana hadi mwisho zikitofautiana wa alama moja.
Liverpool ilimaliza nafasi ya pili kwa alama 92, huku Man City ikitwaa ubingwa kwa alama 93 baada ya timu zote kucheza mechi 38, ambapo kwa mtu ambaye yeye anapima mataji tu unaweza kusema Liverpool walifeli.
“Ukiwapima kwamba walifeli kwa sababu hawakuwa mabingwa ni jambo jingine, unaweza ukapima hivyo ukaona sawa, lakini ukiangalia maendeleo ya timu unaona ni makubwa.” Sisi tunaangalia hicho kitu zaidi kuliko taji peke yake na tunataka timu yetu ipige hatua kubwa sana kwenye mashindano yote tunayoshiriki,” alisema Zakaria.