Samatta, Msuva walivyotusua ndani ya miaka 20 ya Mwanaspoti

BADO tupo ndani ya mwezi wa Mwanaspoti ambalo limetimiza miaka 20, mwezi huu, tangu lianzishwe 2001. Utaendelea kupata habari makini zinazohusu wanasoka na michezo mingine.

Katika makala hii Mwanaspoti linafichua jinsi lilivyoandika habari za baadhi ya wanasoka wa Tanzania wanaocheza nje kwa mafanikio yanayoonekana na kuwashawishi wapenzi wa mchezo huo kufuatilia ligi za nchi walizopo.

Mwanaspoti limekuorozeshea baadhi tu, wenye majina yenye nguvu katika nchi walizopo.

MBWANA SAMATTA-FENERBAHCE

Wakati Mbwana Samatta anaanza kucheza Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza akiwa African Lyon msimu wa 2008/10, Mwanaspoti lilikuwa na miaka saba, baadaye akajiunga na Simba 2010/11 ambapo ndio ikawa mwisho wa kucheza ligi ya ndani.

Baada ya kutoka Simba, Samatta alijiunga na TP Mazembe 2011/2016 ambako nyota yake ilizidi kung’ara katika mataifa mbalimbali na 2016/2020 alikwenda kuichezea Genk ya Ubelgiji. Mwaka 2020 alinunuliwa na Aston Villa ya England na hapo hakukaa muda mrefu kisha akajiunga kwa mkopo na Fenerbahçe ya Uturuki.

Mwanaspoti ni gazeti lililoongoza kuandika habari za Samatta katika hatua zake za kuchezea timu mbalimbali za nje pamoja na kufichua maisha na ametoka familia ya aina gani.

Nje ya Bongo ni peji inayoeleza maisha ya mastaa wanaocheza soka la kulipwa inayotoka kila Jumatatu katika kurasa za 12, 13 na 14, ambapo gazeti hili liliwapa burudani wasomaji kujua Samatta anafanya nini huko alipo. Halikuishia hapo lilifichua maisha yake nje ya soka, ikiwemo mjengo wake wa kifahari na msikiti alioutoa kwa jamii.


THOMAS ULIMWENGU -TP MAZEMBE

Ndani ya miaka 20 ya Mwanaspoti, Thomas Ulimwengu ni miongoni mwa wachezaji wa kizazi hiki walioandikwa sana kuhusiana na maisha yao ya nje, tangu alipoanza kucheza soka kwenye kituo cha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Lakini kituo hicho kikampeleka kwa mkopo Moro United 2009/2010, baadaye akaenda kujiunga na Athletic FC (2010/11), TP Mazembe (2011/2016), AFC Eskilstuna (2017), Sloboda Tuzla (2017/18), Al-Hilal Club (2018), JS Saoura (2019) kisha akarejea TP Mazembe (2020/21).

Mwanaspoti halikubaki nyuma kuandika habari mbalimbali za anachokifanya Ulimwengu akiwa nje hadi anapoitwa timu ya taifa ‘Taifa Stars’.


SIMON MSUVA-WYDAD CASABLANCA

Saimon Msuva ni kati ya wanasoka wa Tanzania waliondikwa zaidi habari za maendeleo yao nje ya nchi kwa miaka 20 ya Mwanaspoti na ana ushirikiano wa hali ya juu katika kutoa ufafanuzi pindi anapohitajika kufanya hivyo.

Msuva alianza kucheza soka la ushindani akiwa katika timu ya Azam FC (2010/2011) kisha akaenda Moro United (2011-2012), Yanga (2012/2017), Difaa El Jadida (2017/2020) na Wydad Casablanca (2020/21), na ndiye aliyetikisa katika usajili wake kwa mwaka huu.


HIMID MAO-ENTAG EL HARBY

Ni kati ya wachezaji ambao wako ndani ya mafanikio ya miaka 20 ya Mwanaspoti ambapo alianzia katika kituo cha soka cha Elite Academy (2005/2007). Hapo gazeti hilo lilikuwa na miaka sita kisha akajiunga na Azam FC (2008/2018), Petrojet (2018/2019), ENPPI (2019) na sasa anakipiga Entag El Harby ya nchini Misri.


DICKSON KIBABAGE - BERRECHID

Kibabage ni kati ya wachezaji wanaokipiga nje wenye mafanikio yanayoonekana.

Alijiunga na Difaa El Jadida ya Morocco 2019 akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro, lakini timu hiyo ikampeleka kwa mkopo Berrechid ambako anapambana na anapata namba ndani ya kikosi cha kwanza.


KELVIN JOHN - BROOKE HOUSE COLLEGE

Japokuwa umri wake amezidiwa na Mwanaspoti, lakini yupo ndani ya mafanikio ya gazeti hili.

Kutokana na kipaji chake na sasa yupo kwenye kituo cha soka cha Brooke House College ambako alijiunga mwaka 2019, lakini pia ni kati ya wachezaji tegemeo kwenye timu ya taifa ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17.


TIBA JOHN - FC BARIYAS

Kabla ya kujiunga na Baniyas ya Falme za Kiarabu alijiunga na Mfk Vyskon 2019 ambako alisajiliwa beki wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’.

Jo-hn ni kati ya wachezaji wanaopambana nchini humo ambapo katika mechi sita za msimu huu amefunga mabao mawili na kutoa pasi ya bao moja, na anaonekana katika kikosi cha kwanza cha timu yake mara kwa mara.


YOHANA MKOMOLA - Inhulets Petrove

Ni kati ya vijana wa Serengeti Boys waliotamba 2016. Kiwango chake kilifanya Etoile Sportive du Sahel imsajili (2016/2017) ambako hakucheza badala yake alijiunga na Yanga (2017), lakini bado ndoto zake za kwenda kucheza nje hakuzimiza ambapo alijiunga na Vorskla Poltava kwa mkopo (2019/2020). Baada ya kukosa nafasi alikwenda kwa mkopo Inhulets Petrove (2020/21) aliyopandisha daraja.