Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maajabu! Seth Bosco siku, saa ileile na Kanumba

Muktasari:

Kinachoshangaza sasa, Seth amekumbwa na mauti siku na muda ule ule ambao, Kanumba naye aliaga dunia na kumfanya Mama Kanumba, Flora Mtegoa akishindwa hata kuamini

APRIL 7, mwaka 2012 tasnia ya filamu nchini ilipata pigo baada ya aliyekuwa nyota wa fani hiyo, Steven Kanumba kufariki dunia ghafla nyumbani kwake kutokana na ugomvi na mpenziwe Elizabeth Michael ‘Lulu’, lakini miaka saba na ushei mdogo wake, Seth Bosco naye amemfuata.
Kinachoshangaza sasa, Seth amekumbwa na mauti siku na muda ule ule ambao, Kanumba naye aliaga dunia na kumfanya Mama Kanumba, Flora Mtegoa akishindwa hata kuamini.
Seth alikumbwa na mauti jana Jumamosi baada ya kuugua kwa muda mrefu kiasi cha kuwa mlemavu wa miguu akiwa nyumbani kwa Mama Kanumba, Mbezi Temboni jijini Dar es salaam.
Mama Kanumba alisema kama alivyoondoka mwanae Kanumba miaka saba iliyopita ndivyo ambavyo, Seth alivyoaga dunia jana, ingawa sababu ya vifo vyao vilitofautiana.
Akizungumzia safari ya mwisho ya Seth, alisema kilitokea saa 6 usiku wa kuamkia Jumamosi kama ilivyo kwa Kanumba na hata tarehe ya vifo vinafanana kiasi cha kumstaajabisha.
Alisema anasikitika kuwapoteza watoto wake wote hao wote katika umri mdogo, kwani Kanumba alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 28 na Seth akiwa na miaka 32.
“Watoto hawa niliowalea mwenyewe wamefariki dunia saa zinazofanana, kwani hata Kanumba alifariki dunia saa sita usiku, usiku wa kuamkia Jumamosi. Hii inaonyesha namna gani undugu wao ulikuwa wa kushibana na wa kweli,” alisema Mama Kanumba.
Kutokana na msiba huo amewaomba wasanii na wadau mbalimbali kumshika mkono kama walivyofanywa wakati wa msiba wa Kanumba.
“Ukizingatia kuwa  Bosco ni msanii mwenzao na mtoto wao hivyo ni vyema wakamsindikiza katika safari yake hii ya mwisho.
Alibainisha kuwa, angetamani kuusafirisha mwili wa mtoto wake huyo kwenda kuzikiwa Bukoba ambapo ndio nyumbani kwao na kwa mujibu wa mila zao zinataka hivyo, lakini kutokana na kutokuwa na uwezo mpaka sasa hivi hajajua atamzika wapi.
“Bado sijajua kama atazikwa hapa ama Bukoba, ila ningependa sana tungemsafirisha kwani ndio mila zetu,” alisema Mama Kanumba.

KABLA YA KIFO
Mama Kanumba amefichua, kabla ya kukata roho Seth aliomba awekewe filamu ya  marehemu kaka  yake  Steven Kanumba.
“Siku za hivi karibuni, Seth alikuwa akieleza akilala alikuwa akimwona ndotoni Kanumba, kitu ambacho kilikuwa kikimshangaza,” alisema na kuongeza
“Hata hivyo, ilipofika saa 11 jioni ya jana (juzi) Ijumaa aliwaaga kuwa analala na kuwaomba atakapoamka saa 12 jioni wamwekee filamu ya Kanumba kwa kile alichoeleza amemkumbuka sana.”
“Pamoja na Seth kuhitaji tumwekee filamu ya Kanumba, lakini alipolala ndio hakuweza kuamka tena na kutazama filamu, kwani hali yake ilibadilika kwa kuanza kutetemeka mpaka kutulazimu kumwita daktari aliyekuwa akimtibu,” Mama Kanumba alisema na kuongeza;
“Tulijitahidi kuokoa maisha yake kwa kumwita daktari wake, lakini ndio hivyo ilipofika saa 6:30 usiku alifariki dunia,” alisema Mama Kanumba.

UGONJWA
Akizungumzia ugonjwa uliomchukua mwanae, Mama Kanumba alisema  alianza kuumwa kama utani miezi kadhaa iliyopita kabla ya tatizo kuwa kubwa na kugeuka kuwa mlemavu wa miguu hadi  kufanyiwa upasuaji kwenye uti wa mgongo.
Mama Kanumba alisema Seth alianza kuumwa akiwa kanisani, baada ya awalui kuamka mzima na kumuaga anaenda kufanya ibada na kudai  akiwa huko wakati akiinama kufunga kamba ya viatu, akahisi kama kapigwa shoti ya umeme mgongoni na alivyorudi akamwambia na ugonjwa kumganda hadi mauti yalipomfika jana.
“Nimehangaika naye sana Seth, ila Mungu amempenda zaidi, ameanza kuumwa kama utani matokeo yake ikifikia hadi hatua ya kuwa mlemavu wa miguu, tulimpeleka Hospitali mbalimbali lakini ndio hivyo amefariki dunia,” alisema Mama Kanumba.
Kwa sasa mwili wa marehemu huyo aliyekuwa pia ni muigizaji wa filamu akifuata nyayo za Kanumba, umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Baadhi ya filamu alizocheza ni Malaika.