Lusajo atoa sababu kushindwa kutupia makundi Shirikisho

Monday May 03 2021
LUSAJO PIC
By Juma Mtanda

Mshambuliaji na nahodha wa klabu ya Namungo, Reliants Lusajo jana alitupia mabao matatu pekee yake katika ushindi wa bao 3-2 dhidi ya JKT Tanzania na kuipeleka Namnugoi hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Jamaa anajua kufunga na moja ya makosa yaliyofanywa na safu ya ulinzi ya Maafande hao pamoja na mlinda mlango wao, Mrisho Mussa yalitoa nafasi ya kuwaadhibu katika dimba la Jamhuri Morogoro.

Akizungumza na Mwanaspoti Lusajo amesema kuwa walicheza vizuri dhidi ya JKT Tanzania na kumfanya awaadhibu Maafande hao kutokana na uzembe wa walinzi na kipa wao kwa kufunga bao tatu pekee yake zilizosaidia timu yake kuibuka na ushindi wa bao 3-2 lakini kukabidhiwa mpira kutokana na heshima hiyo.

Lusajo alisema kuwa kilichochangia yeye kufumania nyavu mara tatu kimetokana na kucheza vizuri, umoja wa timu huku akieleza kuwa ameshindwa kufumania nyavu hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Afrika kuwa walipitia katika kipindi kigumu katika hatua hiyo.

“Umoja wa timu na tumecheza vizuri dhidi ya wapinzani wetu lakini katika mashindano ya Kombe la Shirikisho tulipitia kipindi kigumu na kushindwa kufunga lakini kwa sasa naamini nitafunga na tutafanya vizuri tukipata tena nafasi katika mashindano ya kimataifa.”alisema Lusajo.

LUSAJO PIC2
Advertisement

Lusajo alitupia bao hizo dakika ya 23 baada ya kipa kuutema mpira ulioelezwa langoni kwake huku bao la pili akifunga dakika 27 wakati bao la tatu alifunga dakika ya 42 huku mabao ya JKT Tanzania yalikwamishwa wavuni dakika ya 71 na Mussa Saidi wakati bao la pili likifungwa na Najimu Magulu dakika ya 88.

Kocha wa JKT Tanzania, Abdallah Mohamed alisema kuwa makosa binafsi ndiyo yaliyopelekea wao kuadhibiwa dhidi ya wapinzani wao.

“Ni makosa binafsi ndio yaliyochangia kupoteza huu mchezo, unaweza kuona mwandishi goli la kwanza na tatu ni makosa binafsi yaliyopelekea streka wao kufunga kirahisi baada ya kipa wetu kushindwa kudaka mpira baada ya kudunda na kumpita kabla ya mfungaji kuuwahi na kufunga.”alisema Mohamed.

Mohamed alisema kuwa bao la pili limetokana na kukosa umakini katika safu ya ulinzi.

“Kazi iliyopo ni kurekebisha makosa ili michezo mingine tufanye vizuri lakini timu imecheza vizuri na hawa JKT Tanzania tutakutana nao tena katika ligi kuu tutajipanga nasi tupate ushindi.’alisema Mohamed.

Kwa upande wa kocha wa Namungo, Hemed Seleiman alisema michezo ya ligi ya ndani imekuwa migumu tofauti na michezo ya kimataifa.

Hemed alisema kuwa kipindi cha kwanza vijana wake walicheza vizuri na kupata mabao matatu lakini kipindi cha pili wachezaji wake walipoteza kujiamini na kutoa nafasi kwa wapinzani kupata bao mbili lakini wanashukuru wamepata ushindi.

“Licha ya vijana wangu kupoteza umakini kipindi cha pili na kutoa nafasi kwa wenzetu kupata bao mbili ilitokana na uchovu lakini walipoteza kujiamini na wana kazi ya kufanya kujiondoka katika msimamo wa ligi kuu kwani sio sehemu salama na tumejifunza kitu katika michezo ya kimataifa.”alisema Hemed.

Advertisement