LONNSTORM : Bongo pagumu lakini kitaeleweka

Muktasari:
Kutoka ofisini kwangu Tabata, Mwananchi ni mwendo kama wa dakika 10 tu kwa basi. Baada ya kuingia katika ukumbi wa hoteli hiyo namwona Mzungu mmoja mrefu hivi kama wachezaji wa mpira wa kikapu, kwa bahati nzuri hakuwa peke yake, alikuwa na bosi wake mmoja anayejitambulisha kwa jina la Jari Hyuarinen.
NI majira ya saa sita mchana hivi, nachomoka ofisini kwa haraka kidogo ili kumuwahi kocha Mika Lonnstrom wa Majimaji. Ananiambia yupo katika hoteli ya Landmark iliyopo Ubungo, Dar es Salaam.
Kutoka ofisini kwangu Tabata, Mwananchi ni mwendo kama wa dakika 10 tu kwa basi. Baada ya kuingia katika ukumbi wa hoteli hiyo namwona Mzungu mmoja mrefu hivi kama wachezaji wa mpira wa kikapu, kwa bahati nzuri hakuwa peke yake, alikuwa na bosi wake mmoja anayejitambulisha kwa jina la Jari Hyuarinen.
Namtazama Mika na kugundua kitu, mwili wake unaonekana kupungua kitu, na hapa namwuliza swali langu la kwanza. Je hali ya hewa ya Tanzania imekukataa?
“Hapana, hali ya hewa ya hapa ni nzuri, nimetembea maeneo mengi na nimeyapenda, Songea ni pazuri, ila Mbeya na Tanga nilipapenda zaidi,” anasema huku akitabasamu.
“Najua umegundua kitu katika mwili wangu, vyakula vya hapa sijui vina tatizo gani, si vibaya lakini najikuta kilo zikipungua kila siku, kwa sasa nimepoteza kilo tano,” anaeleza.
Namtazama Mika safari hii kwa makini kidogo najaribu kumuuliza kama amefikia malengo yake katika mechi 10 za msimu huu ama la, pengine hili linachangia kumpunguza kilo.“Tumefikia malengo, tuliweka mkakati wa kukusanya pointi moja katika kila mechi, ukitazama tumekusanya pointi moja zaidi, tuna pointi 11 katika mechi 10, nadhani sasa ni muda wa kufanya tathmini na kuamua moja,” anasema Mika
Usajili
Hapa nakumbuka kauli ya Fred Mbuna kuwa watoto wa Majimaji hawatoi changamoto za maana, namuuliza Mika kama amepanga kusajili ama ataendelea na hao tu.
“Ni kweli, kikosi changu kina watoto sana na wakati mwingine wanashindwa kuhimili mikiki mikiki ya Ligi, mechi kama ya Simba ilikuwa kubwa sana kwao,” anasema wakati huu akionekana kuwa makini.
“Ukiachana na Fred (Mbuna) na Oddo (Nombo), kipa wetu pekee (David Burhan) ndiye amefikisha miaka 24, wengine wote ni chini ya hapo, wengi ni miaka 20 na 21, ni ngumu kutegemea makubwa kutoka kwao. “Hapa tunatakiwa kuamua moja sasa, kama tunataka tu kubaki katika Ligi basi tunaweza kubaki na wachezaji tulionao, kama tunataka kufanya vizuri ni lazima tusajili wachezaji wazuri watano,” anasema Mika na kuchukua glasi yake ya maji na kunywa funda moja kabla ya kuendelea.
“Nafasi ya ulinzi ndiyo muhimu zaidi, tumefungwa mabao 14, ni mengi sana, tunatakiwa kuimarisha hapo, nataka pia kusajili katika nafasi ya ushambuliaji, bado tumefunga mabao machache.”
Kuuza wachezaji
Wakati nikiwa mjini Songea kabla ya msimu kuanza, nilizungumza na Mika kwa kina na alisema miongoni mwa malengo yake ni kuuza wachezaji kwenda katika timu kubwa, na hili linakuwa swali langu linalofuata.
“Ni kweli, nategemea kufanya hivyo hasa ukizingatia wachezaji wangu wengi ni vijana, lakini hili linategemea pia na malengo ya wamiliki wa timu, kama nitakaa muda zaidi na wakiamua, tutauza wachezaji wengi.
“Mbali na kuuza wachezaji katika timu za hapa, natazama pia fursa za kuwapatia timu Ulaya, ila hili litategemea na usalama uliopo huko na mawakala watakaofanya kazi,” anasema Mika
Namtazama kwa makini na kutamani kumchokoza kidogo, hapa namuulza kama amepata dili la kwenda timu nyingine ama la.
“Nimepata ofa kadhaa za timu za hapa, wamenifata na kutaka nifanye nao kazi, hata hivyo nimewaambia wasubiri kwanza, naheshimu mkataba wangu na Majimaji,” anasema huku akicheka
Mechi za ugenini
Katika kumbukumbu zangu inaonyesha kuwa Majimaji haijashinda mechi yoyote ugenini, namuuliza Mika juu ya hili kama wanakwenda kutalii mikoani ama wanafanyaje.
“Zimekuwa ni mechi ngumu sana kwetu kutokana na umbali, tunasafiri masaa kati ya 60-70 ili kwenda kucheza, tulikwenda Tanga kucheza na Mgambo tukafika jioni na mechi ni kesho, wachezaji hawataweza kufanya vizuri katika mazingira hayo,” anasema Mika na kuishauri TFF itazame upya ratiba hizo ngumu.Hapa namuuliza juu ya Ligi, anaitazamaje ligi ya Tanzania na kama kilichopo na matarajio yake vinafanana.
“Nilishtuka kidogo nilipofika hapa, baadhi ya viwanja ni vibovu sana, watu wa hapa wanatakiwa kuviboresha, ligi itakuwa nzuri zaidi, pia wanatakiwa kuitangaza ligi ili ifahamike zaidi, watu wengi wananiuliza juu ya Ligi ya huku, wanatamani kufahamu,” anasema Mika.
Kombe la FA
Swali langu jingine kwa Mika linakuwa juu ya michuano ya Kombe la FA, namuuliza anaichukuliaje michuano hii na nafasi ya timu yake ikoje.
“Ni michuano mizuri na muhimu zaidi kwa timu ndogo, napenda sana michuano ya mtoano maana ukikomaa katika mechi moja unaweza kusonga mbele, siyo kama ligi ambapo unatakiwa kushinda mechi nyingi.
“Naweza kutazama pia kama nafasi ya kuwachezesha wachezaji wanaocheza mara chache lakini kwangu nitaipa kipaumbele, nitachezesha kikosi changu bora zaidi ili kuwa katika nafasi nzuri,” anafafanua.