LIVE: Serengeti Boys vs Uganda nusu fainali

Dar es Salaam. Namba zinaipa nafasi kubwa timu ya taifa ya vijana wa umri chini ya miaka 17, ‘Serengeti Boys’ kufuzu hatua ya fainali ya mashindano ya kuwania kufuzu Fainali za Afrika mwakani kwa vijana wenye umri huo yanayoendelea jijini.
Rekodi za mechi tatu zilizopita kwenye hatua ya makundi zinaibeba Serengeti Boys mbele ya Uganda ambayo inakutana nao kwenye nusu fainali ya kwanza ya mashindano hayo kwenye Uwanja wa Taifa, kuanzia saa 11.00 jioni.
Serengeti Boys inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na safu imara zaidi ya ulinzi ambayo imeruhusu bao moja tu katika hatua ya makundi huku kukiwa hakuna timu nyingine yoyote iliyofanya hivyo.
Lakini pia Serengeti Boys inashika nafasi ya tatu katika kufumania nyavu hadi sasa na imefunga mabao 11 ikiwa nyuma ya Uganda iliyofunga mabao 17 na Ethiopia ina mabao 13.
Hata hivyo, Ethiopia na Uganda ambazo zilikuwa Kundi B zenyewe zimeonekana kubebwa zaidi na udhaifu wa timu za Djibouti na Sudan Kusini ambazo zilikuwa nyanya kwenye mashindano, zikiruhusu zaidi ya mabao 15 kila moja kwenye mechi zao nne walizocheza.
Kingine kilichozinufaisha Uganda na Ethiopia hadi zikaweza kufunga idadi kubwa ya mabao ni uwepo wa idadi kubwa ya timu kwenye kundi lake ambapo kulikuwa na timu tano ukiziongeza pia Sudan Kusini, Kenya na Djibout wakati Kundi A lenyewe lilikuwa na timu nne tu ambazo ni Serengeti Boys, Sudan, Rwanda na Burundi.
Sifa kubwa inayoibeba Serengeti Boys kwenye mashindano hayo ni muunganiko bora wa kitimu ambao inao unaochagizwa na uwezo wa mchezaji mmojammoja. Hilo limepelekea Serengeti Boys kumiliki mpira na kutengeneza idadi kubwa ya nafasi za mabao kwa muda mrefu jambo linalosababisha timu pinzani iwe nyuma mara kwa mara ikijilinda.
Uimara huo wa Serengeti Boys umekuwa ukibebwa zaidi na safu tishio ya ushambuliaji inayoundwa na wachezaji Kelvin John aliyefunga mabao sita kwenye mashindano hayo na kupiga pasi mbili za mabao hadi sasa pamoja na mwenzake Agiri Ngoda aliyefunga mabao mawili.
Wawili hao wamefunga bao katika kila mechi kwenye hatua ya makundi na ndio wanaotazamwa zaidi kuivunja safu ya ulinzi ya Uganda ambayo inaonekana sio ngumu kupitika.
Lakini uti wa mgongo wa mashambulizi ya Serengeti Boys unajengwa na nyota wawili wanaocheza kwenye safu ya kiungo, nahodha Morice Abraham pamoja na Mustafa Nankuku ambao ndio wamekuwa wakifanya kazi kubwa katika kuichezesha timu na kulinda safu ya ulinzi ya timu hiyo.
Kocha wa Serengeti Boys, Oscar Milambo aliliambia gazeti hili kuwa amewaandaa vyema vijana wake kupata matokeo mazuri kwenye mchezo huo.
“Ninaamini haitokuwa mechi rahisi lakini kwa upande wetu tumejiandaa kucheza dhidi ya timu yoyote ile ambayo iko mbele yetu. Tunawaheshimu Uganda lakini ninaamini vijana watajituma kuhakikisha tunapata ushindi na kufuzu hatua ya fainali ili tubakize kombe nyumbani.
Jambo la muhimu ni kuwaandaa vizuri kisaikolojia vijana ili kutimiza lengo tulilojiwekea,” alisema Milambo
LIVE UPDATES KUTOKA UWANJA WA TAIFA
Mechi inachezwa saa 11 jioni leo Ijumaa...
>Timu zinaingia uwanjani
> Nyimbo za Taifa zinapigwa kwa kila timu
>Dakika ya 2' Tanzania 0-0 Uganda
>Uganda wanapata bao la kuongoza dakika ya 4'
>Dakika ya 11' Serengeti Boys wanasawazisha
>Dakika ya 20' vijana wa Uganda wanaonekana kucheza kwa kasi ili kuhakikisha wanapata bao lakini safu ya ulinzi Tanzania imekuwa makini zaidi
>Serengeti Boys wanagongeana pasi vyema dakika ya 24 hata hivyo wanakosa bao
>Dakika ya 25' vijana wa Tanzania wanafanya shambulizi hata hivyo mpirsa unaishi mikononi mwa kipa wa Uganda
>Mpaka dakika ya 27' Tanzania wamecheza faulo 2 huku Uganda wakiwa wamecheza faulo 5
>Mpaka dakika ya 29' Tanzania hawana offside wakati Uganda wamefikisha 2
>Dakika ya 38' mabao Tanzania 1-1 Uganda
>Dakika 45 za kipindi cha kwanza timu zinakwenda mapumziko
>Timu zimerejea uwanjani na mpira unaendelea kipindi cha pili...
>Dakika ya 76' Uganda wanapata bao la pili
Dakika ya 90+3 Uganda wanapata bao la tatu