Ligi Kuu Bara kuanza Agosti 14
Muktasari:
- Mwanaspoti limepata taarifa za ndani kutoka TPLB kwamba, hivi karibuni kalenda ya matukio kwa msimu wa 2026-2027, ikiashiria mwanzo wa michuano mbalimbali ya soka hapa nchini itawekwa hadharani.
WAKATI ikisubiriwa ratiba ya Ligi Kuu ya NBC kwa msimu ujao 2026-2027 itangazwe ili kila timu ifahamu inaanzia wapi, taarifa kutoka Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) zinasema ligi hiyo inatarajiwa kuanza Agosti 14, 2026.
Mwanaspoti limepata taarifa za ndani kutoka TPLB kwamba, hivi karibuni kalenda ya matukio kwa msimu wa 2026-2027, ikiashiria mwanzo wa michuano mbalimbali ya soka hapa nchini itawekwa hadharani.
Kalenda hii inatoa muongozo kuhusu tarehe muhimu za kuanza kwa Ligi Kuu ya NBC, mashindano ya Kombe la Shirikisho la CRDB, Ngao ya Jamii na michuano mingine.
“Kalenda ya matukio kwa msimu wa 2026-2027 itatoka muda si mrefu na msimu ujao wa ligi utaanza Agosti 14, kutoka kwa kalenda hiyo mapema ni kuzipa timu nafasi ya kujipanga na maandalizi ya kambi zao za msimu,” kilisema chanzo hicho.
Kuhusu kutangazwa ratiba ya Ligi Kuu ya NBC kwa msimu wa 2026-2027, Mtendaji Mkuu wa TPLB, Cornel Barnabas, alisema: “Hivi karibuni tutatangaza kuhusu msimu mpya, tunawashukuru wadau kwa ushirikiano wa msimu uliopita na sasa tunajipanga kwa msimu ujao.”
Katika hatua nyingine, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia alisema kumekuwa na changamoto kwenye ratiba ya Ligi Kuu kutokana na kuathiriwa na mashindano ya Mapinduzi Cup na Muungano Cup, japo mashindano hayo ni muhimu. Karia alisema wamepokea mapendekezo kuona namna gani mashindano hayo yafanyike.
Alisema kutokana na mwakani kuwepo kwa mashindano ya AFCON ambayo yataanza katikati ya mwezi Juni, ni lazima ligi iishe mwezi mmoja kabla ili timu ya taifa ipate muda wa kujiandaa.
Ligi hiyo inayoshirikisha timu 16, msimu wa 2025-2026 ulianza Septeba 17, 2025 na kuhitimishwa Juni 30, 2026 ambapo Yanga ilitwaa ubingwa, Mtibwa Sugar na KMC zilishuka daraja, huku Mbeya City na Tanzania Prisons zikicheza mechi za mtoano kuwania kubaki.
Kwa msimu ujao, tayari Kagera Sugar na Geita Gold zimepanda daraja kutoka Ligi ya Championship kuchukua nafasi ya Mtibwa na KMC, huku Polisi Tanzania iliyoifunga Mbeya Kwanza kwa jumla ya mabao 7-1 katika mtoano wa kuwania kupanda ligi kuu, inakwenda kucheza mtoano mwingine.
Jana Mbeya City ilirudiana na Tanzania Prisons katika mtoano wa kubaki ligi kuu. Mechi ya kwanza Mbeya City ilishinda 2-0, hivyo anayepoteza hapa anakwenda kukabiliana na Polisi Tanzania kusaka timu itakayoshiriki LIgi Kuu ya NBC msimu wa 2026-2027.