Kyombo haoni ugumu kwa Bacca, Mwamnyeto

Muktasari:

  • Singida itakuwa mwenyeji wa Yanga kesho Jumapili kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kuanzia saa 10:00 jioni katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, huku mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa jijini Dar es Salaam Yanga ilipata ushindi wa mabao 2-0.

Mshambuliaji wa Singida Fountain Gate, Habib Kyombo amesema licha ya safu ya ulinzi ya Yanga ikiongozwa na mabeki, Ibrahim Bacca na Bakari Mwamnyeto kuwa na ukuta mgumu, lakini wamepata mbinu za kuipenya na kufunga mabao.

Singida itakuwa mwenyeji wa Yanga kesho Jumapili kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kuanzia saa 10:00 jioni katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, huku mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa jijini Dar es Salaam Yanga ilipata ushindi wa mabao 2-0.

Licha ya kutofunga bao katika mechi sita mfululizo, Kyombo amesema safu yao ya ushambuliaji inayoongozwa na yeye, Dickson Ambundo, Francy Kazadi, Nicolas Gyan na Thomas Ulimwengu imenolewa na kupewa mbinu za kuipa mabao timu yao kesho dhidi ya Yanga.

Timu hiyo imepoteza mechi mbili za ligi na kushinda moja tangu ihamie CCM Kirumba Februari 18 mwaka huu huku ikipoteza mchezo mmoja wa Kombe la Shirikisho na kushinda mmoja.

"Sisi kama wachezaji tumejiandaa vizuri tuna morali nzuri mwalimu ametupa maelekezo mazuri tuko tayari kupambana. Mchezo wa kesho utakuwa mzuri kwetu mwalimu ameshatuandaa vizuri ametupa mbinu tunaamini tutafanya vizuri na kuipa timu matokeo mazuri," amesema nyota huyo wa zamani wa Simba.

"Siyo kweli kwamba safu yetu ya ushambuliaji iko butu, tunaendelea kumpa sapoti mwalimu kwa kuhakikisha tunafanya vizuri katika mechi zinazokuja ili malengo ya klabu ya ajenda 10 za makocha wapya zifanikiwe," amesema.

Kocha Msaidizi wa Singida Fountain Gate, Ngawina Ngawina, amesema kutokana na ubora mkubwa walionao Yanga watakwenda kwa tahadhari kubwa, huku akitamba kuwa wachezaji wanakuwa na shauku ya kufanya vizuri kwenye mechi kubwa kama hiyo hivyo hatumii nguvu kubwa kuwaelekeza bali kuwakumbusha tu vitu vichache.

"Tunajua timu ya Yanga ina ubora, tunaiheshimu, tutakwenda kwa tahadhari kubwa lakini naamini mwenye maandalizi mazuri atapata matokeo. Wachezaji wote wako katika hali nzuri yeyote atakayepata nafasi atatufanyia kazi nzuri," amesema Ngawina na kuongeza;

"Ni mechi kubwa wachezaji wenyewe wanajua haihitajiki kazi kubwa, wanajua nini wafanye wanahitaji kukumbushana tu vitu vichache naamini hawatatuangusha, tunakwenda kupambana ili kupata alama tatu au moja," amesema.